Hofu ndiyo sumu inayoua mafanikio zaidi ya kitu kingine chochote. Hofu imewazuia watu wengi kufanyia kazi ndoto za maisha yao. Hofu imewatisha watu kuendelea hata baada ya kuwa wameanza. Na hofu imekuwa inatumiwa na watu kuwarudisha wengine nyuma.
Kama huamini hili hebu jiulize wewe mwenyewe, kama usingekuwa na hofu yoyote kwenye maisha yako, je ungekuwa unaishi kama unavyoishi sasa? Je ungefanya kazi au biashara unayofanya sasa? Ungeendesha maisha yako kama unavyoendesha sasa?
Kama utakuwa mkweli na nafsi yako, utakuwa umeona ya kwamba maamuzi mengi ya maisha yako umeyafanya au kuepuka kuyafanya kutokana na hofu fulani. Labda unajua kabisa ajira uliyonayo haitakufikisha unapotaka, lakini huwezi kuacha kwa sababu unahofia maisha yatakua magumu. Unajua kabisa unahitaji kuanzisha biashara, lakini huanzishi kwa sababu unahofu utashindwa au kupata hasara.
Hofu, hofu, hofu ni sumu kubwa, pamoja na kwamba tumekuwa tunaiandikia kila siku, lakini bado tunahitaji mbinu bora zaidi za kuzishinda hofu zetu.
Leo nakushirikisha hofu kuu mbili, ambazo ndiyo zinawarudisha watu wengi nyuma, zinawafanya washindwe kuwa na yale maisha ya ndoto zao.
Hofu ya kwanza ni kutokuwa na uhakika.
Laiti kama angekuwepo anayeijua kesho inakuwaje, tungekuwa mbali sana, si kweli? Hii ndiyo changamoto kubwa ya maisha yetu, hakuna mwenye uhakika kesho itakwendaje. Hakuna mwenye uhakika wa lolote lijalo, sasa ukosefu huu wa uhakika wengine wameutumia kama hofu ya kushindwa kuanza.
Unataka kufungua biashara lakini huna uhakika mambo yatakwendaje, huna uhakika kama utapata faida unayotaka. Na hofu hii inakufanya uone ni bora kusubiri ili usipoteze fedha zako.
Hofu ya pili ni kutokuwa tayari.
Hivi ni nani ambaye amewahi kuwa tayari kwa jambo lolote lile kwenye maisha yake? Wachache sana, mara nyingi huwa hatupo tayari kwa mambo yoyote tunayofanya, lakini hatuna namna, inatubidi tuyafanye tu.
Hii hali ya kutokuwa tayari inaleta hofu ambayo inawafanya wengi kuendelea kusubiri wakiamini kwamba bado hawajawa tayari. Wanasubiri na kusubiri lakini cha kushangaza ni kwamba haifiki wakati wanakuwa tayari.
Ni sawa na mtu anayesema akipata kazi ataanza biashara, anapata kazi lakini haanzi biashara, anasema nikishaanza familia nitaanza biashara. Anakuwa na familia na sasa anasema watoto wakishamaliza shule nitaanza biashara. Watoto wanamaliza shule na anasema nikishastaafu nitaanza biashara. Anastaafu na kupokea mafao yake lakini hawezi kuanzisha biashara aliyokuwa anapanga kuanzisha, kwa sababu kila mara kuna jambo jipya la kufanya.
Ni nini dawa ya hofu hizi mbili?
Dawa ya hofu hizi ni kujitambua, kujua ya kwamba hakuna wakati ambao tutakuwa na uhakika wa kila kitu, na pia haiwezi kufika mahali tukajiona tumeshakuwa tayari kabisa. Muhimu ni kuchukua hatua, kuanza na hatua moja rahisi, na hatimaye kwenda hatua inayofuata. Unaendelea kupiga hatua hivi mpaka unafika unakotaka kufika.
Ndiyo utakutana na changamoto, na ndiyo utahitaji kujifunza mengi zaidi, lakini unajua nini, ANZA SASA, ANZA. Unachohitaji ni kuanza, hata kama huna uhakika, hata kama unajiona hujawa tayari, wewe anza na mengine utaweza kuyafanya kwa urahisi ukishaanza.
Gari iliyopo kwenye mwendo inatumia mafuta kidogo kuliko gari inayoanza mwendo. Anza mwendo sasa, utahitaji mafuta kidogo baadaye kuendeleza mwendo wako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK