Kuna mambo mengi kwenye maisha ambayo yamekuwa yanawashangaza wengi. Yaani jambo linatokea na wewe unabaki mdomo wazi kwa sababu hukutegemea jambo hilo litokee.

Mfano wewe ni mwajiriwa na ghafla unafika kazini na kupewa kazi ya kwamba huna kazi tena.

Au wewe ni mfanyabiashara na ghafla unashangaa umepata hasara kubwa kwenye biashara yako. Au umeibiwa kwenye biashara yako.

Au mtu wako wa karibu, ghafla unapata taarifa kwamba amefariki dunia.

Haya ni mambo ya kushangaza sana, ni mambo ambayo mara nyingi yanatuumiza na kupelekea kutaka kukata tamaa na maisha.

Lakini je, ni sahihi kwetu kushangazwa na mambo haya?

Kwa jibu la haraka ndiyo, ni sahihi, kwa sababu hakuna ajuaye kesho inakuja na nini.

Lakini jibu makini ni hapana, hatupaswi kushangazwa na mambo haya.

Kwa nini hatupaswi kushangazwa na mambo haya?

Kwa sababu mambo haya ni sehemu ya maisha, watu wanapata kazi na watu wanakosa kazi. Watu wanaanzisha biashara na watu wanafunga biashara. Watu wanazaliwa na watu wanakufa.

Hivyo badala ya kushangazwa na mambo haya, baada ya kujidanganya kwamba hayawezi kutokea, itakuwa bora kwetu kama tutategemea mambo haya kutokea kabla hata hayajatokea.

Kama umeajiriwa, tegemea muda wowote kufukuzwa kazi hiyo. Kama unafanya biashara tegemea muda wowote kushindwa kwenye biashara hiyo. Na kama kuna mtu unampenda, tegemea muda wowote kumkosa mtu huyo.

Lakini hiyo ni kuwa hasi, si vibaya kuwa hasi?

Swali kubwa utakaloniuliza ni wewe Makirita, kila siku unasema tuwe chanya na siyo hasi, je huoni hii ni kuwa hasi?

Jibu la swali hili ni hapana, sikufundishi kuwa hasi, bali nakufundisha kuwa chanya kupitia hasi. Kwa nini?

Unapotegemea kufukuzwa kazi muda wowote unafanya kazi yako kwa umakini na kujiandaa na maisha bila ya kazi hiyo. Unapotegemea biashara yako kupata hasara unakuwa mwangalifu zaidi kwenye biashara hiyo. Na unapotegemea mtu kufa muda wowote utampa muda zaidi, utamwonesha upendo zaidi na kuhakikisha unatumia kila fursa uliyonayo sasa kuwa karibu na mtu huyo.

Hivyo rafiki, usishangazwe na jambo lolote, tegemea kila jambo kutokea na chukua hatua sasa kabla halijatokea, likishatokea shukuru na songa mbele. Kujaribu kukataa kwamba halijatokea ni kupoteza muda wako na kujichelewesha kufanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK