Wote tunapenda uhuru kwenye maisha, na mafanikio ya kweli yanakuja pale mtu anapokuwa huru. Hata kama utakuwa na kila unachotaka, kama utanyimwa uhuru wa kuwa na yale maisha unayotaka, hutaweza kuyafurahia maisha yako na hii itakufanya usione maana ya mafanikio yako.

Pamoja na hitaji hili kubwa la uhuru, bado watu wengi wamekuwa wanaendelea kutumiwa na watu wengine. Wanatumiwa na wengine na hivyo kushindwa kuwa huru na kufanya yale wanayotaka kwenye maisha yao.
Kuna kitu kimoja ambacho kimekuwa kinawafanya watu watumiwe na watu wengine, kimekuwa kinawafanya watu wawe kwenye gereza la kukosa uhuru wa maisha yao. Kitu hicho ni kukosa NIDHAMU BINAFSI.
Ni hivi rafiki, kama huna nidhamu binafsi, huwezi kuwa na uhuru wa maisha yako, utaishia kutumiwa na wengine, na vibaya zaidi kwa faida zao binafsi. Kwa kukosa nidhamu binafsi utaendelea kuwa chini ya wengine, ukifanya yale wanayotaka wao ufanye, iwe unataka au la.
Tuangalie mifano ya kila siku kwenye maisha yetu;
Utakuwa mwajiriwa maisha yako yote kama utashindwa kuwa na nidhamu binafsi, ya kuweza kuanzisha biashara yako au kufanya uwekezaji wa kuweza kukutoa kwenye ajira hiyo. Au kukufanya usitegemee ajira hiyo kama chanzo pekee cha kipato.
Utakuwa tegemezi kwa mwajiri wako kila siku kama utashindwa kuwa na nidhamu binafsi ya kutumia kipato chako vizuri ili kuweza kujijengea uhuru wa kifedha kadiri siku zinavyozidi kwenda.
Utaendelea kugawana kipato chako na wakopeshaji kila siku kama utashindwa kujijengea nidhamu binafsi ya kudhibiti matumizi yako ya fedha na kuhakikisha matumizi hayazidi mapato yako.
Kama ambavyo umeona rafiki, nidhamu binafsi ndiyo msingi mkuu wa uhuru wa maisha yako. Na kwa kuwa uhuru ndiyo mafanikio ya kweli ya maisha, basi nidhamu binafsi ni msingi muhimu wa kuwa na mafanikio kwenye maisha yako.
Jijengee nidhamu binafsi ili uweze kufurahia uhuru wa maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK