Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo,
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kwenye kile tulichochagua kufanya.
Tumia muda wako wa leo vizuri rafiki, kwa sababu ukishapita, huwezi kuupata tena.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu MCHAKATO na TUKIO.
Vitu vingi ambavyo tunaviona kwa wengine ni MATUKIO, matukio hayo yanatupa sisi hamasa kubwa na kutufanya tuamini tunaweza kufanya makubwa.
Mfano wa MATUKIO…
1. Alianza biashara na mtaji kidogo sasa hivi ni bilionea.
2. Alianza kilimo kidogo kidogo sasa hivi anavuna kiasi kikubwa.
3. Alianza sanaa kiutani utani lakini sasa hivi ni msanii mkubwa.
4. Alianza kazi kwenye nafasi ya chini kabisa na sasa hivi ni bosi mkubwa.
Matukio ni mengi, matukio ni rahisi kuonekana, matukio yanaleta hamasa kubwa.
Kwenye matukio unaona pale mtu alipoanzia na pale alipo sasa, hivyo tu.
Lakini kwenye kila tukio kuna MCHAKATO, hakuna tukio linalotokea hewani, upo mchakato ambao mtu anakuwa amepitia mpaka kufika pale ambapo amefika sasa.
Kila mchakato una magumu yake, ambayo mtu ameweza kuyavuka mpaka akafika alipotaka kufika.
Mchakato ni vigumu sana kuonekana, kwa sababu hakuna mtu anaweza kupoteza muda wake kufuatilia mtu ambaye hata hajulikani anaelekea wapi, na watu hawana uhakika kama atafika anakotaka kufika. Hivyo dunia inapenda matukio, lakini haipendi michakato.
Mfano ya MICHAKATO ni;
1. Alianza biashara, akashindwa, akaanza tena, akapata hasara, akaendelea, akaibiwa, akaanza upya, mshirika wake akamvurudga, akaanza tena, uchumi ukawa mbovu. Hakukata tamaa na sasa ni mfanyabiashara mkubwa.
2. Alianzia kazi ngazi ya chini kabisa, akawa anapenda kujifunza na kujitolea zaidi. Alikuwa mtu wa kwanza kufika kazini na wa kwisho kuondoka. Wakati wengine wanapiga soga, yeye alikuwa akijifunza njia bora za kufanya kazi yake. Wakati wengine wanafanya kwa mazoea, yeye alikuwa anaboresha zaidi. Wenzake wakaanza kumtengenezea visa, akasimamishwa kazi kwa makosa ya kutengenezewa, baada ya uchunguzi kufanyika akarudishwa. Akaendelea kuweka juhudi kubwa na sasa ni bosi mkubwa.
Kwenye kila kikubwa unachoona leo, hakijajikuta pale, upo mchakatonuliopitiwa, ambao siyo rahisi.
Hivyo basi rafiki yangu, usiwe kama kundi kubwa la watu,mla kushangilia MATUKIO, nenda mbele zaidi na ona MCHAKATO ambao watu wamepitia mpaka kufikia tukio hilo. Utajifunza mengi mno unayopaswa kufanyia kazi.
Nakutakia siku njema sana rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
http://www.makirita.info