Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa u buheri wa afya na unaendelea vema katika shughuli zako unazozifanya. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo, ni siku ya kipekee sana kwako kwenda kufanya kilicho bora na kutegemea kupata kilicho bora.

Mpendwa msomaji, nipende kutumia nafasi hii kukualika tena katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja mada nzuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Rafiki, tafadhali twende sanjari na mimi mpaka pale tamati ya kipindi chetu cha leo.

Katika somo letu la leo tutakwenda kujifunza wote kwa pamoja chumvi iliyokosa au kupoteza thamani katika zama hizi za taarifa. Je unaijua ni chumvi gani? karibu sana mpendwa msomaji tuweze kujifunza wote kwa pamoja.

SOMA; Sehemu Kubwa Ya Watanzania Hatufanyi Kazi, Na Hili Ni Tatizo Kubwa Kwa Maendeleo.

Kwa kufanya tafakari ya kawaida, wote tunaelewa ya kwamba kazi ya chumvi ni kuleta ladha kwenye chakula. Na chakula kisichokuwa na chumvi kinakuwa kimekosa ladha kabisa hata ukila chakula ambacho hakina chumvi hufurahii kuendelea kula chakula. Kama tunavyojua zamani kabla ya kugundulika kwa teknolojia ya kuhifadhia vyakula yaani majokofu watu walikuwa wanatumia chumvi ili kusaidia chakula au kitoweo kama vile nyama kuweza kukaa kwa muda mrefu bila kuharibika.

Katika maisha yetu sisi binadamu hapa duniani tumealikwa kuwa chumvi, swali la kujiuliza miongoni mwetu tumeshakuwa kama chumvi iliyokosa ladha katika chakula. Wengi wameshapoteza ladha katika mahusiano yao, yawe ni mahusiano ya kindugu, jamaa, rafiki na hata mahusiano ya kimapenzi yaani mke na mume au wachumba wanaotarajia kufunga ndoa baadaye. Inawezekana hapo ulipo umeshakuwa ni chumvi isiyokuwa na thamani katika maisha ya watu.

Katika tafakari hii ya chumvi, sisi binadamu tumealikwa kuwa chumvi duniani sasa swali la kujiuliza je wewe ni chumvi iliyopoteza thamani au ni chumvi yenye thamani? Kama tunavyojua katika hali ya kawaida chumvi iliyopoteza thamani ni ile chumvi ambayo haina ladha kwenye chakula, kumbe basi, kama wewe ni chumvi iliyopoteza thamani basi umekuwa huna ladha. 

Katika tafakari hii chumvi ni sisi binadamu na chakula ndiyo dunia, chumvi ile yenye thamani ndiyo chumvi yenye ladha inayohitajika duniani.

SOMA; Jinsi ya kugeuza kipaji chako kuwa biashara inayokuingizia kipato.

Mpendwa msomaji, mpaka hapa umeshajigundua je wewe ni chumvi yenye thamani duniani au ni chumvi iliyopoteza ladha duniani? Kama sisi ndiyo chumvi na matendo yetu ndiyo yanaleta uhai duniani. Huwezi kuhubiri haki kama wewe siyo mtu mwenye haki, kama wewe ni chumvi yenye thamani basi matendo yako ndiyo yatadhihirisha kuwa wewe ni uhai.

Kwa hiyo, matendo yetu yamepoteza ladha katika dunia ya leo. Kama wewe huna thamani unayotoa basi ni chumvi iliyopoteza ladha yaani huna thamani unayotoa duniani. Matendo yako yaleta uhai katika dunia? Maandiko ya Biblia yanatualika kwa kusema zaeni mkaijaze dunia je unafikiri utawezaje kuijaza dunia kama wewe ni chumvi iliyopoteza thamani? Wewe ni chumvi iliyopoteza thamani? Kama wewe ni chumvi iliyopoteza thamani maana yake chakula chako kitakuwa hakina ladha, je ni nani ambaye ataweza kula chakula ambacho hakina ladha wakati kuna chakula chenye ladha?

SOMA; Tabia Moja Ya Binadamu Ambayo Unaweza Kuitumia Kunufaika Kibiashara.

Rafiki, huenda umeshakuwa chumvi ilipoteza thamani yaani isiyokuwa na ladha katika familia yako, huna ladha kwa mwenza wako, huna ladha kwa watoto wako na hata kwa jamii nzima umeshakufa tayari mioyoni mwa watu. Wewe ni kiongozi je wewe ni chumvi yenye thamani au ni chumvi iliyopoteza ladha? Huenda umeshapoteza ladha kwa watu unaowaongoza je umechukua hatua gani? Huenda umeshapoteza ladha katika huduma unayotoa, wateja wako siku hizi wanakukimbia kwa sababu umepoteza ladha kwao yaani umekuwa chumvi isiyokuwa na thamani.

Hatua ya kuchukua leo, jiulize swali hili? Je wewe ni chumvi yenye thamani au ni chumvi iliyopoteza ladha? Fanya tafakari kwa kuchunguza maisha yako, matendo na mwenendo mzima wa maisha yako unaendaje. Chagua kuwa chumvi yenye ladha hapa duniani na siyo chumvi isiyokuwa na thamani na kuwa ladha inayoleta ubora katika jamii.

Kwa hiyo, maisha yetu ndiyo yanaleta uhai, jinsi matendo yako yalivyo ndivyo yanadhihirisha kama wewe ni chumvi yenye thamani au chumvi iliyokosa ladha. Kazi ya chumvi ni kuleta ladha kwenye chakula hivyo jitahidi kuwa chumvi yenye ladha mahali popote ulipo. Nikuache uendelee na tafakari hii ya chumvi kwa kina zaidi kwa kuangaza maeneo mbalimbali ya maisha.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com