Kwenye maisha yetu, tunazo nafasi za kuchagua vile tunavyotaka wenyewe na nafasi nyingine hatuwezi kuchagua wenyewe, tunajikuta tayari tupo kwenye nafasi hizo.
Kwa mfano huwezi kuchagua uzaliwe na wazazi gani, au wadogo na ndugu zako wawe watu wa aina gani. Hawa ni watu wanaokuja na kuwepo kwenye maisha yako bila ya wewe mwenyewe kuchagua. Pia huwezi kuchagua uzaliwe wapi, wewe unajikuta tayari umeshazaliwa kwenye asili fulani. Nafasi hizi tunazopewa kwenye maisha mara nyingi tutaishi nazo maisha yetu yote.
Zipo nafasi nyingine muhimu ambazo tunachagua sisi wenyewe. Nafasi hizi tuna nguvu ya kuchagua nini tunataka na mazingira gani tunataka kuwepo kwa namna tunavyotaka kwenda na maisha yetu.
Kwa mfano una nafasi ya kuchagua marafiki zako wawe watu gani, watu wa aina gani, wenye tabia zipi na mwelekeo gani. Marafiki zako ni watu watakaokuwa na ushawishi mkubwa kwako hivyo ni muhimu kuwachagua kwa umakini.
Una nafasi ya kuchagua mwenza wako kwenye maisha, iwe ni mke au mume. Huyu ni mtu ambaye utatumia muda wako mwingi wa maisha yako pamoja naye hivyo anahitaji kuwa mtu ambaye mnaendana kweli na mnaweza kuvumiliana ili kuwa na maisha bora.
Una nafasi ya kuchagua ni biashara gani ufanye. Na kama umechagua kuwa mfanyabiashara kwenye maisha yako, maana hii ndiyo njia yako ya kuingiza kipato, utakwenda nayo muda mrefu. Ni muhimu uchague biashara ambayo inaendana na wewe ili iwe kitu kizuri kwako.
Una nafasi ya kuchagua mwajiri au bosi wako kwenye kazi. Ndiyo hii ni nafasi yako mwenyewe kuchagua. Kwa kuwa unataka maisha bora, na unapenda kufanya kazi unayofanya, basi unahitaji kuchagua mwajiri wako vizuri. Unahitaji mwajiri anayekwenda kule unakotaka kwenda wewe.
Una nafasi ya kuchagua ni chakula gani ule, hii ni muhimu sana kwa sababu vyakula tunavyokula ndivyo vinajenga au kubomoa afya zetu. Hivyo unahitaji kuchagua kwa makini ili kuwa na afya bora.
Una nafasi ya kuchagua taarifa za kuingiza kwenye akili yako, magazeti ya kusoma, tv za kuangalia na hata mitandao ya kutembelea. Hiki ni kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wako mwenyewe wa kuchagua. Taarifa unazoruhusu ziingie kwenye akili yako zinakujenga au kukubomoa. Chagua kwa makini taarifa ambazo zinakujenga.
Kwa nini nakwambia yote haya rafiki?
- Kwa sababu watu wengi wamejikuta kwenye nafasi ambazo wanafikiri hawawezi kuzibadili, wanafikiri wameshikiliwa pale maisha yao yote.
- Kwa sababu watu wengi wamesahau kwamba sehemu nyingi wanazolalamikia sasa wamechagua wenyewe na siyo kwamba walizaliwa nazo. Kwa mfano mtu anayemlalamikia mwajiri wake, anajisahaulisha kwamba ni yeye mwenyewe aliandika barua ya maombi kwenye kazi hiyo. Na hivyo anaweza kuchukua hatua ya kuachana na mwajiri huyo.
- Kwa sababu watu wengi hawajui kama mtazamo hasi unasambaa kama ugonjwa wa kuambukizwa, kadiri unavyokaa na wenye ugonjwa na wewe ndivyo unavyoupata. Hivyo ni muhimu kuhakikisha wale wanaokuzunguka hawana mtazamo hasi, ambao utakuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Fanya usafi kwenye maisha yako, hakikisha watu au vitu ambavyo umechagua kimakosa unafanya marekebisho ili ubaki na machaguo bora kabisa kwenye maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK