Kitu kimoja muhimu unachopaswa kujua kwenye maisha yako ni kwamba hata kama ungekuwa mtu wa aina gani, hata kama ungefanya jambo kubwa na zuri kiasi gani, siyo kila mtu atakubaliana na wewe.
Kama Waswahili wanavyosema, hata ukicheza kwenye maji, wenye husuda watasema unawatimulia vumbi, ndiyo uhalisia wa maisha. Hata kama ukikazana kufanikiwa, wapo watu watakaoangalia kasoro zako na kuzitumia kubeza mafanikio yako. Na kama ukishindwa ndiyo kabisa watu wana kila sababu ya kukusema watakavyo.
Inasemekana kwamba theluthi moja ya watu watakukubali kwa chochote kile utakachofanya, kiwe kizuri au kibaya. Theluthi nyingine moja watakupinga kwa chochote utakachofanya, hata kama ni kizuri kiasi gani. Na theluthi nyingine moja hawatajali hata unafanya nini, yaani hawana muda na wewe.
Sasa unachohitaji wewe kwenye maisha yako siyo watu wa kukukubali au kukupinga, bali unahitaji watu sahihi kwako. Unahitaji watu ambao wanaamini kile unachoamini wewe, wanaokwenda kule unakokwenda wewe. Hawawezi kuwa watu wote, hata kama ungekuwa wa kipekee kiasi gani.
Unatumiaje hili kwenye maisha yako?
Kwenye biashara, siyo kila mtu anaweza kuwa mteja wako. Ila kuna watu ambao ni wateja sahihi kwako. Kuna watu ambao hawatanunua kwako hata kama ungewauzia kwa bei ya hasara. Na wapo watakaonunua kwako hata kama bei ni kubwa. Kikubwa unachopaswa kufanya ni kuwatafuta wale wateja sahihi wa biashara yako, na kuwaridhisha kwa kuhakikisha unatatua matatizo yao na kuwatimizia mahitaji yao.
Kwenye ajira, siyo kila mtu unaweza kufanya naye kazi, siyo kila mtu anaweza kuwa mwajiri wako. Hivyo unahitaji kutafuta watu ambao mnaamini sawa, watu ambao mna uelekeo sawa. Hii itaifanya kazi yako kuwa ya maana kwako. Hakuna kitu kinachosha kama kufanya kazi na watu ambao hamwendani. Wewe unaamini kwenye haki wenzako wanaamini kwenye kuwaumiza wengine.
Na hata kwenye maisha yako, ya familia na hata ya kijamii. Huwezi kuwa na urafiki na kila mtu, na huwezi kwenda vizuri na kila mtu hata ndani ya familia. Hivyo chagua wale watu ambao mnaendana na kisha tengeneza nao mahusiano mazuri. Haimaanishi uwatenge wengine, bali kujua mipaka ili kuepusha matatizo yasiyo na maana kwako.
Usitake kwenda na kila mtu, nenda na watu ambao ni sahihi kwako na maisha yako yatakuwa bora sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK