Hongera rafiki kwa siku hii mpya na nzuri sana ya leo. Ni nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora kabisa.

img-20161217-wa0002
Ule muda ambao ulikuwa unausubiri ndiyo umeshafika, jana ulisema utafanya kesho, na kesho yenyewe ndiyo leo. Hivyo usiahirishe tena kufanya leo.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu kile kinachotutoa kwenye safari ya mafanikio.
Kwa nini tunaweza kupanga mambo mazuri na makubwa, lakini kwenye kutekeleza tunashindwa? Kwa nini tunapoanza kufanya mambo tunaishia njiani na hatufiki kule tulipopanga kufika?
Jibu ni moja, tunakosa FOCUS.

Dunia tunayoishi ina kelele nyingi mno, ina mambo mengi ambayo yanatutamanisha kuondoka kwenye kile tunachofanya, kwa kuona mambo hayo ni muhimu zaidi. Kwa kushindwa kujizuia, tunajikita tumetekwa na mambo hayo na kuacha kile tunachokifanya.

Tunachopaswa kujua leo ni kwamba, hakuna kitu muhimu zaidi ya kile ambacho tumepanga sisi wenyewe kufanya. Kipaumbele chetu namba moja kabisa ni yale ambayo tumepanga kuyafanya.
Hivyo kuda wetu wote, nguvu zetu zote na akili zetu zote zinapaswa kuelekezwa kwenye jambo lile muhimu tunalofanya.
Haya mengine yanayoonekana muhimu lazima tuyaepuke kama tunataka kufanikiwa.
Facebook inaweza kusubiri,
Wasap inaweza kusubiri,
Instagram inaweza kusubiri,
Magazeti yanaweza kusubiri,
Tv na redio zinaweza kusubiri.
Kipaumbele chako namba moja ni ndoto yako na mipango uliyojiwekea.
FOCUS kwenye mambo hayo muhimu zaidi na utaona matokeo mazuri kwenye kile unachofanya.

Nakutakia siku njema sana rafiki yangu, leo kakomae kufanya mambo matatu muhimu sana kwako, hayo mengine yasahau kabisa.

Rafiki na kocha wako,
#KochaMakirita