Hongera rafiki yangu kwa siku hii bora sana ya leo.
Hii ni nafasi ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.
Tutumie muda wetu wa leo vizuri rafiki.

img-20161217-wa0002

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu SAA MOJA KILA SIKU.
Iwapo utatumia saa moja kila siku, siku tano za wiki kujifunza kitu fulani, ndani ya miaka mitano utakuwa mtaalamu uliyebobea kwenye kitu hicho.
Yaani iwapo utatenge saa moja tu na kuiwekeza kujifunza kile unachofanya, au kile unachotaka kufanya, kadiri unavyokwenda utaelewa zaidi na utafika hatua unajua nje ndani ya kile unachofanya.

Kama ni biashara utajua kila eneo la biadhara hiyo, changamoto kuu na namna ya kuzivuka, wateja na tabia zao, mwenendo wa biashara na matarajio ya baadaye na mengine mengi zaidi.

Kama ni utaalamu utaelewa mengi zaidi kuhusu taaluka hiyo, utaona njia bora zaidi za kuwasaidia wengine na hatua bora zaidi za kupiga.
Hii ni kwa kutenga saa moja tu kila siku na kujifunza kuhusu eneo unalotaka kuwa bora.
Vipi ukiamua kutenga masaa mawili au zaidi? Hakika utafika mbali ndani ya muda mfupi zaidi.

Kama ulikuwa hujaanza hili anza sasa, katika masaa yako 24 ya siku, tenga saa moja ya kujifunza kwa undani kuhusu kile unachofanya au unachotaka kufanya. Tengeneza nidhamu ya kufuata hilo kila siku, na utaweza kufanya makubwa sana.

Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki yako,
#KochaMakirita