Ulipozaliwa, ulikuwa mweupe kabisa, siyo weupe wa rangi, bali weupe kwamba hukuwa na chochote. Kama ni daftari basi tunasema halikuwa limeandikwa chochote. Lakini dakika chache baada ya kuzaliwa ulianza kujazwa vitu ambavyo vingi umeshikilia mpaka sasa, hujawahi kuvihoji kama vina msaada kwako au la.

Ulizaliwa ukiwa huna jina, kabisa, hadhi, dini, elimu wala mtazamo. Dakika chache baada ya kuzaliwa wakakupa jina, baadaye ukalibeba kabila la wazazi wako, kisha ukaibeba dini uliyowakuta nayo, ukaingia kwenye mfumo wa elimu na kujikuta unaishi kulingana na taratibu na tamaduni za jamii inayokuzunguka. Sisemi kwamba haya yote ni mabaya kwako, bali swali la msingi ni je yana msaada kwako? Je una uhakika siyo kikwazo cha wewe kuwa na maisha bora na yenye furaha? Hili ndilo tunalokwenda kuliangalia leo kwenye makala hii ya FALSAFA MPYA YA MAISHA.

Nikukaribishe rafiki yangu kwenye makala ye leo ya falsafa mpya ya maisha, ambapo tunachukua jukumu la kutengeneza falsafa ya maisha yetu, falsafa ambayo inatuwezesha kuwa na maisha bora na yenye furaha. Hili ni jukumu letu wenyewe, kwa sababu kulikwepa tunalazimika kuishi falsafa za wengine, ambazo haziendani na sisi.

Katika makala ya leo tunakwenda kuangalia falsafa za kuacha kuishi, hizi ni zile falsafa ambazo zimezoeleka kwenye jamii lakini hazina msaada kwetu, na wakati mwingine ni kikwazo kwetu kuwa na maisha bora na yenye furaha. Mara nyingi hatupati nafasi ya kuhoji falsafa hizi kwa sababu ndiyo tumekua nazo, ndiyo tunaziona kama sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Hivyo zinakuwa kikwazo kwetu na tusijue kipi cha kufanya.

Kumbuka jukumu la kwanza kabisa la mwanafalsafa ni kuwa na uhuru wa kimawazo, kuweza kuhoji chochote kile, CHOCHOTE kile bila ya kuhofia kwamba anakosea. Kama huwezi kuhoji kila kitu, ili kuchimba zaidi na kujiridhisha, huwezi kuwa mwanafalsafa. Leo kama wanafalsafa tunakwenda kuhoji kila kitu, na kama tutahoji kitu ambacho kitakuumiza, basi huenda bado hujakomaa kifalsafa. Kuhoji haimaanishi kupinga au kudharau, badala yake ni kutaka kujiridhisha ili unapoamua kuchukua hatua uchukue hatua moja unayoweza kuisimamia.

Zifuatazo ni falsafa ambazo tumekuwa tunaziishi kwenye jamii zetu na zimekuwa kikwazo kwa mafanikio yetu. Tuzihoji hapa na kujua hatua sahihi kwetu kuchukua.

  1. Bila ya elimu huwezi kuwa na maisha ya mafanikio.

Hii ni falsafa ambayo ilishika kasi sana wakati wa ujio wa mapinduzi ya viwanda na kuanzishwa kwa ajira rasmi. Kabla ya hapo kila mtu alifanya shughuli zake hivyo elimu ilikuwa sehemu ya kitu mtu anapenda kufanya, hasa elimu ya falsafa. Lakini ujio wa viwanda, na uhitaji wa wataalamu, mfumo rasmi wa elimu ulianzishwa na falsafa ikawa kwamba kama usiposoma huwezi kupata kazi nzuri na hivyo huwezi kuwa na maisha mazuri.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Acha Kuishi Falsafa Hizi Ambazo Zinakuzuia Kuishi Maisha Bora Na Ya Furaha.

Moja kwa moja falsafa hii ni ya uongo, uongo kabisa. Miaka zaidi ya elfu mbili iliyopita watu walikuwa na maisha bora na yenye mafanikio, japo hawakuwa na mfumo rasmi wa elimu. Zilikuwepo shule za falsafa tu, ambapo watu walisoma siyo waajiriwe, bali wajue zaidi kuhusu mazingira yao na kuhusu maisha kwa ujumla.

Hivyo sisemi kwamba elimu haifai, au elimu haina maana, kujua kusoma na kuandika ni hitaji muhimu mno kwa maisha yako. Kujua kuhusu mazingira yako ni muhimu mno. Kujua kuhusu historia za wale waliotutangulia ni muhimu sana.

Kitu ambacho tunakosea ni kuhusisha elimu na maisha ya mafanikio. Huu ulikuwa mkakati wa watu kupata wafanyakazi wa kudumu kwenye makampuni yao. Sasa hili linapotea kwa sababu tunaona nafasi za kazi siyo nyingi kama ilivyokuwa inafikiriwa huko nyuma. Na mashine zinachukua sehemu kubwa ya kazi za watu.

Hivyo basi mwanafalsafa mwenzangu, umuhimu wa elimu kwenye maisha yetu ni mkubwa, lakini mafanikio yetu yanatokana na namna tunavyoyachukulia maisha yetu na siyo kutokana na elimu tuliyonayo. Kama hilo la elimu kubwa ndiyo mafanikio makubwa, tungetegemea kila profesa awe na maisha ya mafanikio makubwa, lakini hilo siyo kweli. Hivyo hakuna uhusiano wa karibu kati ya elimu kubwa na mafanikio makubwa. Mafanikio yanatokana na maono ya mtu na namna anavyoyafanyia kazi, bila ya kujali ana elimu kubwa au la.

MUHIMU; Kinyume cha hii pia ni kweli. Tumekuwa tunaona hadithi za watu ambao hawakusoma au waliacha masomo na kisha kuwa mabilionea. Hivyo wengine wanatengeneza falsafa kwamba kufanikiwa hakuhitaji elimu, siyo kweli, elimu unaihitaji, lakini haina uhusiano na mafanikio. Elimu ni kwa ajili ya kustaarabika wewe binafsi, mafanikio utaamua wewe mwenyewe.

  1. Dini yetu ni bora (ya kweli) kuliko dini za wengine.

Dini nyingi zilijengwa kwenye misingi hii ili ziweze kukua na kustawi. Ilikuwa ni vita ya sisi dhidi ya wao, ukiwa kwenye dini yetu wewe ni mtu mtakatifu na utaiona mbingu. Ukiwa kwenye dini ya wale wewe ni mtu mwenye dhambi na utachomwa kwenye ziwa la moto milele. Na baadhi ya dini zinatoa majina ya ajabu kabisa kwa wale ambao hawaamini kwenye dini hizo.

SOMA; Tumia Vikwazo Ulivyonavyo Kufikia Mafanikio.

Najua hili litakuumiza lakini nikuambie tu ni uongo. Siyo kweli kwamba dini yako wewe ni bora kuliko dini za wengine. Siyo kweli kwamba dini yako wewe ndiyo ya kweli na ya wokovu kuliko za wengine. Kama tutaangalia ubora basi tunaweza kusema dini zote ni bora na dini zote siyo bora. Kama tutaangalia ukweli basi tunaweza kusema dini zote ni za kweli na dini zote ni za uongo. Inategemea wewe unaangalia wapi.

Swala la dini bora na ya kweli kuliko nyingine lilianzishwa wakati wa uanzilishi na ukuaji wa dini mbalimbali. Ili kupata wafuasi, ilibidi dini hizi ziwaoneshe watu kwamba kuwa upande huu ni sahihi kuliko upande ule. Hili limekuwa na faida kwenye dini katika kupata wafuasi, lakini halina faida kwa wale wafuasi.

Kukubali kwamba dini yako ni bora kuliko ya wengine, kunaharibu ushirikiano na wengine, kunatengeneza uhasama ambao tumeona umekuwa unaitesa dunia.

Wewe kama mwanafalsafa, elewa kwamba dini yako ni sahihi na ya mwingine pia ni sahihi. Elewa kwamba kila mtu anaamini kile anachoamini kulingana na namna anavyoyachukulia maisha na namba alivyokuzwa. Huenda wewe ungezaliwa na wazazi wa dini tofauti na uliyopo sasa, ungekuwa mfuasi wa dini ile ya tofauti.

Ukishamaliza hilo la dini ipi bora na ipi siyo bora, sasa turudi kwenye dini yako. Je kipi unakipata kwenye dini yako? Unapata ukuaji wa kiroho? Unakua zaidi kiimani? Au unaishia kuwa tu mfuasi wa dini, kuhudhuria ibada na kutoa sadaka kwa sababu ndivyo kila mtu anavyofanya? Ni lazima dini yoyote unayoifuata, ikusaidie kukua kiroho na kuimarisha imani yako kwenye maisha. Imani hiyo ndiyo ikuwezeshe kupambana na changamoto za maisha na hata kufikia mafanikio. Usiwe tu mfuasi kwa sababu umejikuta pale, hoji na kama hupati majibu sahihi, yatafute majibu sahihi, usikubali kuwa mfungwa wa dini, kuwa huru kiimani na kiroho.

  1. Kama ipo ipo tu.

Falsafa nyingine hiyo hapo, imetengeneza wazembe wengi, ambao hawataki kuchukua hatua, kwa sababu jamii kwa namna fulani imewaaminisha kwamba kuna watu ambao wametengenewa kufanikiwa na kupata, na wengine hawajatengewa kufanikiwa. Hivyo juhudi zozote ambazo mtu atachukua, haziwezi kubadili hali hiyo.

Naomba nikuambie hapa haraka sana na mara moja ya kwamba huu siyo ukweli. Siyo kweli kwama kama ipo ipo tu, siyo kweli kwamba kuna watu wachache ambao wametengewa mafanikio na wengine hawawezi kufanikiwa. Siyo kweli kwamba masikini ataendelea kuwa masikini hata afanye nini?

Ukweli ni kwamba maisha yanakupa kile unachokipigania. Ukikubali maisha ya chini utaendelea kupata hayo. Ukiyakataa na kutaka maisha bora zaidi utayapata pia. Dunia haiwezi kumbishia mtu ambaye ameamua kweli kutoka pale alipo na kupiga hatua. Na pia dunia haiwezi kumbeba mtu ambaye ameamua kulala.

Juhudi zina mchango mkubwa wa popote unapotaka kufika, weka juhudi na sahau kabisa falsafa za kukukatisha tamaa.

  1. Aliyekupa wewe ndiye aliyeninyima mimi.

Ningekuwa na mamlaka ningemfuta uanafalsafa mtu yeyote anayetumia kauli hii. Kwa kifupi namaanisha hustahili kuwa mwanafalsafa kama unaamini yupo anayegawa, na kwa sababu fulani amewapa wengine na kukunyima wewe.

SOMA; Sababu Namba Moja Kwa Nini Hufanikiwi Kwenye Kazi Unayofanya.

Hii ni kauli ya kukata tamaa na kuwaonea wengine wivu, hii ni kauli ya kujishusha na kujiona hufai. Na hii ni kauli ya kuficha uzembe wako, kwa sababu hujaweza kuweka juhudi na kupata, basi unajiaminisha wengine wamepewa na wewe umenyimwa.

Acha kabisa kauli hii, futa kabisa falsafa hii kwenye akili yako. Na fanyia kazi chochote unachokitaka.

Iko hivi mwanafalsafa mwenzangu, haijalishi imani yako ya dini ikoje, chochote tunachokitaka, kipo hapa duniani. Na dunia haijui hata kama upo, dunia inaendelea na mambo yake kama kawaida, itaendelea kujizungusha kwenye mhimili wake, na itaendelea kulizunguka jua, kila siku, iwe wewe utaamka au utalala. Dunia haitasubiri wewe mpaka uwe tayari, dunia inafanya yake.

Hivyo kama wewe hutafanya yako, unachagua mwenyewe kubaki nyuma. Kama unawaona wenzako wanapata ambayo wewe hupati, usijidanganye kwamba wao wamepewa na wewe umenyimwa, jiambie ukweli kwamba kuna mambo wanafanya ambayo wewe hufanyi, hivyo jifunze na yafanye hayo utapata matokeo mazuri pia.

  1. Kazi fulani ndiyo zenye mafanikio, nyingine hazina mafanikio.

Hakuna kitu kimeharibu watu kama falsafa hii kwamba kazi fulani ndiyo zina maisha ya mafanikio, na jamii imetengeneza picha hii kwa muda mrefu ambayo imeharibu sana maisha ya watu. Mwulize mtoto mdogo ambaye ameshafika shuleni anataka kufanya kazi gani atakapokuwa mtu mzima, atakuambua daktari, rubani, mwalimu, mhasibu na polisi. Karibu watoto wote wanajibu hivyo. Lakini tunapokuja kwenye uhalisia, siyo kila mtu kwenye jamii ni daktari, mwalimu, rubani, polisi au mhasibu. Watu hawa ni wachache mno, wengi wanafanya kazi za kawaida kabisa. Huenda na wewe ni mmoja wa waliosema kazi hizo ukiwa mdogo na sasa unafanya vitu tofauti kabisa.

Siyo kweli kwamba mafanikio yapo kwenye kazi fulani fulani tu, mafanikio ni kile mtu anachoamua yeye mwenyewe. Hata anayefanya usafi kwenye ofisi au anayezoa matakataka anaweza kuwa na maisha ya mafanikio, kama ataamua kuwa na maisha ya mafanikio.

Uongo huu pia umeingia mpaka kwenye biashara, kuna biashara ambazi zinaonekana ndiyo zenye mafanikio, biashara za madini, fedha na vyombo vya moto. Lakini wapo wauza mkaa ambao wana maisha ya mafanikio.

Falsafa hii siyo tu ya uongo, bali pia inavuruga na kuharibu maisha ya wengi. Kwa mfano, mtu aliyeamini kwenye maisha yake kwamba kuwa daktari ndiyo mafanikio kwenye maisha yake, ila akashindwa kufaulu masomo ya sayansi, ataishi maisha yake akisema kama ninge…. atashindwa kuyafurahia yale maisha aliyonayo sasa na kuwaambalia madaktari kama watu ambao wana maisha mazuri kuliko yeye. Na wakati huo pia kuna aliyeweza kuufikia udaktari, lakini baada ya kuingia kwenye kazi hayaoni yale mafanikio aliyofikiria angekutana nayo.

Nirudie tena mwanafalsafa mwenzangu, mafanikio ni kile unachoamua wewe mwenyewe, popote ulipo na kwa chochote unachofanya. Hakuna kazi fulani ambazo zimetengwa kwa ajili ya mafanikio na nyingine ni za kusukuma tu siku.

Zipo falsafa nyingi za uongo ambazo tumelishwa na kuaminishwa, hizi ni chache tu. Kwa maarifa haya endelea kuhoji falsafa nyingine zote ambazo umekuwa unaenda nazo. Hoji kila kitu, hoji na kuona kama unachoamini ni sahihi au la. Ukishahoji na kujua ukweli ni upi, usikubali tena kurudi nyuma, hata kama kila mtu kwenye jamii anafanya kile ambacho wewe umegundua siyo sahihi. Wanafalsafa wote wamekuwa wanaonekana ni watu wanaokosea mpaka pale ukweli unapokuja kuwekwa hadharani.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.