Hongera rafiki kwa asubuhi nyingine nzuri sana ya leo.
Leo ni siku mpya na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili tuweze kupata matokeo makubwa.
Tutumie muda wetu wa leo vizuri rafiki.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu INSTANT GRATIFICATION au RAHA YA HAPO KWA PAPO.
Mtoto mdogo anapotaka kitu, anakitaka sasa na atatumia kila mbinu mpaka apate kile anachotaka. Hayojali kingine chochote mpaka apate kile anachotaka. Anaweza kulia mpaka akaumwa kichwa ili tu apate anachotaka.
Lakini unapokuwa mtu mzima, unapaswa kuacha tabia hii na kuanza kufikiria kwamba siyo kila unachokitaka unapaswa kukipata hapo hapo hasa vitu vya raha.
Unapaswa kujua ya kwamba kuna gharama unapaswa kulipa ili kupata unachotaka na hii haitokei haraka.
Cha kushangaza, wapo watu wazima wengi ambao bado wanaendelea na tabia hii ya utoto. Wanataka kitu na wanakitaka sasa, hivyo watatumia kila njia mpaka ambazo siyo sahihi mradi tu wapate kile wanachotaka.
Na inapokuja kwenye raha na starehe, basi wengi wanataka sasa, hawana muda wa kusubiri.
Watu wanataka furaha sasa na kama hawawezi kuipata kwa njia za kawaida, basi wanaitafuta kwa kutumia vilevi.
Watu wanataka hela ya kununua kitu fulani sasa hivi na kama hawana fedha hiyo wanakikbilia kukopa.
Watu wanataka wawe na kipato sasa, hawana muda wa kusubiri na ndiyo maana wapo tayari kukaa kwenye ajira zenye maslahi kidogo kuliko kufanya biashara. Ajira inawapa kidogo sasa, biashara inabidi wasubiri, na wao subira hawana.
Kwa kifupi ni kwamba kama huna subira, kama kila unachotaka unakitaka sasa, hutaweza kufanikiwa. Kwa sababu siku zote mambo mazuri yanahitaji subira. Mambo mazuri hayataki haraka wala pupa.
Anza sasa kujijengea nidhamu ya kuwa na subira, na anza na vitu vidogo. Kwa mfano siyo lazima ukimbilie kula kitu kwa sababu umekiona, au jinyime kitu ambacho unakitaka sana kwa sasa.
Kwa mfano kama unataka sana kunywa soda au bia muda fulani, jinyime kunywa, kwa wakati huo. Hii siyo kujitesa, bali kujijengea nidhamu ya kusubiri na kujua kwamba siyo kila kitu unakipata muds huo unapokitaka.
Nakutakia siku njema sana rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
http://www.makirita.info