Moja ya sababu zinazopelekea watu kukosa vitu wanavyotaka, ni kukosa maarifa sahihi ya kile wanachotaka.

Yaani watu wanajua kabisa ni nini wanataka, ila hawajui njia sahihi ya kupata kile ambacho wanakitaka. Na hii inawapotezea muda kujaribu vitu ambavyo haviwezi kuwapatia kile wanachotaka.

Moja ya maeneo ambayo watu wamepotezwa sana ni eneo la utajiri.

Kila mtu anapenda kuwa tajiri, na hata kama hupendi kutumia neno hilo, basi unapenda kuwa na uhuru wa kifedha. Unapenda kuwa na fedha za kutimiza mahitaji yako bila ya shida.

Lakini ni wachache sana wanaofikia utajiri huo, wengi wanaishia kujaribu mara nyingi lakini wanapoteza muda. Tofauti ya wanaoupata na wanaoukosa haianzii kwenye uwezo wala nafasi, bali inaanzia kwenye kuujua msingi sahihi wa kile unachokitaka.

Kwa mfano, kwenye utajiri, wale wanaofanikiwa na kutajirika kweli wanajua utajiri siyo jambo la kulala masikini na kuamka tajiri. Wanajua utajiri unahitaji muda, na juhudi za kutosha. Wanajua hutajiriki kwa siku bali unahitaji miongo kutajirika.

Lakini wasikilize wale ambao wanashindwa, wasikilize wale walionasa kwenye utajiri, na utaona tofauti kubwa. Wao wanaamini kuna siri imefichwa ambayo wakiijua tu wanatajirika. Wanaamini kuna ‘zali la mentali’ ambalo wakilipata na wao wanatajirika. Wanaamini ipo siku tu na wao watafanikiwa, wanaamini kuna siku wataamka na bahati zao na kupata mafanikio. Wanachofikiria ni kwamba, utajiri wao utakuja ndani ya siku moja.

Kinachotokea sasa;

Kwa wale wanaojua utajiri unachukua muda, wanaweka muda wa kutosha na baadaye wanafanikiwa. Wanakuwa ni watu wavumilivu wanaojua muda ni muhimu.

Ila kwa upande wa pili, kila siku wanajaribu kitu kipya, kila siku wanakimbia na fursa mpya. Wakisikia hiki kinalipa wapo, wakisikia kingine kinalipa zaidi wanaacha kile wanachofanya na kwenda kuanza hicho kipya. Wakisikia mahali kuna njia rahisi ya kupata fedha unawakuta wamejazana. Wanapoteza muda na kuhangaika na mwisho wa siku wanabaki na umasikini wao.

Kuwa na msingi sahihi wa chochote unachotaka, msingi sahihi ndiyo utakaokufikisha kule unakotaka kufika.

Utajiri haupatikani ndani ya siku, bali unapatikana ndani ya miongo. Usijidanganye wala usidanganyike, jua kitu sahihi na tumia njia sahihi kukipata.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK