Kila siku kuna habari mpya na malalamiko ya watu walioaminiwa na kupewa nafasi ya uongozi kutumia vibaya madaraka yao. Hali hii imekuwa inapelekea watu kuumia na kupata madhara makubwa.
Tatizo hili lipo kuanzia uongozi wa juu kabisa wa nchi mpaka uongozi wa chini kabisa wa mtaa. Na pia linaenda mpaka kwenye uongozi wa familia, uongozi wa kazi na hata uongozi wa biashara.
Chanzo kikuu cha matatizo haya ya uongozi ni watu kukosa maarifa sahihi ya kiuongozi. Watu wanajikuta na madaraka makubwa ambayo hawajui wayatumieje, mwishowe wanayatumia kimakosa na wanaleta madhara makubwa kwao na kwa wengine kwa ujumla.
Watu wengi wamekuwa hawana utamaduni wa kujisomea maarifa ya uongozi na hata historia za mambo yaliyowahi kutokea huko nyuma. Namna ambavyo watu walitumia vizuri madaraka yao na kufanikiwa na namna ambavyo wengine waliyatumia vibaya na wakashindwa kabisa.
Hivyo tatizo kuu kabisa ni watu kukosa maarifa sahihi, na kwa kuwa wengi hawana utamaduni wa kujisomea, basi wanaishia kufanya mambo kwa mazoea au kwa kuangalia wengine wanafanya nini.
Suluhisho la tatizo hili ni watu waanze kutafuta maarifa sahihi ya uongozi. Kwa sababu kila mmoja wetu ana nafasi fulani ya uongozi, basi ni vyema tukajijengea utaratibu wa kujifunza na kujisomea kuhusu uongozi. Lazima tujenge utaratibu wa kujifunza kutokana na historia za watu waliopita.

KITABU KIMOJA CHA UONGOZI AMBACHO NASHAURI KILA MTU AKISOME.
Katika utaratibu wangu wa kujisomea vitabu, nimekutana na kitabu kimoja ambacho nimekuwa nakisoma na kukisikiliza mara kwa mara. Kitabu hichi nilikutana nacho kwa mara ya kwanza mwaka 2013 na nimekuwa nakisoma kila mara. Kwenye gari nina AUDIO BOOK ya kitabu hiki, na mara nyingi ninapokuwa kwenye foleni huwa nasikiliza kitabu hiki. Kupitia kitabu hiki nimekuwa naona wazi makosa makubwa ambayo viongozi na hata watu wa kawaida wanayafanya na yanaharibu kabisa sifa zao.

Kitabu hiki kinaitwa THE 48 LAWS OF POWER, ambacho kimeandikwa na mwandishi ROBERT GREEN. Mwandishi amechimba sana historia ya tangu enzi na enzi na kuonesha namba ambavyo watu wamekuwa wanayatumia madaraka kwa mafanikio na wanaoyatumia vibaya na kushindwa.
Mwandishi amekuna na sheria 48 za madaraka ambapo kwa kila sheria ametoa mifano ya watu waliotii sheria hiyo na kufanikiwa na mifano ya watu waliokiuka sheria hizo na kuumia. Na sheria ya kwanza kabisa kwenye kitabu hiki inaitwa NEVER OUTSHINE THE MASTER, yaani usitake kuonekana wewe upo juu kuliko mkubwa wako, hata kama unajua kuliko mkubwa wako, kuonesha hilo wazi ni lazima atakuondoa. Na ametoa mifano ya waliotii sheria hii na kufanikiwa na walioikiuka na wakaishia kuondolewa kwenye madaraka madogo waliyokuwa nayo.
Hiki ni kitabu ambacho nashauri kila mtu akisome, kwa namna ninavyokielewa kitabu hiki kinaweza kukusaidia kwa pande mbili.
Upande wa kwanza kinakupa mbinu za kiuongozi ambazo unaweza kuzitumia popote, kuanzia kwenye familia, kazi, biashara, mahusiano. Hapa unapata njia sahihi za kufuata ili kuweza kutimiza kile unachotaka.
Upande wa pili kinakuzuia wewe kutumika kwa faida ya wengine. Baadhi ya sheria kwenye kitabu hiki zinaonesha namna gani viongozi wanaweza kuwatumia watu wengine kwa manufaa yao. Kwa mfano unaweza kufanya kazi wewe lakini sifa akazibeba mtu mwingine. Kupitia kitabu hichi utajifunza namna ya kulinda sifa yako na kuhakikisha hutimiki na wengine.
Ushauri wangu ni kila mtu akisome kitabu hiki, maana ni mgodi wa dhahabu linapokuja swala la uongozi.
Raisi mteule wa Marekani Bwana Donald Trump, kwa sehemu kubwa alitumia sheria za kitabu hiki na ndiyo maana aliweza kushinda kinyume na mategemeo ya wengi.

ANGALIZO; KITABU HIKI KINAWEZA KUWA HATARI.
Sheria za kitabu hiki, kama zitatumika vibaya zinaweza kuzalisha viongozi hatari kabisa. zinaweza kuzalisha viongozi ambao ni madikteta, wanaowatumia watu kupata chochote wanachotaka wao.
Hivyo ni imani yangu kwamba utakuwa na hekima na busara ya kukuwezesha kukichambua kitabu hiki na kuchukua yale mazuri yanayoweza kuleta faida kwa nchi yetu.
Mwisho kabisa kama yupo mtu anayeweza kumfikishia Raisi ujumbe huu, basi amshauri sana asome kitabu hiki. Kina mambo mazuri yatakayomwezesha kuongoza vizuri.

Unaweza kupata kitabu hiki kwa kukinunua kwenye maduka makubwa ya vitabu, au kupakua hapa bure nakala tete (softcopy) ya kitabu, kwa link nitakayoweka. Kama utapenda AUDIO BOOK ili uweze kuisikiliza popote ulipo tunaweza kuwasiliana na ukapata. Audio book ni kubwa, zaidi ya masaa 10 ya kusikiliza, hivyo unaweza kuwa unasikiliza kila siku unapokuwa kwenye gari.
Link ya kupakua nakala tete bure fungua; https://www.dropbox.com/s/69jkp6qxado4n5a/Robert%20Greene%20-%20The%2048%20laws%20of%20power.pdf?dl=0

Kupata AUDIO BOOK ya kitabu hiki na vingine fungua link hii; http://www.amkamtanzania.com/p/blog-page.html
Nikutakie usomaji mwema wa kitabu hiki cha THE 48 LAWS OF POWER, pata maarifa na ongeza hekima na busara yako katika kuyatumia kwa usahihi.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.amkamtanzania.com