Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Tumepata nafasi nyingine nzuri na ya kipekee kwenda kuweka juhudi kubwa kwenye kile ambacho tumechagua kufanya.
Tumia muda wa leo vizuri rafiki.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUUZIWA.
Kwa bahati mbaya au nzuri, kila mtu kuna kitu anataka kukuuzia, iwe ni bidhaa, huduma, wazo, au hata imani.
Tunaweza kuona watu wanania nzuri na kile wanatuambia, lakini ukichunguza kwa ndani utagundua kuna kitu mtu anataka kukuuzia. Na mara nyingi watu huwa hawaweki hilo wazi, hasa kama wanataka kukuuzia kitu ambacho siyo muhimu kwako.
Dalili za kwamba mtu anataka kukuuzia kitu ni hizi;
💥Mtu akikuambia ipo njia rahisi na ya haraka ya kupata utajiri, ambayo haihusishi kuweka juhudi kubwa na muda, STUKA, KUNA KITU ANATAKA KUKUUZIA.
💥Mtu akikuambia ipo njia rahisi na ya haraka ya kupunguza uzito, ambayo haihusishi wewe kubadili mtindo wako wa kula, mtindo wa maisha na ufanyaji wa mazoezi, STUKA, KUNA KITU ANATAKA KUKUUZIA.
💥Katika vitu vyovyote vinavyofanana, labda A na B mtu akikuambia A ni bora kuliko B, STUKA, KUNA KITU ANATAKA KUKUUZIA.
💥Mtu akikuambia hii ni fursa ya kipekee, hutakuja kuipata tena, chukua hatua haraka sana sasa, STUKA, KUNA KITU ANATAKA KUKUUZIA.
💥Mtu akikuambia, chama fulani cha siasa ni bora kuliko chama kingine, STUKA, KUNA KITU ANATAKA KUKUUZIA.
Kwa kuwa kila mtu kuna kitu anauza, tatizo siyo watu kutuuzia, tatizo ni pale watu wanapokuuzia kitu ambacho siyo sahihi na hivyo kupoteza fedha na muda wako.
Kuwa makini kwenye kila jambo, hakikisha unajua ni nini mtu anataka kukuuzia na kina manufaa gani kwako.
Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
http://www.makirita.info