Kila siku ninapowasiliana na watu, hasa wanaoniadikia wakitaka ushauri, wengi wanakuwa wamekwama, wanataka kuanza biashara lakini hawajui waanzie wapi. Wengine wanasema mtaji ndiyo hawana. Wengine tayari wana biashara ila wanashindwa kuzikuza.

Visingizio na sababu ni nyingi sana linapokuja swala la biashara. Lakini ukweli ni kwamba misingi ya kuanzisha na kuendesha biashara ni ile ile, bado haijabadilika na sijui kama itabadilika kwa siku zijazo.

Ipo misingi mikuu mitano, najua unaijua lakini hebu tukumbushane ili kuhakikisha tupo sawa wote.

Msingi wa kwanza; unahitaji kuwa na kitu cha kuuza.

Haijalishi ni kitu gani, muhimu ni kiwe na thamani kwa wengine. Inaweza kuwa bidhaa au huduma. Inaweza kuwa umetengeneza mwenyewe au unachukua kwa wanaozalisha na kuuza reja reja. Kwa vyovyote vile, unahitaji kitu ambacho unaweza kuuza.

SOMA; UKURASA WA 673; Misingi Mikuu Miwili Ya Kukuza Biashara Yoyote Ile.

Msingi wa pili; unahitaji kuwa na watu wanaotaka kununua kitu unachouza.

Hawa wanaitwa wateja, ni watu ambao wana shida, changamoto au mahitaji ambayo yanaweza kutatuliwa na kile unachouza. Hawa ni wale wanaotafuta thamani ambayo wewe unaitoa kupitia biashara yako. Ni watu muhimu sana kwenye ukuaji wa biashara yako. Unahitaji kuwapa thamani na wao wakupe fedha zao walizozipata kwa shida.

Msingi wa tatu; unahitaji kuwa na bei ya kile unachouza.

Kwa kuwa unataka kumpa mteja kile anachotaka, na wewe unataka maisha yako yaweze kwenda vizuri, basi unahitaji kuwa na bei ya kuuza kile unachouza. Hapa unakuwa na bei itakayomwezesha mteja kupata anachotaka, na wewe kuweza kuendelea kuishi na kufanya biashara. Kwa maana hiyo bei aweze kuimudu mteja na wewe uweze kupata faida.

SOMA; Jenga biashara yako kwenye misingi hii mitatu na itakuwa imara.

Msingi wa nne; unahitaji njia ya kumfikishia mteja kile unachomuuzia.

Mteja anapataje kile ambacho unakiuza wewe? Unampelekea pale alipo, au yeye anakuja hapo ulipo wewe. Unahitaji kuwa na njia ambayo itakuwezesha kuwafikishia wateja kile ambacho umechagua kuuza.

Msingi wa tano; unahitaji njia ya kuwafikia wateja wengi zaidi.

Wateja watajuaje kama wewe upo kwenye biashara, watajuaje kama wakija kwako watapata mahitaji yao na kutatua matatizo yao? Ni lazima uwe na njia ya kuwafikishia wateja taarifa zako, njia ya kuwafikia wateja wapya. Hapa unahitaji kuwa na njia bora ya kuitangaza biashara yako, ambayo itawafikia wateja husika wa biashara yako.

Ni misingi hiyo mitano rafiki, kama unakwama kuanza biashara anzia hapo. Na kama upo kwenye biashara lakini haifanyi vizuri, angalia katika misingi hiyo mitano, upo haupo vizuri.

Je bidhaa au huduma unayouza ina thamani? Ina uhitaji kwa watu?

Je wapo watu ambao kweli wanahitaji kile unachouza?

Je bei yako inaendana na uhalisia wa wateja uliopanga kuwafikia?

Je wateja wanaweza kufika kwenye biashara yako au wewe unaweza kuwafikia pale walipo?

Je watu wanajua kama biashara yako ipo?

Tatizo lolote la biashara linaanzia kwenye misingi hiyo mitano, ifanyie kazi kila siku.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK