Mara nyingi uuzaji wa viwanja na majengo huleta faida kubwa na yenye tija kwa muuzaji, huwa ni sehemu ya kukua kiuchumi na kujipongeza kwa kile alichopata kutokana na juhudi zake. Lakini kwa watu wengine hali huwa tofauti sana, huwa ni huzuni na masikitiko kutawala mioyoni mwao. Hata hivyo Lengo la Makala hii ni kukuwezesha kufanya biashara hizi ili upate fedha nyingi zinazotokana na uwekezaji wako kwenye ardhi. Siku zote matokeo ya maamuzi yetu ndio huleta furaha au msongo wa mawazo ndani ya maisha yetu. Watu huamua kuuza viwanja na nyumba zao kwa sababu mbalimbali ambazo huwasukuma kufanya maamuzi hayo, kila mtu huwa na sababu tofauti na mwingine, lakini wengi wao sababu hufanana. Kilichonisukuma kuandika Makala hii ni kuona idadi kubwa ya watu wanaofika ofisini kwetu wana sababu ambazo hazina mashiko mbele ya uso wa dunia ya leo. Binafsi sipendi kuona watu wanapoteza rasilimali zao kwa sababu ambazo hazina tija yeyote. Ingawa wengi wao tumejitahidi kuwabadili mitazamo hasi waliyonayo na kuanza safari mpya yenye matumaini ya ushindi bado naamini wapo wengine wengi kwenye jamii zetu wenye mitazamo hasi kuhusu uwekezaji huu wa ardhi na majengo (Real estate, finance and investment). Yafuatayo ni baadhi ya sababu ambazo hazikubaliki kwenye uwekezaji wa ardhi. 

1. UMEPATA FURSA YA KAZI MJI WA MBALI
Hakuna aijuaye kesho, lakini usemi huu usitufanye tukose tumaini la kesho. Katika hali ya kutafuta ni kawaida ya watu kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa sababu mbalimbali za kimaisha. Sababu mojawapo huwa ni kuhamishwa kikazi au kupata fursa mpya ya kiuchumi sehemu nyingine. Jambo hili huwa ni changamoto kwa baadhi ya marafiki zetu, hujikuta wapo njia panda na wasipate maamuzi sahihi. Marafiki zetu hawa wameshindwa kutambua kuwa hali ya maendeleo ya sasa inatulazimisha watu kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine ili kupata rasilimali uchumi na jamii. Jambo kama hili linapotokea kwako usifanye maamuzi dhaifu, hata unapokwenda huwezi jua kuwa utatumia muda gani au utaishi milele pasipo kutokea fursa nyingine sehemu tofauti ya mji huo mpya. Nyakati za leo lazima uwe na makazi yako rasmi hata kama unafanya shughuli zako sehemu tofauti za miji. Zipo njia mbadala za kukidhi aina tofauti za makazi pale unapopata fursa nje ya mji unaoishi, muhimu ni kutafakari kabla hujafanya maamuzi.

SOMA; Yafahamu Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Kwenye Eneo La Ujenzi Kabla Hujajenga Nyumba Yako 

2. FAMILIA IMEONGEZEKA NA UNAHITAJI NYUMBA KUBWA ZAIDI
Familia nyingi za Kiafrika ikiwemo Tanzania bado tuna utamaduni wa kuishi kindugu, hali hii husababisha mtu anayemiliki uchumi mkubwa tofauti na wengine kulazimika kuwahudumia wale wasio imara kiuchumi. Katika utamaduni huu endapo utajenga nyumba ya kukidhi mahitaji ya familia uliyonayo na mambo mengine ukajimudu vema hali hii huwavutia ndugu wengine kuja kujumuika kupata mahitaji hayo pasipo ukomo wa muda. Hivyo mwisho wa siku utagundua kuwa nyumba uliyonayo imeshindwa kukidhi mahitaji ya ziada kwa ajili ya ongezeko kubwa la wageni ndani ya familia. Katika hali hii watu wengi huamua kutafuta uwezekano wa kutafuta nyumba iliyo kubwa Zaidi kwa kuwa uwezo huo wanao mikononi mwao. Watu hawa wanasahau kuwa mahitaji ya binadamu hayana ukomo milele yote, wanasahau kuwa hata hiyo nyumba atakayo nunua itawavutia wengine Zaidi, gharama ya kukidhi mahitaji ya makazi hayo mapya itaongezeka maradufu siku za usoni na hali ya uchumi hubadilika wakati wowote. Pia itafika wakati nyumba hiyo ataiona ni kubwa pale watoto watakapokuwa shuleni au wameondoka nyumbani kwa ajili ya kujitegemea wenyewe.

SOMA; Faida Za Uwekezaji Wa Majengo Kwenye Maeneo Salama Na Yaliyopimwa Na Wataalam Wa Ardhi 

3. KUTOELEWANA NA JIRANI
“Nahofia sana watoto wangu watachangamana na watoto wa jirani ambao hawana maadili, jirani yangu ni mtata sana na mbaya Zaidi lazima nipite kwake ndipo niingie au kutoka kwangu, sina amani kabisa na jirani yangu, hakika nakosa raha ya maisha.” Hayo ni maneno ya baadhi ya marafiki zetu. Kuna baadhi ya marafiki zetu hufanya biashara ya ardhi na majengo kwa hasara iliyopitiliza kwa sababu za kimtazamo tu. Biashara yoyote lazima itawaliwe na mtazamo chanya wa kiuchumi na si vinginevyo. Na sio kweli kwamba endapo utauza na kuondoka mahali hapo utakuwa umeondoa tatizo na jirani yako na kwamba utakuwa umefanikiwa Zaidi kimaisha. Ni muhimu kubadili mtazamo hasi ulionao dhidi ya wengine na utazame Zaidi fursa za kiuchumi hapo ulipo au unapotaka kwenda. Kuwa chanya kifikra kutakusaidia kufanya maamuzi sahihi tofauti na kuzidiwa na hisia mbaya dhidi ya wengine waliokuzunguka.

SOMA; Ili Upate Mafanikio Ya Kudumu, Wekeza Kwenye Ardhi Na Majengo 

 4. KUONGEZEKA KWA GHARAMA ZA MAISHA
Hali ya maisha ya kiuchumi ni ngumu kutabiri, hii ni kutokana na mfumo wa maisha ya kiuchumi kutegemeana na sera za kisiasa na kijamii. Kila jamii imejiwekea utaratibu wa namna ya kuendesha maisha yao kwa umoja wao, hali hii imesababisha kuwepo na baadhi ya matabaka ndani ya jamii. Watu wengi wamejikuta wakisukumwa kuondoka maeneo yao kwa kuwa wanajiona kuwa wapo tofauti na wengine, hujiona ni wanyonge na wakosefu mbele ya walio imara kiuchumi. Mbaya Zaidi anapokwenda ndio kuna hali mbaya Zaidi kiuchumi na kijamii, anakwenda mahali hakuna umeme, hakuna maji safi na salama, miundombinu ya usafiri ni shida. Kwake ufumbuzi pekee ni kuwakimbia wenye nguvu kiuchumi na sio yeye kujiimarisha kiuchumi Zaidi yao, na anapotarajia kwenda hajui kwamba atatumia nguvu za ziada ili apambane na hali mbaya ya uchumi atakayoikuta. 

5. IMANI MBAYA KUHUSU JAMII INAYOKUZUNGUKA
Ndani ya sayari ya dunia kuna mengi ya kustaajabisha akili ya mwanadamu, mengine hufurahisha na mengine huzunisha nafsi zetu. Ndani ya Tanzania kuna aina mbalimbali za utamaduni ambazo hutumika kuratibu maisha ya jamii. Baadhi ya tamaduni hufanana na nyingi hutofautiana baina ya watu ndani ya jamii zetu. Mara nyingi tofauti hii husababisha Mafarakano yanayotokana na taswira ya wivu, chuki, dharau na fitina miongoni mwa wanajamii. Hili ni tatizo la kifikra linalojenga mtazamo hasi wa imani dhidi ya tamaduni nyingine. Dunia ya leo inamlazimisha mwanadamu achangamane na wengine ili aweze kufanikiwa, lakini wengine wamekwama kutokana na kushindwa kubadili mitazamo yao hasi dhidi ya wengine. Hii isiwe sababu ya kughadhibika na kuamua kuwakimbia ikiwa unapokwenda pia kuna watu kama hao pia.

Yapo makosa ambayo hutakiwi kuyaruhusu kutokea katika maisha yako. Uwekezaji wa ardhi na majengo lazima ukusaidie kukabiliana na hali mbaya ya kiuchumi pale itakapokukabili, uwekezaji wa aina hii unapaswa ukusaidie kutoka kwenye hali mbaya ya kiuchumi na kufanikiwa Zaidi. Ni muhimu kuzingatia hilo kwa sababu maisha tuliyonayo yanategemea yale yote tunayoyafanya. 

Kumbuka hata hivyo wengi wetu kuna wakati tunashindwa kufanikiwa sana kutokana na kuruhusu makosa ya aina hii yatokee katika maisha yetu.

Mwisho kabisa, imani na mitazamo hasi ni chanzo cha watu kutoaminiana na yote kabisa kuogopana na kuchukiana. Upendo haujengwi katika kutiliana mashaka. Mafanikio ya kweli hupatikana kwenye jamii iliyo salama katika hali zote.

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma na mshauri wa ujenzi.
Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888
Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com