Habari za leo rafiki?

Changamoto ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku na ni kupitia changamoto ndipo tunapojifunza na kupiga hatua zaidi. Bila ya changamoto maisha yasingekuwa na raha ya kuishi, kwa sababu kila kitu kingekwenda vizuri na kusingekuwa na haja ya kufikiri zaidi na kupambana zaidi. Lakini pia changamoto nyingine zinatokana na sisi wenyewe kukosa maarifa sahihi ya kufanya mambo, hivyo tunapopata maarifa changamoto hizo zinatoweka kwa sababu tunakuwa tumepata uwezo wa kufanya maamuzi sahihi. 

 

Swala la kuwasaidia wengine moja kwa moja kifedha imekuwa ni changamoto kubwa kwa wengi. Imekuwa inawakwamisha wengi kupiga hatua kwa sababu kipato kidogo wanachopata kinakuwa kinategemewa na wengi. Na tatizo kubwa kwenye utegemezi wa aina hiyo ni kwamba watu wakishajua wanapata fedha sehemu fulani, basi mawazo yao yote yanapelekwa pale, hawafikirii tena njia nyingine za kutatua changamoto zao.

SOMA; Mambo Muhimu Ya Kufanya Pale Ndugu Zako Wanapokuona Wewe Ni Mbaya(Mchawi) Kwa Sababu Una Mafanikio.

Leo kupitia makala hii ya ushauri wa changamoto tunakwenda kuangalia namna ya kuondokana na changamoto hii ya mzigo wa kuwasaidia wengine na pia tutaangalia njia bora kabisa ya kuweza kuwasaidia watu wengine.

Kabla hatujaangalia nini cha kufanya, tupate maoni ya msomaji mwenzetu anayesumbuliwa na changamoto hii;

Ni kwamba kwa miezi minne nina uwezo wa kupata milioni moja ya Kitanzania lakini hainisaidii maana sioni umuhimu wake kwani nikiipata inaisha bila kujua ndani ya mwezi maana nina huruma sana na watu wanaoniomba pesa kwani wanajua napokea kiasi kikubwa cha pesa ndani ya muda huo na tendo hili hunilazimu niwasaidie na mwishowe najikuta sina pesa tena mpaka nisubiri miezi mingine minne tena na nikizipata mwendo ni uleule zinaisha tu wakati malengo yangu makubwa ni kufanya biashara kupitia hiyo pesa ili nipate pesa ya kutosha niweze kuwainua hawa wanaoniomba pesa lakini inashindikana TAFADHALI USHAURI. ANSIGARIUS K. M.

Rafiki, hivi ndivyo changamoto hii ya utegemezi inavyokuwa mzigo kwa wengi. Watu wanashindwa kupiga hatua kwenye maisha sababu ya utegemezi mkubwa kutoka kwa wengine. 

Lakini ipo njia ya kuweza kuondokana na hili na kuweza kutengeneza uhuru wa kifedha pamoja na kuwasaidia wengine vizuri zaidi. Hapa tutajadili njia hizo.

1. Saidia kulingana na uwezo wako.

Kusaidia ni kuzuri kwa sababu ni kweli wapo watu wenye uhitaji zaidi yetu sisi, lakini kusaidia mpaka wewe mwenyewe unabaki huna kitu siyo kitu kizuri, humsaidii yule unayefikiria unamsaidia na wewe mwenyewe unajiweka kwenye hali mbaya zaidi. Wape watu msaada kulingana na uwezo wako na hivyo ili kuhakikisha mambo yako yanakwenda vizuri, kuwa na kiwango maalumu cha kutoa msaada kwa wale wenye uhitaji. Na kila mwezi au wakati mwingine wa malipo kwako, msaada wako usizidi kiwango kile.

Kwa mfano unaweza kuchagua kwamba asilimia 10 ya kipato chako ndiyo utakayotoa msaada. Toa msaada wa kiasi hicho na kikishaisha usitoe tena, subiri mpaka kipato kingine. Kwa njia hii utaweza kutenga fedha kwa ajili ya mambo mengine muhimu kwenye maisha yako kama biashara na uwekezaji ili baadaye uweze kufikia uhuru wa kifedha.

SOMA; Jinsi Ya Kuepuka Dharura Zako Na Za Wengine Kuwa Kikwazo Cha Kufikia Malengo Yako.

mtu kujua una fedha au huna.

Kosa kubwa ambalo watu wengi wamekuwa wanafanya ni kuruhusu kila mtu ajue kwamba sasa hivi ana fedha au la. Hujawahi kujiuliza kwa nini ukiwa na fedha watu wanakuja na shida kubwa na muhimu sana wewe kuwasaidia, lakini ukiwa huna fedha watu hao huwaoni?

Hii ni kwa sababu watu wakishajua una fedha, basi wanapata sababu kubwa ya kukueleza ili uwapatie fedha, ndivyo tabia za binadamu zilivyo.

Watu wengi wanapopata fedha tabia zao hubadilika kabisa. Ataanza kutoa ofa zisizo na msingi, ataanza kufanya manunuzi ambayo hayakuwa yamepangiliwa na hata mwonekano wake unabadilika. Na kwa wale ambao ni walevi, ndiyo kabisa dunia nzima itajua kwamba wana fedha. Watu hawa fedha zinapoisha kila mtu anajua kwa sababu wananyong’onyea, hawaonekani kabisa.

Kama ulishajenga utaratibu huu wa kimaisha, wa watu kujua kirahisi kwamba una fedha au huna, uvunje haraka. Vunja utaratibu huo ili watu waache kukutabiria na kupata fedha kutoka kwako kirahisi.

Hata kama umeajiriwa na watu wanajua mwisho wa mwezi unapokea mshahara, bado usikubali kuonekana mwisho wa mwezi una fedha. Endesha maisha yako kwa usawa kila siku na watu wasiweze kukutabiria kiurahisi kama una fedha ua la. Kwa njia hii utaepusha wale ambao hawana uhitaji sana ila wanatengeneza uhitaji pale wanapojua kwamba una fedha.

3. Ikumbuke njia bora kabisa ya kuwasaidia masikini.

Unaijua njia bora kabisa ya kuwasaidia masikini? Ni wewe kutokuwa masikini. Sasa unapowasaidia watu na wewe kubaki huna kitu, hujawasaidia chochote, kwa sababu na wewe unakuwa mmoja wao kwamba huna kitu. Mnapokuwa wote hamna kitu baadaye hakuna atakayeweza kumsaidia mwenzake. Kama ni ajira unayo, siku ikiisha wote mnakuwa wa kusaidiwa.

Hivyo wakati unawasaidia wengine fikiria sana hili, je kuwasaidia kwako wengine kunakuacha wewe ukiwa na shida zaidi ya wao? Kama jibu ni ndiyo kaa chini na ujipange upya.

4. Usiwape watu samaki, wafundishe namna ya kuvua samaki.

Ukimpa mtu samaki atamla halafu atarudi tena kwako akitaka samaki. Ukimfundisha mtu namna ya kuvua samaki utampa uhuru wa maisha yake na kuondoa utegemezi kwako. Hivi pia ndivyo ilivyo kwenye msaada wa kifedha. Ukiwapa watu fedha watazitumia na zikiisha watarudi tena kwako, kwa sababu fedha siku zote huwa hazitoshi na matatizo ni mengi. Lakini kama utawafundisha watu hao namna ya kujitengenezea kipato chao wenyewe, utawatengenezea uhuru wa kifedha na wewe utakuwa huru pia.

SOMA; Kama Unajibebesha Mizigo Hii Katika Maisha Yako, Sahau Kuhusu Mafanikio.

Hivyo kwa kila mtu anayekutegemea, angalia ni kwa namna gani unaweza kumtengenezea njia ya kumwingizia kipato, hata kama ni kidogo sana. Faida nyingine ya kufanya hivi ni kumfanya mtu aone uchungu wa kutafuta fedha hivyo kuzitumia vizuri. Mtu anapopata fedha kirahisi, haoni uchungu wake na anazitumia kirahisi.

5. Kumbuka sheria kuu ya fedha kwako.

Kama utashindwa kufuata hayo manne niliyokushirikisha hapo juu, basi kila unapopata fedha kumbuka sheria kuu ya fedha kwako, ambayo ni JILIPE WEWE MWENYEWE KWANZA. Hata kama huwezi kabisa kuacha kuwasaidia wengine, kwa sababu hawajiwezi kabisa na wanakutegemea wewe moja kwa moja, basi kumbuka hili; JILIPE WEWE MWENYEWE KWANZA.

Kwa kila kipato chako tenga asilimia ambayo unajilipa, isipungue asilimia kumi. Na unapopokea kipato jilipe, ile inayobaki sasa unaweza kufanya chochote unachotaka, unaweza hata kuigawa yote, lakini, chonde chonde usiguse ile ambayo umejilipa wewe mwenyewe. Hii uliyojilipa siyo kwa ajili ya msaada au dharura, bali kwa ajili ya uwekezaji ili uweze kufikia uhuru wa kifedha hapo baadaye. Weka fedha hiyo kwenye mfumo ambao huwezi kuziumia hata kama una shida kiasi gani. Mfano kuweka kwenye akaunti maalumu au kuwekeza kwenye mifuko ambayo hutoi kwa urahisi kama ukiweka benki.

Anza kujilipa wewe mwenyewe kwanza kwa kila kipato, na inayobaki itumie kadiri unavyoona inafaa.

Fanyia kazi mambo haya matano muhimu tuliyojifunza kuhusu kutoa msaada kwa wengine kwa kuondokana na mzigo wa utegemezi na kuwawezesha watu kujitengenezea kipato chao wenyewe. Ni muhimu sana uzingatie haya ili na wewe mwenyewe uweze kufikia uhuru wa kifedha.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.

Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea MOBILE UNIVERSITY, bonyeza hayo maandishi.