Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?
Karibu tena kwenye makala yetu ya leo ya FALSAFA MPYA YA MAISHA, ambapo tunakwenda kujifunza mambo muhimu ya kuzingatia ili kuweza kuwa na maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa.
Moja ya vitu muhimu sana tunavyopaswa kuvizingatia kwenye falsafa yetu ya maisha ni UKWELI. Tumewahi kujifunza na huu ni msingi wa falsafa yetu mpya kwamba UKIUJUA UKWELI BASI UNAKUWA UMEPATA UHURU WA KWELI. Kama ambavyo imeandikwa kwenye vitabu mbalimbali vya dini na falsafa kwamba ijue kweli nayo itakuweka huru.
Leo nina habari za kusikitisha mwanafalsafa mwenzangu, habari hizo ni kwamba hatuujui ukweli, na hatuwezi kuufikia ukweli kwa asilimia 100. Hatuujui ukweli kwa sababu maisha kwenye jamii zetu yamejaa upotoshwaji mkubwa sana. Wapo watu wanaopotosha watu ili wao waendelee kunufaika au watimize kile ambacho wanakitaka.
Kwa mfano tukiangalia kwenye dunia ya sasa ambayo tumeunganishwa kama kijiji, basi ukweli ndiyo unazidi kuzikwa. Vyombo vya habari vitakupa habari ambazo siyo kweli kwa asilimia 100. Watahakikisha wanaibadili habari ili iende kama wanavyotaka wao na watimize kile ambacho wanataka kutimiza. Kama ni kupata wafuasi wengi zaidi a baadaye kupata faida.
Mitandao ya kijamii ndiyo kabisa imeupoteza ukweli, mengi ambao watu wanashirikisha kwenye mitandao ya kijamii siyo kweli kwa asilimia 100. Sasa hivi hata maisha ya kawaida tu ya watu wanakwepa ukweli na kuishi maigizo. Ndiyo maana utamwona kila mtu kwenye mitandao hii ana furaha na maisha bora, lakini utakapokutana naye kwenye uhalisia, mambo ni tofauti kabisa na ulivyodhani kupitia mitandao.
Kilichoharibu na kuzika kabisa ukweli, ni biashara na nia ya kupata faida kubwa. Ili kupata faida kubwa, wafanyabiashara wengi wamekuwa hawasemi ukweli kwa asilimia 100. Wamekuwa wanaugeuza ukweli uendane na kile wanachofanya wao, ili uendelee kuwa mteja wao. Wanahakikisha unasukumwa kuendelea kuwa mteja wao ili waendelee kunufaika.
Hata dini ambazo mwanzo zilitegemewa kuwa chanzo cha ukweli, kwa sasa mambo yamebadilika. Hakuna tena ukweli wa asilimia 100 kupitia kwenye dini, bali kila dini imekuwa na malengo yake ya kuhakikisha inapata wafuasi wa kutosha. Hivyo kitabu kimoja cha dini, kinazalisha madhehebu mengi kulingana na mtu anavyoweza kukitumia kitabu hicho kuwafanya watu wawe wafuasi wao.
Kila kitu kinachoendelea kwenye maisha yetu, ukweli umefichwa na wachache, na mara nyingi ukweli haujulikani kabisa.
Kufichwa au kutokujulikana kwa ukweli hakujaanza leo, hiki ni kitu ambacho kimekuwepo tangu kuwepo kwa maisha hapa duniani. Kwa mfano kabla ya karne ya kumi na nne, mambo mengi tunayoyajua leo kupitia sayansi hayakuwepo kabisa. Ilikuwa siyo ruhusa mtu kuja na maelezo yake ya kisayansi kuhusu jambo lolote lile. Bali utawala ndiyo ulikuwa na jukumu la kuwaambia watu nini maana ya vitu fulani.
Kwa mfano utawala wa Roma ulisema kwamba dunia ipo katikati na jua linaizunguka dunia. Huu ulichukuliwa ndiyo ukweli na hakuna aliyeruhusiwa kuhoji au kupinga. Hata alipotokea mtu na ushahidi kwamba dunia haipo katikati na jua halizinguki dunia, badala yake jua lipo katikati na dunia inazunguka jua, alionekana anaharibu watu na kuhukumiwa kufungwa.
Kati ya karne ya 14 mpaka ya 17 kulitokea mwamko mkubwa (Renaissance) huko Ulaya ambao ndiyo ulipelekea sayansi kufufuka tena na watu kuanza kuutafuta ukweli. Lakini mpaka sasa bado ukweli tunaendelea kuutafuta, hata sasa mengi tunayoyajua siyo ukweli kwa asilimia 100.
Hivyo sisi kama wanafalsafa, tunahitaji kuwa na njia ya kuweza kuuchuja ukweli na kuondokana na uongo ambao unafanana na ukweli kwenye macho ya wengi.
Jiulize ni mara ngapi au umeona watu wangapi wakidanganywa kuingia kwenye biashara au shughuli fulani ili wapate utajiri lakini wasiupate? Jiulize mara ngapi watu wamedanganywa kutumia kitu fulani ili afya zao ziwe bora (mfano kupungua uzito) lakini hawapati matokeo wanayotaka? Jiulize kwa nini kila baada ya miaka mitano wanasiasa wanakuja na uongo ule ule na bado watu wanaendelea kuwapigia kura?
Yote haya ni kwa sababu watu hawana njia ya uhakika ya kuweza kuuchuja ukweli, na hivyo wanapojikuta wakiwa na taarifa nyingi, hawajui ukweli ni upi na uongo ni upi, wanajikuta wakiamini chochote wanachoambiwa.
Sasa sisi wanafalsafa tunatumia hatua hizi sita kuchuja ukweli, kwenye jambo lolote tunaloambiwa, tunaloona au hata tunalofikiria sisi wenyewe.
Hatua ya kwanza; uzoefu binafsi (PERSONAL EXPERIENCE).
Kitu chochote unachosikia au kuona au kufikiria, hebu jiulize je wewe mwenyewe una uzoefu binafsi katika kitu hicho? Umesikia kwamba mtu ameweza kufanya kitu fulani, hebu jiulize je wewe umewahi kufanya kitu kama hicho?
Hii ni hatua ya kwanza na muhimu sana kwenye kuuchuja ukweli, kwa sababu kama wewe mwenyewe una uzoefu na kitu fulani, basi kuna uwezekano ni kweli.
Hatari ya hatua hii ni kwamba hisia zetu zinaweza kuingilia uwezo wetu wa kufikiri. Tunaweza kujikuta tunaunganisha matukio ambayo hata hayaendani ili tu yakubaliane na ukweli tunaotaka kudhibitisha.
Inapokuja kwenye uzoefu binafsi, usijaribu kukaribisha uzoefu uendane, ali angalia kama wewe umewahi kufanya kama hicho unachoona au kusikia.
Hatua ya pili; uzoefu wa wale ambao unawajua (EXPERIENCE OF PEOPLE YOU KNOW)
Hatua ya pili ya kuchuja ukweli ni kuwaangalia wale ambao unawajua na kuona kama na wao wamewahi kupata au kufanya kama vile unavyoona au kusikia. Mara nyingi tunapotaka kufanya kitu, huwa tunaomba ushauri kwa wale ambao wametuzunguka, tukiamini ya kwamba wanaweza kuwa na uzoefu au ujuzi kuliko sisi. Hii ni njia muhimu ya kuchuja ukweli, kwa sababu kama mtu ana uzoefu, anaweza kukusaidia usitumbukie kwenye hatari.
Hatari ya hatua hii ni kwamba huwezi kutegemea moja kwa moja kwenye uzoefu wa wengine. Mara nyingi watu huwa hawasemi ukweli, na wengine wanaweza kukudanganya kwa kuogopa kukuambia ukweli, hasa pale ukweli unapokuwa unaumiza.
Unapotumia hatua hii unahitaji uangalifu wa hali ya juu, kwa sababu unachoona kwa watu kinaweza kisiwe kweli, kuna mengi yanaweza kuhusika. Pia wanachokuambia watu huwezi kukitegemea kwa asilimia 100.
Hatua ya tatu; Wataalamu (EXPERTS).
Hatua ya tatu ya kuuchuja ukweli ni kupitia wataalamu, hawa ni watu ambao wana uelewa mkubwa sana kuhusu jambo fulani. Kama kuna kitu unataka kufanya, ni busara kuwatafuta wataalamu wa jambo hilo na wakakupa mawazo yao na uzoefu wao kuhusiana na jambo hilo. Iwe ni kazi au hata biashara, wapo watu ambao wana maarifa, uelewa na uzoefu mkubwa kwenye jambo hilo, ambao kupitia wao unaweza kujifunza mengi unayohitaji ili kuweza kuchukua hatua sahihi.
Hatari ya hatua hii ni kwamba wataalamu hawa wanafanya hivyo ili kupata fedha, hivyo hawatakuambia ukweli halisi kama ukweli huo unapelekea wao kukosa fedha. Unaweza kwenda kwa mtaalamu wa biashara ukiwa na wazo lako la biashara, akawa anajua kabisa kwamba hilo wazo lako hutaweza kulifanya, lakini kama umelipa hatakuambia hivyo, atakupa moyo kwamba ukiweka juhudi na kutokukata tamaa utafanikiwa.
Hivyo unahitaji kuwa makini sana na chochote unachoambiwa na wataalamu. Maana wengi mno wamepotezwa na wataalamu, na pia wengi wamenufaishwa na wataalamu.
Hatua ya nne; tafiti za kisayansi (SCIENTIFIC STUDIES).
Hatua nyingine muhimu ya kuuchuja ukweli ni kuangalia tafiti zilizofanywa kwenye eneo ambalo unataka kupata ukweli. Tafiti mara nyingi zinaonesha uhalisia wa jambo husika, kwa sababu tafiti zinafanywa kwa majaribio halisi na baadaye kutumika kama kielelezo cha kuonesha hali kwa ujumla ipoje. Tafiti hizi zinauhalisia zaidi kuliko maneno tu ya kuongea, kwa sababu watu wanakuwa wamefanya majaribio na kuona matokeo halisi.
Hatari ya hatua hii ni kwamba mara nyingi mtu anayefanya utafiti husika, anaweza kuuelekeza ule utafiti ulete majibu anayotaka wewe. Na pia hakuna njia bora ya kudanganya kwa kutumia namba kama kutumia takwimu. Takwimu zile zile watu wanaweza kuzibadili watakavyo na kukuonesha ukweli ambao wanataka wao uone, ambao siyo uhalisia.
Hivyo unapotumia tafiti kama chujio la ukweli, ni lazima uende ndani zaidi na kuona namna utafiti huo ulivyofanyika.
Hatua ya tano; akili ya kawaida (COMMON SENSE).
Hatua nyingine unayopaswa kutumia kuchuja ukweli ni kutumia akili ya kawaida. Hapa unafikiria tu kwa kawaida je jambo kama hili linawezekana? Au linaweza kutokea? Katika mambo mengi tunayopitia kila siku, ukiweka tu akili ya kawaida, unaona kabisa kama inawezekana au la, kama ni kweli au la. Kuna kauli moja maarufu sana ambayo inasema “kama una wasiwasi kwamba kitu siyo cha kweli, basi siyo cha kweli.” Yaani “if something is too good to be true, then it is”. Hapa unatumia tu akili ya kawaida na kujaribu kuyaweka mambo pamoja, ukiona hayaendani basi unajua hapo kuna kitu siyo sawa.
Hatari ya njia hii ni kujidanganya wewe mwenyewe, hasa pale unapojiamini kupita kiasi. Unaweza kujiamini unaweza kweli kutumia akili ya kawaida, kumbe kujiamini kwako ni kwa uongo. Na kama umekuwa kwenye jamiia ambayo umelelewa kwenye misingi ambayo siyo ya kweli, akili yako ya kawaida itakupeleka kwenye mambo ambayo siyo ya kweli.
Hivyo unapotumia akili yako ya kawaida, kwanza jua akili hiyo ipo kwenye upande upi.
Hatua ya sita; kutambua mwenendo (PATTERN RECOGNITION).
Hatua ya sita na ya mwisho ya kuuchuja ukweli ni kuangalia mwenendo wa vitu kwa umakini. Ukiangalia mwenendo wa kila kitu kuna vitu fulani ambavyo utavitambua vinakwenda pamoja. Hii ni njia bora sana ya kujua ukweli, japo unakuhitaji muda ili kuweza kuitumia vizuri. Kwa mfano kama kila mara unapokula samaki basi mwili wako unawasha, basi utajua kuna namna mwili wako hauendani na samaki. Mara ya kwanza kula samaki na mwili ukawasha utafikiri labda una tatizo jingine, mara ya pili pia utaona kuna tatizo lakini hutafikiria samaki. Ni mpaka ikuchukue muda mrefu, uanze kuangalia ni wakati gani unawashwa sana na baada ya nini. Hapo ndipo utaona uhusiano wa wewe kula samaki na kuwashwa.
Hatari ya hatua hii ni jambo fulani kutokea kwa bahati tu, yaani mambo mawili yanatokea pamoja lakini hayana uhusiano wowote wa karibu. Kama ambavyo wazee wa zamani waliwakataza wanawake wajawazito wasile mayai kwa sababu watoto hawataota nywele. Ukweli halisi ilikuwa siyo kutoota nywele, bali wajawazito wakila mayai kwa sana wakati wa ujauzito basi watoto wanakuwa wakubwa sana kiasi cha kushindwa kutumia njia ya kawaida ya uzazi. Na kwa kuwa enzi hizo hakukuwa na njia za upasuaji, basi ilikuwa hatari kwa wanawake wanaopata watoto wakubwa.
Wakati mwingine njia hii inaingiliwa na hisia zetu wenyewe, kupitia mambo ambayo tunapendelea kufanya. Tunaweza kuyahusianisha mambo ambayo hayana uhusiano wowote kwa sababu tu tunataka yawe hivyo.
Hivyo unapotumia njia hii, hakikisha unafuatilia kwa undani kweli na kuona uhusiano wa mambo yanayotokea uko wapi.
Hivi ndizo hatua sita za kuuchuja ukweli, na kama ambavyo tumeona, kila njia ina hatari au changamoto yake na ndiyo maana kuufikia ukweli kwa asilimia 100 ni kitu kigumu mno. Kadiri unavyotumia hatua nyingi kwenye jambo moja, ndivyo unavyozidi kuukaribia ukweli, japo kuufikia kabisa bado ni kitu kigumu.
Njia moja ya uhakika ya kuukaribia ukweli.
Kwa kuwa kuufikia ukweli kwa asilimia 100 ni kugumu na kwa sababu tunahitaji kupata ukweli ili kuweza kuchukua hatua sahihi, ipo njia moja ambayo inatusogeza karibu zaidi na ukweli. Njia hii haitupi ukweli kwa uhakika wa asilimia 100, lakini inatusogeza karibu sana na ukweli.
Njia hiyo ni MSIMAMO (CONSISTENCY). Kama jambo linatokea mara zote kwa njia ile ile bila ya kubadilika kwa namna yoyote ile, basi jambo hili linaweza kuwa kweli. Msimamo ndipo msingi wa tafiti za kisayansi ulipojengwa, na msimamo ndipo unapohitaji kujenga msingi wako wa ukweli.
Kwa mfano tunasema ya kwamba dunia ina nguvu ya mvutano, ambayo inavuta vitu vyote viende katikati ya dunia. Kwa nini, kwa sababu kila mara ambapo utarusha kitu juu, lazima kirudi chini. Uende Ulaya, uende Amerika, ukirusha kitu juu lazima kitarudi chini. Kwa nini kitu kirudi chini na siyo kwenda juu moja kwa moja? Kwa akili ya kawaida, lazima kutakuwa na nguvu inayovuta kitu hicho kirudi chini. Hapo tunapata sehemu kubwa ya ukweli, japo siyo ukweli wote kwa sababu hatujui kwa hakika nguvu hii inatoka wapi na inafanyaje kazi. ndiyo zipo tafiti na majibu ya kuonesha nguvu hii inatokana na sumaku iliyopo ndani ya dunia, lakini bado siyo ukweli kwa asilimia 100. Kuna uwezekano wa kuwepo kwa vitu vingi ambavyo bado hatujavijua mpaka sasa.
Hivyo mwanafalsafa mwenzangu, kwenye jukumu letu la kuujua ukweli, tuanze na msingi wa msimamo.
Kama mtu amekufuata na kukuambia ukifanya biashara fulani basi utafanikiwa sana, anza kuwaangalia wafanyabiashara ya aina hiyo kama wana mafanikio. Na usiwaangalie waliopo eneo moja pekee, bali angalia walipo maeneo ambayo yanatofautiana.
Kama mtu anakufuata na kukuambia kwamba ana njia ya mkato na ya haraka ya kufika kwenye utajiri, mwambie akuoneshe watu wote ambao wametumia njia hiyo. Na angalia kwa kipindi cha muda mrefu, labda hata miaka 100 iliyopita, angalia watu waliotumia njia hiyo na mwisho wao ulikuwaje.
Chochote unachotaka kupata ukweli, angalia msimamo wa matokeo kutoka kwa wengine ambao tayari wameshafanya. Kama matokeo ni yale yale, kwa watu tofauti ambao wapo sehemu tofauti basi unaukaribia ukweli. Japokuwa msimamo hautupi ukweli kwa asilimia 100 kwa sababu zipo changamoto zake, lakini unatusogeza karibu sana na ukweli.
Usikubali tena kudanganyika kwa mambo ambayo yapo wazi kabisa, tumia hatua sita za kuchuja ukweli na mwisho kabisa angalia msimamo wa yale matokeo unayotarajia kupata.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK
Shukran kocha makirita
LikeLike
Karibu Hendry
LikeLike