Naongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ilinkuweza kupata matokeo bora.

IMG_20170102_073855
Tufanye makubwa leo kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu kuiambia dunia kwamba wewe ni bora,
Hili ni jambo ambalo unapaswa kulifanya kila mara, iambie dunia kwamba wewe bora na onesha wazi wazi ubora wako jinsi ulivyo.
Najua hili linakwenda kinyume na mazoea yetu kwenye jamii,
Tunaambiwa tusijisifu wenyewe bali tusubiri wengine watusifu,
Ukisema wewe ni bora wengine wanaona unaringa au unajiona sana,
Lakini kumbuka hayo yote ni mapungufu ya jamii ambayo yamewafanya wengi kuendelea kuwa kawaida.
Jamii haipendi watu ambao siyo wa kawaida, na ndiyo maana utakapoiambia dunia wewe ni bora, kuna namna ambavyo itageuza hilo lionekane ni baya.
Ni muhimu sana uiambie dunia wewe ni bora kwa sababu;
1. Kelele ni nyingi sana, wengi hawajui hata kama upo, wamezwa na kelele nyingi, hivyo unahitaji kuhakikisha wale wanaohitaji uwepo wako wanajua upo.
2. Kila mtu anaweza kufanya kila kitu, watu wanaangalia ubora. Na kwa kuwa wengi unaoanza kufanya nao kazi hawakujui, wanahitaji kuanza kupata hamasa kupitia maneno yako. Unapowaambia wewe ni bora, unawashawishi wakujaribu, unapoonesha ubora huo wanakuwa na wewe daima.

Iambie dunia wewe ni bora, na kila nafasi unayoipata onesha ubora mkubwa uliopo ndani yako. Baada ya muda kila mtu atakuwa anazungumzia ubora wako na siyo wewe mwenyewe kuuzungumzia.

Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz