Maswali Muhimu Ya Kujiuliza Leo Katika Maisha Yako.Habari mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa uko salama na unaendelea vizuri katika maisha yako. Kama uko katika changamoto au wakati mgumu katika maisha yako pole sana endelea kukabiliana nayo na ujue ya kwamba hakuna hali ya kudumu katika maisha yako vumilia tu hilo nalo litapita na utarudia katika hali yako ya kawaida. Tunamshukuru Mungu pia kwa zawadi ya siku hii ya leo kwa kunistahilisha kuandika makala hii na kukustahilisha wewe kuweza kuwa msomaji wangu kupitia mtandao huu. 

Nashukuru sana rafiki yangu kwa kuendelea kuwa pamoja na mimi kupitia mtandao huu hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kukualika tena katika makala yetu ya leo.

Katika makala yetu ya leo tutakwenda kujifunza maswali muhimu ya kujiuliza leo katika maisha yako. Je ni maswali gani? Karibu mpenzi msomaji tuweze kusafiri kwa pamoja mpaka mwisho wa makala hii ili uweze kujua yale mazuri niliyokuandalia siku hii ya leo. Mwandishi na mwana falsafa jim rohn aliwahi kusema ‘’ if you want to change your result, you have to change your thinking first’’ akiwa na maana ya kwamba kama unataka kubadilisha matokeo yako, unatakiwa kwanza kubadilisha mtazamo wako wa kufikiri. Hivyo basi kama unataka kubadilisha kitu chochote katika maisha yako unatakiwa kubadilisha kwanza namna unavyofikiria mambo.
Mpendwa rafiki, tumia muda wako leo mchache na jiulize maswali yafuatayo katika maisha yako.

1. Hali ya afya yako ikoje kwa sasa? Afya yako ndio utajiri namba moja duniani utakaokuwezesha kutimiza malengo yako yote uliyojiwekea hapa duniani. Unakula vizuri vyakula vya kujenga mwili na kuupa mwili kinga dhidi ya magonjwa? Unafanya mazoezi ya mwili? Unapunguza uzito? Unakunywa maji mengi? Unakula matunda? Au unakula vyakula vyepesi vya kuharibu mwili wako kama vile chips na vinywaji kama vile soda.

2. Mtazamo wako juu ya maisha yako ukoje kila siku? Maisha yako unayachuliaje je katika mtazamo chanya au hasi. Maisha yako yametawaliwa na furaha au huzuni? Maisha ni furaha na una uamuzi wa kuchagua kuishi kwa furaha au huzuni bila kujali matatizo uliyokuwa nayo. Kama unaishi maisha yako katika mtazamo chanya ni rahisi kuishi katika furaha na mafanikio lakini ukiishi katika mtazamo hasi lazima utaona maisha ni huzuni badala ya furaha na utakuwa mlalamikaji na mtu wa kulaumu.

3. Mahusiano yako kiujumla katika idara hizi zifuatazo yako?

i. Mahusiano yako na familia yako ya koje? Mara ya mwisho ni lini ulimwambia au uliwaambia watoto wako kuwa unawapenda au nakupenda? Mara ya mwisho ni lini uliwakumbatia na kuwabusu watoto wako? Watoto wanahitaji upendo na kuhisi kuthaminiwa je watoto wako au katika familia yako wanaonja falsafa ya tunda la upendo? Au umeshakufa siku nyingi katika mioyo ya watoto wako wanakusubiri tu wakuzike? Unapata muda wa kukaa na familia yako?

ii. Mahusiano yako na mpenzi au mwenza wako yakoje? Falsafa ya upendo ipo? Uaminifu, kuvumiliana, furaha , amani ipo katika mahusiano yenu? Kama ipo au hakuna unachukua hatua gani kurekebisha hiyo hali? Vuta picha ya nyuma mlivyokutana wakati mko katika uchumba jinsi ulivyokuwa unaonesha upendo na kujali ni sawa na sasa? Kama siyo nani ni kiini cha kosa na umechukua hatua gani baada ya kujua kama wewe au yeye ndio kiini cha kosa kinachowafanya mwendelee kuishi maisha ambayo hayastahili kuishi kama wapenzi?

iii. Mahusiano yako ya koje na marafiki wako, ndugu, jamaa na jirani zako? Umekuwa ni faraja au kikwazo kwa watu hawa wa karibu kwako? Marafiki zako na watu waliokuzunguka wananufaikaje na wewe, wanajifunza nini kutoka kwako au wewe ndio umegeuka kuwa adui wa kurusha makombora ya kusengenya, umbea, wivu, chuki na kutokusamehe na kulipa visasi? Jitafakari leo na uchukue hatua chanya.

4. Ni kwa namna gani unailisha akili yako chakula? Unatakiwa kuilisha chakula akili yako na chakula cha akili au ubongo wako ni maarifa na siyo kitu kingine. Jiulize katika taaluma uliyosomea umeshasoma vitabu vingapi vya kuongeza maarifa tofauti tofauti na vitabu vya darasani yaani ambavyo haviko katika mtaala wa darasani? Tokea umalize shule au chuo ni mara ngapi umesoma kitabu kwa ajili ya kuona akili yako? Ni mara ngapi unasoma makala chanya za kujenga na kusikiliza sauti zilizorekodiwa za watu makini duniani? Au wewe ndio unakomaa na kufuatilia udaku katika magazeti, mitandao ya kijamii kujua Fulani kafanya nini na mengine mengi je unafikiri hiyo ndio njia ya kuongeza maarifa kwa fuatilia udaku? Soma vitabu rafiki na jifunze kwa watu utalisha ubongo wako maarifa mapya kila siku.

5 .Maisha yako yana msaada kwa watu wengine? Unaishi maisha ya kushawishi watu au unaishi maisha ya kugeuka kuwa mwalimu mzuri wa kukosoa na kukatisha tamaa watu au unaishi maisha ya kuwaaminisha watu kuwa mambo yanawezekana kama mtu akiamua kuchukua hatua. Jiulize swali hili leo.

6. Malengo yako uliyojiwekea mwaka huu au wiki hii umefanikiwa kiasi gani? Jiulize maswali muhimu yote uliyojiwekea kuhusu malengo yako na halafu utachukua hatua je umefanikiwa kiasi gani? Kama unaishi bila malengo basi wewe ni mtu ambaye huna mwelekeo na mwelekeo wowote utakuchukua katika maisha yako kama hujajiwekea malengo.

7. Maisha yako ya kiroho yakoje? Hapa angalia katika imani yako angalia mahusiano yako na Mungu wako yakoje? Imani yako ikoje imekua au imelala na kumbuka kuwa imani ni zawadi kutoka kwa Mungu huwezi kuishika wala kuiona.

8. Unatumiaje zawadi ya muda uliyopewa bure? Muda ni mojawapo ya zawadi ya kipekee sana tuliyopewa bure. Je unautumiaje muda wako? Mwanafalsafa na mwandishi Seneca aliwahi kusema ‘’ life, if well lived, is long enough’’ akiwa na maana ya kwamba maisha ni marefu kama ukiishi vizuri au ukitumia muda wako vizuri hapa duniani. Je unatumiaje muda wako ili kuacha alama hapa duniani? Jiulize swali hili muhimu sana katika maisha yako. Tumia muda wako vizuri na muda ndio maisha yako rafiki. Tumia muda wako kuacha alama ya wewe kuendelea kuishi hata kama hutokuwepo duniani.

Hatua ya kuchukua leo, kaa chini na tenga muda wako halafu jiulize maswali yote muhimu katika maisha yako na chukua hatua chanya mara moja leo.

Mwisho, somo letu la leo lilitualika kuweza kujiuliza maswali muhimu katika maisha yetu ili tuweze kupata matokeo tofauti. Ili tubadilishe maisha yetu ni lazima kwanza tubadilishe namna ya kufikiri kwanza na njia nzuri ya kufikiri ni pamoja na kujiuliza maswali muhimu na makini kwenye maisha yako. Nakutakia utekelezaji mwema katika haya uliyoweza kujifunza leo.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s