Umeianzaje siku hii nzuri ya leo rafiki?
Ni matumaini yangu upo vizuri na umeshajipanga vyema kuhakikisha leo hii unakwenda kufanya makubwa.

img-20161217-wa0002
Ni kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo utaweza kufanya makubwa zaidi siku hii ya leo.
Hata dakika moja usisahau msingi huo wa mafanikio.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUFANYA VIZURI,
Ninachoamini ni kwamba, chochote ambacho unafanya kwenye maisha yako, kuanzia kazi, biashara na maisha kwa ujumla, umechagua wewe mwenyewe. Na hata kama hukuchagua basi umeridhika na unachofanya ndiyo maana mpaka sasa unafanya. Ingekuwa hujaridhika ungeshaacha zamani sana na kufanya kile kinachokuridhisha.

Sasa ambacho sikielewi ni pale unapofanya kile ulichochagua kufanya kwa ukawaida, unaamua kufanya hovyo, wala hujali matokeo gani unazalisha. Wewe mwenyewe umekubali kufanya, halafu unaamua kufanya hovyo. Hii siyo sawa kabisa.
Chochote kile unachochagua kufanya, chagua kukifanya vizuri sana, kadiri ya uwezo wako. Weka juhudi zako zote, weka maarifa yako yote na hakikisha unatoa matokeo bora kabisa.
Dunia ya sasa, njia ya uhakika ya kutokufanikiwa na kupotea kabisa, ni kufanya mambo ya kawaida, kufanya mambo ya hovyo.
Hakuna atakayehangaika na wewe, utajipoteza mwenyewe taratibu.

Hata kama umechagua kufagia barabara, ifagie vizuri sana, mpaka kila anayepita kwenye barabara ile aseme hapa pamefagiliwa vizuri sana.

Una uwezo wa kufanya kazi zako vizuri na kwa ubora,
Amua kuanza leo na weka juhudi kila siku.
Unapimwa kwa unachozalisha.

Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT