Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni siku nyingine mpya kabisa ambapo tumepata nafasi nyingine ya kwenda kuweka juhudi zaidi leo ili kupata matokeo bora zaidi.

IMG_20170102_073855
Ni kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambao tuna uhakika wa kufanya makubwa kwenye siku yetu hii nzuri sana ya leo.

Asubuhi ya leo tutafakari NANI ALIYETUNGA HIZO SHERIA?
Unapoamua kushika hatamu ya maisha yako,
Unapoamua kufanikiwa licha ya changamoto zote unazopitia,
Unapoamua kutangaza vita na umasikini na kuhakikisha unakuwa tajiri,
Unapoamua kupambana mpaka tone lako la mwisho kuhakikisha unafanikiwa,
Wapo watu watakaokuja na hadithi zao kukuonesha kwamba wewe haupo sahihi..
Utakapowaambia ndoto zako kubwa wanakuambia kwa nini ujisumbue na hayo makubwa, kwa nini usiridhike na kile unachopata sasa?
Utakapowaambia huutaki tena umasikini na lazima uwe tajiri, watakuambia una tamaa ya fedha,
Utakapofanya kazi zaidi ya muda wa kawaida watakuambia unapenda sana kazi,
Utakapowaambia hapana kwa mahitaji yao ambayo siyo muhimu kwa muda na fedha zako watakuambia unaringa,
Kwa vyovyote vile, chochote cha tofauti ambacho utafanya, watu watatafuta njia ya kukifanya kionekane siyo sahihi.

Swali moja muhimu la kujiuliza, ambalo linafanya hayo yote yasikuzuie ni hili; NANI ALIYETUNGA HIZO SHERIA?
Jiulize nani aliyetunga hiyo sheria ya namna watu wanapaswa kufanya kazi kawaida?
Nani aliyetunga hiyo sheria ya watu wasipende fedha?
Nani aliyetunga hiyo sheria ya kusema ndiyo kwenye kila kitu ambacho watu wanataka kwako?
Ukijiukiza swali hili, utagundua hizi ni sheria za hovyo ambazo watu wanajiwekea wenyewe.
Na sheria hizi zinafuatwa zaidi na wale ambao wameshindwa, ambao hawana mafanikio.
Hivyo uchaguzi ni wako, ufuate sheria hizo na uishie kushindwa, kuwa wa kawaida na kuwa masikini au uvunje sheria hizo na kuishi maisha ya kafanikio?
Maisha ni yako na uchaguzi ni wako.
Chagua sawasawa.

Uwe na siku bora sana leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT