Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Tumepata nafasi nyingine ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili tuweze kupata matokeo bora.

img-20161217-wa0002
Tutumie siku hii ya leo vizuri rafiki.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUANZA KUFANYA.
Watu wengi wana mawazo makubwa na mazuri sana ya namna wanavyoweza kufanya maisha yao kuwa bora.
Wana mawazo bora ya kibiashara, kikazi na hata maisha kwa ujumla.
Lakini mawazo haya wako nayo siku zote na hawajaweza kuyatumia.
Wapo wanaojipa sababu kwamba bado hawajawa tayari, wengine wanafikiri bado wapo kwenye maandalizi.

Kitu ambacho nataka nikukumbushe asubuhi hii wewe rafiki yangu ni KUANZA KUFANYA.
Wazo lolote zuri ulilonalo, halitaweza kukusaidia kama huanzi kupiga hatua.
Mipango yote mizuri ambayo unaweka, haina manufaa kwako ikiwa hutaanza kuifanyia kazi.
Sababu yoyote unayojipa ya kusubiri, ni sababu ya kujidanganya.
Kwa sababu kama kitu ni kizuri na kama ni muhimu kweli kwako, basi inabidi uanze kukifanya.

Kuanza kufanya hakumaanishi utafanikiwa, na mara nyingi hutafanikiwa. Bali kuanza kufanya kunakupa faida ya kujifunza mengi ambayo hukuyajua awali.
Hivyo chochote unachofikiria, chochote unachopanga kufanya, anza kufanya na anza hata kwa hatua ndogo kabisa.
Unajifunza mengi kwa kufanya, unakuwa bora zaidi kwa kufanya.
Mipango ni mizuri, lakini kama hakuna utekelezaji, ni upotevu wa muda.
Kila dakika unayoitumia kurudia rudia mipango yako bila ya utekelezaji wowote, ni dakika ambayo umechagua kuipoteza.
Nafikiri unajua huna dakika nyingi za kupoteza kama unavyopoteza sasa.
Hivyo ANZA. KUFANYA.

Nakutakia siku njema sana rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
http://www.makirita.info