Maisha yetu ni mkusanyiko wa siku tunazokuwepo hapa duniani. Jinsi unavyoishi vizuri kila siku, ndivyo unavyojijengea maisha ya mafanikio. Kama kila siku yako inakwenda hovyo, basi hata maisha yako yote yatakuwa hovyo. Hivyo kabla hata hatujaangalia maisha yako ya miaka 10, 20 mpaka 50 ijayo yatakuwaje kwako, hebu anza kuangalia siku yako moja inakwendaje kwako.

Wanafalsafa wote wanakubaliana kwamba kuishi vizuri leo, ndiyo maisha bora kwako. Kufanya yale uliyopanga kufanya leo, ni maandalizi mazuri ya kesho na hata kama kesho hiyo hutaiona basi utakuwa umekamilisha nafasi yako ya leo.

Kwenye makala yetu ya leo ya FALSAFA MPYA YA MAISHA tutakwenda kujifunza nidhamu tatu muhimu za kujijengea kila siku, ili uweze kuwa na siku bora na mwishowe maisha bora. Tunakwenda kujifunza mambo matatu ya kuzingatia kila siku na kila wakati, na maisha yatanyooka yenyewe.

Unajua kwenye maisha, kuna mambo machache ambayo wewe unapaswa kuyagusa, na yenyewe yanagusa mambo mengine na mengine na mwishowe unaona matokeo makubwa. Kama ilivyo kwenye kuendesha gari au hata mashine yoyote, wewe utahitaji kuwasha gari, kuweka gia na kukanyaga mafuta, ghafla unashangaa gari inaenda, hujui hata nini kimeendelea huko kwenye injini mpaka matairi yanasukumwa kwenda.

Hivi ndivyo maisha yalivyo, kuna mengi huwezi kuyaelezea, lakini ukifanya baadhi ya mambo kwa usahihi, unashangaa kila kitu kinakwenda vizuri. Unashangaa watu uliokuwa unawatafuta wanakuja wenyewe, changamoto zilizokuwa zinakuzuia zinaondoka zenyewe na wale waliokuwa wanakupinga wanaanza kukuunga mkono.

Nidhamu tatu tunazokwenda kujifunza leo, ni sehemu ya hatua chache ambazo mtu ukichukua, zinaleta matokeo makubwa kwenye maisha yako. Ni hatua ndogo unazochukua kila siku, lakini matokeo yake ni makubwa kwako kila siku na kwa siku zijazo pia.

Karibu tujifunze nidhamu tatu muhimu za kujifunza na kujijengea kila siku ili kuwa na maisha bora kila siku.

NIDHAMU YA KWANZA; MTAZAMO.

Kila mtu kuna namna anavyoipokea na kuichukulia dunia inayomzunguka. Mtazamo ulionao juu ya dunia, maisha na kila kinachokuzungusha, unaweza kuyafanya maisha yako kuwa bora kila siku au kuwa hovyo zaidi.

Jinsi unavyochukulia kila kitu kinachoendelea kwenye maisha yako, kuna madhara makubwa kwa hatua utakazochukua na matokeo ya hatua hizo kwenye maisha yako.

Kuna mitazamo mingi ambayo watu wanayo juu ya dunia na maisha kwa ujumla. Wapo ambao wanachukulia maisha kama vita, kama mapambano ambapo wenye nguvu wanapata na wanyonge wanakosa. Wapo ambao wanachukulia maisha kama mchezo, ambapo anayetumia mbinu nzuri anashinda mara zote.

Mtazamo wowote ambao unauchukua na kuishi nao kwenye maisha yako, kwanza kabisa lazima uwe mtazamo chanya, mtazamo wa kwamba inawezekana na hivyo ukusukume kuchukua hatua. Usiwe na mtazamo hasi kwamba haiwezekani mtazamo huu utakukatisha tamaa na utashindwa kuchukua hatua.

Pia hakikisha mtazamo wako unakuwa wa utele na siyo uhaba. Wapo watu wanaochukulia kila kitu kwa uhaba, hivyo kuwa na uchoyo na kushindwa kutoa kwa wengine. Watu hawa wanajikuta wakiwa na maisha magumu kila siku, mpaka wanapokufa. Unahitaji kuwa na mtazamo wa utele, kwamba dunia ina fursa nyingi kwa kila mtu kuweza kupata anachotaka. Kwa mtazamo huu na kuchukua hatua sahihi, kunayafanya maisha ya kila siku kuwa bora.

NIDHAMU YA PILI; KUCHUKUA HATUA.

Haijalishi unajua kiasi gani, haijalishi una mtazamo chanya kiasi gani, haijalishi una nia njema kiasi gani, hakuna kitakachotokea kwenye maisha yako kama hutachukua hatua. Kuchukua hatua ni nidhamu muhimu kujifunza na kufanyia kazi kila siku.

Kila siku hakikisha unachukua hatua kuelekea kule unakotaka kufika, elewa vizuri hapa, ni hatua na siyo maneno au mipango. Piga hatua, fanya kitu, hata kama ni kidogo sana, ni bora kuliko kutokufanya kabisa.

Kama kuna kitu chochote ambacho unataka kwenye maisha yako, unahitaji kuchukua hatua ili kuweza kukipata. Kama kuna kitu ambacho hukipendi, pia unahitaji kuchukua hatua kukibadili. Hakuna kitakachotokea bila wewe mwenyewe kuchukua hatua.

Iishi kila siku yako kwa kupiga hatua kuelekea kwenye maisha ambayo unataka kufika. Kila siku hesabu ni hatua zipi umeweza kupiga, na zipi umeshindwa kupiga ili uweze kuwa bora zaidi kwa siku zinazokuja.

Mabadiliko na mafanikio yoyote kwenye maisha, yanatokana na kuchukua hatua, kufanya kitu.

Wakati mwingine watu wamekuwa wakisubiri na hawachukui hatua kwa kujiambia kwamba bado hawajawa tayari. Tatizo la kuwa tayari ni kwamba hakuna wakati utajiona tayari umekuwa tayari. Kila siku kuna kitu hujakamilisha, hivyo ni vyema kuchukua hatua kwa pale ulipo sasa na mengine utaendelea kurekebisha kadiri unavyokwenda.

NIDHAMU YA TATU; UTASHI.

Mambo yote yanayotokea kwenye maisha yetu yamegawanyika katika makundi mawili muhimu, kuna mambo ambao yapo chini ya udhibiti wetu na kuna mambo ambayo hayapo chini ya udhibiti wetu. Katika mambo ambayo hayapo chini ya udhibiti wetu, hakuna tunachoweza kufanya kuyabadili hivyo hayapaswi kutupa usumbufu wowote ule.

Kwa yale mambo ambayo yapo chini ya udhibiti wetu, nayo yamegawanyika katika makundi mawili. Kuna mambo ambayo tunaweza kuyabadili sisi wenyewe na kuna mambo ambayo hatuwezi kuyabadili. Kwa yale tunayoweza kuyabadili tunapaswa kufanya hivyo mara moja, kwa yale ambayo hatuwezi kuyabadili moja kwa moja tunapaswa kutafuta namna ya kuyafanya yasiwe kikwazo kwetu.

Tunapaswa kutumia utashi kuyajua vizuri mambo yanayotokea kwenye maisha yetu yapo kwenye kundi gani ili tuweze kuchukua hatua stahiki kila siku.

Kwa mfano kama umekosa kitu kwa sababu wewe ni mfupi au mrefu, hakuna unachoweza kufanya kubadili kuhusu ufupi au urefu wako. Hivyo hili halipaswi kukubughudhi kwa namna yoyote ile. Unaachana nalo na uangalie yale yanayoweza kuendana na wewe.

Kama umeshindwa kukamilisha majukumu yako kwa sababu kuna mtu mwingine alipaswa kukamilisha sehemu yake ili wewe uendelee, ni kitu ambacho kipo chini yako lakini huwezi kubadili moja kwa moja. Hivyo wakati mwingine usifanye kazi na watu wa aina hiyo.

Kama umepata hasara kwenye biashara kwa kushindwa kutunza vizuri hesabu zako za biashara, hilo sasa ni tatizo lako na unahitaji kulitatua haraka.

Kila tatizo unalopitia kwenye maisha yako, kabla hujaanza kulalamika na kuruhusu likusumbue, kwanza liweke sehemu sahihi, je lipo chini ya uwezo wako au la. Na kama lipo chini ya uwezo wako je unaweza kulibadili au la. Ukifanya hivi kila siku na kwa kila jambo, utajikuta unatatua matatizo yako kwa urahisi na utaondokana kabisa na msongo wa mawazo.

Mara nyingi watu wanapata msongo wa mawazo kwa kufikiria sana vitu ambavyo havipo chini ya uwezo wao na kama vipo chini ya uwezo wao basi hawawezi kubadili moja kwa moja. Kwa mfano kama ulitaka kuwahi mahali, na wakati unaenda ukakutana na foleni ndefu ya magari ambayo inakuchelewesha, kukasirika na kufikiria sana hali hiyo hakutakusaidia chochote. Hapa unapaswa kuangalia je foleni ipo ndani ya uwezo wako? Jibu ni hapana, na je kuwahi kupo ndani ya uwezo wako? Jibu ni ndiyo. Je unaweza kuwahi sasa? Jibu ni hapana. Na je unawezaje kubadili hilo? Hapa sasa utakuja na mpango wa kuwahi mapema zaidi popote unapopanga kwenda ili hata ukikutana na foleni, isikucheleweshe.

Hizi ndiyo nidhamu tatu muhimu tunapaswa kujijenga na kuziishi kila siku ili tuwe na siku bora na mwisho tuwe na maisha bora kabisa.

Kumbuka lengo la falsafa mpya ya maisha ni kuyafanya maisha yetu kuwa bora zaidi, yenye furaha na mafanikio makubwa. Sasa unaonaje pale unapokuwa na mtazamo sahihi wa maisha yako, kuwa mtu wa kuchukua hatua na kutumia utashi kutatua matatizo yako ya kila siku? Je maisha yako yataendelea kuwa ya kawaida? Hakika utakuwa na maisha bora sana.

Sasa umeshajua, kilichobaki ni wewe kuchukua hatua kila siku, KILA SIKU.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK