Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa kwenye kile tulichochagua kufanya. Tumia muda wako wa leo vizuri rafiki yangu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu ushauri wa bure.
Kwa kuanza kabisa, hakuna kitu cha bure, kila kitu kina gharama yake. Kama gharama haipo kwenye fedha basi itakuwa kwenye muda. Na kama haipo kwenye muda basi itakuwa kwenye utu wako.
Watu wengi wamekuwa wakikimbilia kitu kilichoandikwa BURE, bila ya kujua zipo gharama ambazo zimejificha nyuma ya hiyo BURE.

Sasa leo tuangalie ushauri wa bure,
Hakuna kitu ambacho kinawagharimu watu kama huu ushauri wa bure.
Wanapewa ushauri na watu ambao hawana uelewa wala uzoefu kwenye jambo wanaloshauri, zaidi ya wao kuwa wamesikia.

Ushauri huu unakuja kukugharimu pale unapokutana na changamoto, ambazo hukuzitegemea wakati unaanza. Hapa ndipo unapoanza kuumia.
Ushauri huu huwa unaanza na ule uvumi kwamba kitu fulani kinalipa, au kitu fulani NDIYO HABARI YA MJINI.
Wengi wanakimbilia vitu hivyo na kuishia kuumia.

Ufanye nini?
Ili kuepuka madhara ya ushauri wa bure, unaposikia watu wanasema kitu fulani kinalipa, usikimbilie kufanya, badala yake tafuta watu wenye uelewa, tafuta watu wenye uzoefu na tafuta watu wanaofanya kisha fanya nao mazungunzo. Kwa sababu watu hawa siyo rahisi kuwapata, ni lazima uingie gharama ili kuwapata.
Ukishawapata jifunze kila kitu unachotaka kujua, kisha chukua hatua.

ANGALIZO;
Usije ukatumia hii kama sababu ya kuchelewa kuanza, au kutokuanza kabisa. Hakikisha unapata ushauri bora mapema ili uweze kuchukua hatua mapema.

Nakutakia siku njema sana rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
http://www.makirita.info