Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa kwenye kile ambacho tumechagua kufanya.

Kumbuka hatima ya maisha yako ipo mikononi mwako.
Ni uamuzi wako yawe bora au yawe hovyo.
Asubuhi ya leo tutafakari MAMBO YANAPOKWENDA VIZURI, kwa sababi hapa ndipo wengi wanapopotea.
Najua utakuwa umeshaona watu wengi ambao walianza kufanikiwa lakini mafanikio yakapotea na kurudi kwenye maisha magumu.
Huenda wewe umewahi kupitia hatua hiyo, ya mambo kwenda vizuri lakini ghafla ukapoteza nafasi hiyo na kurudi kwenye msoto.
Iko hivi binadamu huwa tuna tabia ya kujisahau, tunaweza kuwa tumeteseka na kujitahidi sana mpaka kufikia hatua ya mambo kwenda vizuri. Ila tukishafika hapo tunajisahau, tunaona tumefika hapo kwa sababu sisi ni wajanja sana na tutakaa hapo daima.
Tunasahau kile kilichotufikisha pale na kuacha kukifanya. Mara ghafla tunaporomoka na kurudi chini kabisa.
Hili limekuwa linatokea kila mara kwa watu, mtu anaanza kazi kwa unyenyekevu, anapanda vyeo akifika juu kidogo anajisahau na hatimaye kupoteza kazi hiyo.
Mtu anaanza biashara kwa juhudi na kujinyima na kuweza kuikuza biashara yake mpaka inaanza kumtengenezea faids kubwa, anajisahau na kuanza kutumia fedha hovyo na kupunguza juhudi kwenye biashara yake.
Kwa hatua yoyote unayopiga, usijisahau, kumbuka vizuri ulipotoka na kumbuka kipi kimekufikisha hapo ulipo sasa. Usijisahaulishe hata siku moja, na mara zote ongeza juhudi zaidi.
Nakutakia siku njema sana.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
http://www.makirita.info