Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Hongera kwa nafasi hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kupata matokeo makubwa sana.
Katumie muda wa leo vizuri rafiki.

Asubuhi ya leo tunatafakari kuhusu INVESTMENT yaani UWEKEZAJI.
Ukweli ni kwamba huwezi kufanikiwa kama huwekezi, kwa sababu kitu unachofanya leo hakileti majibu leo leo, bali kinaandaa mazingira ya majibu mazuri siku za baadaye.
Kwa maana hiyo basi, mafanikio yetu yanatokana na uwekezaji tunaofanya.
Na tunaposema uwekezaji, hatumaanishi fedha pekee, bali tunamaanisha vitu vyote ambavyo vinatusukuma kwenda kuwa na maisha bora sana baadaye.
Hivyo unahitaji kuwekeza muda, katika mafanikio yako. Iwe ni kazi au biashara, hutaanza kufanya leo na kuanza kuyafurahia mafanikio leo. Unahitaji kuwekeza muda, ujitoke kwa kuda kuyatengeneza mafanikio.
Unahitaji pia kuwekeza nguvu, kwa sababu mambo yote mazuri yanahitaji juhudi zako. Unapoweka nguvu unatengeneza mazingira mazuri ya kufanikiwa baadaye.
Unahitaji kuwekeza hata utu wako pia, kwa kuwa tayari kufanya mambo ambayo huenda yatashindwa na watu watakucheka na kukudharau, lakini unakuwa tayari kufanya.
Na pia unahitaji kuwekeza fedha.
Nakukumbusha haya japo najua unayajua kwa sababu najua kuna wakati unaweka vitu lakini huoni matokeo. Jua matokeo yanakuja, na kadiri unavyowekeza, ndivyo unavyotengeneza matokeo makubwa ya baadaye.
Unakwenda kuwekeza nini leo?
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
http://www.makirita.info