Kila mtu ana hofu katika maisha yake, hofu hizi zinatokana na mazingira mbalimbali yanayotuzunguka.

Tumekuwa tunajifunza njia mbalimbali za kuondokana na hofu, kukabiliana na hofu na hata kuishinda hofu ili isikuzuie kufanya yale ambayo ni muhimu kwenye maisha yako.

Leo tunakwenda kujifunza dawa kamili ya hofu, hii ni dawa ambayo inatibu kabisa hofu. Kwa dawa hii hofu zote ulizonazo zinaondoka kabisa na unakuwa tayari kufanya chochote ambacho umekuwa unataka kufanya.

Mwajiriwa ana hofu kuliko mwajiri, unajua ni kwa nini?

Mtu ambaye anafanya biashara yenye wateja wachache, ana hofu kuliko yule ambaye anafanya biashara yenye wateja wengi. Unapata picha hapa?

Mtu ambaye anafanya kitu kwa mara ya kwanza, ana hofu kuliko ambaye amezoea kufanya kitu hicho kila siku.

Kwa mifano hii ya maisha yetu ya kila siku, tunaona dawa ya hofu ni UHURU KAMILI. Unapokuwa na uhuru kamili kwenye jambo lolote unalofanya, hofu inaondoka. Unapokuwa huru hofu haiwezi kukaa ndani yako, kwa sababu hofu inakaa kwa wale ambao hawapo huru.

Unapokuwa huru kwenye kile unachofanya, kama umejiajiri, unakuwa tayari kufanya makubwa kuliko yule ambaye ameajiriwa, ambaye hana uhuru kamili. Kuna baadhi ya mambo anapenda kufanya na ni muhimu, ila anahofia yasije kupelekea yeye kukosa kazi yake.

Hivyo pia kwenye biashara, kama una wateja wachache unaowategemea kwenye biashara yako, utahofia kufanya baadhi ya maamuzi kwa hofu ya kuwapoteza wateja hao. Lakini unapokuwa na wateja wengi, hofu hii inapungua kwa sababu unakuwa na uhuru.

Ufanye nini?

Kuondokana na hofu, tafuta uhuru kamili. Fanya yale mambo ambayo una uhuru mkubwa wa kuyafanya, utaondokana kabisa na hofu na kuweza kuchukua hatua kubwa kwenye maisha yako.

Siyo maeneo yote unaweza kuwa na uhuru kamili kwa wakati mmoja, hivyo kubali kwenye baadhi ya maeneo utaendelea kuwa na hofu kwenye maamuzi unayofanya. Lakini usiruhusu hili liendelee kwa muda mrefu. Kumbuka kikubwa tunachopigania kwenye maisha yetu ni uhuru, ukishakuwa huru unaweza kuwa na maisha bora.

Njia kuu ya kuupata uhuru kamili ni kuujua ukweli, ukishaujua ukweli na ukachagua kuishi ukweli huo, ni lazima utakuwa huru.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK