Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?
Ni matumaini yangu kwamba uko vizuri na unakwenda kuianza siku hii ya kipekee ukiwa na hamasa ya hali ya juu.
Najua leo utakwenda kuweka juhudi kubwa kwenye kile unachofanya.
Na nina uhakika utafanya makubwa leo.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu FURSA MPYA….
Kama kuna kitu ambacho dunia haiwezi kukaukiwa basi ni FURSA MPYA, zipo nyingi na kila siku kuna fursa mpya utaisikia. Na ukiwa makini zaidi, kila kinachokuzunguka ni fursa.
Sasa watu wengi wamekuwa wanababaishwa na fursa, leo unamkuta anaanza kitu fulani ambacho ni kizuri, kesho inajitokeza fursa nyingine, anaachana na ya mwanzo na kuanza hiyo mpya. Wakati anaendelea anaona fursa nyingine bora zaidi, anaacha aliyokuwa anafanya na kuanza hiyo mpya. Au wakati mwingine anafanya zote kwa pamoja. Ukimuuliza atakuambia fursa hizi ni nzuri zikipita ndiyo nimezikosa.
Fursa ni nyingi mno, lakini huwezi kukimbizana nazo. Huwezi kujaribu kila fursa, utapoteza muda mwingi na mwisho wa siku unajikuta hujakamilisha jambo lolote kubwa. Muda unaopoteza kwenye kila kuanza fursa mpya, ungekuwa muhimu kuchagua kitu kimoja na kuweka juhudi kubwa.
Ufanye nini?
1. Kuwa na vipaumbele kwenye maisha yako, jua maeneo gani upo vizuri na yatumie hayo kwenye shughuli zako.
2. Chagua aina ya fursa ambazo utazitumia macho, ambazo ukizisikia utazifikiria. Na nyingine zote achana nazo.
3. Chagua fursa moja utakayoifanyia kazi, na weka juhudi zako zote pale, usihangaike na fursa nyingine wakati unajenga misingi ya fursa ya kwanza.
4. Ukishasimamisha misingi, unaweza kuangalia fursa nyingine, ZINAZOENDANA na fursa uliyochagua, usihangaike na vitu vingine vipya kabisa.
5. Fursa mpya siyo njia ya mkato na ya haraka ya kufanikiwa. Fursa kuwa mpya haimaanishi ni mteremko, lazima uweke kazi.
Bilionea Richard Branson anasema, FURSA ZA KIBIASHARA NI SAWA JA MABASI YA ABIRIA, UKIKOSA MOJA KUNA JINGINE LINAKUJA.
Usibabaishwe na fursa mpya, chagua unachotaka kufanyia kazi ja weka juhudi zako pale.
Mafanikio ni zao la juhudi, maarifa, nidhamu, uvumilivu na kutokukata tamaa. Hakuna fursa mpya kwenye hiyo orodha.
Nakutakia siku njema sana rafiki yangu.
Rafiki na Kocha,
Makirita Amani,