Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa uko salama siku hii ya leo na unaendelea vizuri kabisa katika shughuli zako za kila siku. Leo ni siku ya kwanza kabisa ya mwezi wa tatu katika mwaka 2017, ni zawadi ya kipekee kwetu kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha. Kama unavyojua wako wenzetu waliotamani kuweza kufika siku hii ya leo lakini hawakuweza kufika, kwa hiyo tunaalikwa kumshukuru Mungu kila wakati kwa kuweza kutustahilisha tena mimi na wewe siku hii.

 

Leo ni siku bora sana na ya kipekee kwetu hivyo tunakwenda kufanya makubwa na kutegemea kupata makubwa, tusimamie nidhamu, uadilifu na kujituma katika siku yetu hii ya leo. Tunaalikwa kutumia vizuri muda wetu wa leo katika kuzalisha mambo chanya na siyo hasi, tumia zawadi yako ya muda vizuri kwani ukipoteza muda huwezi kuupata tena.

Mpendwa msomaji, nipende kukualika tena katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia. Leo tutakwenda kujifunza kitu kinacholeta jawabu la mambo yote hapa duniani, je unajua jawabu la mambo yote hapa duniani? Karibu mpenzi msomaji tuweze kusafiri pamoja hadi pale tamati ya kipindi chetu cha leo.

Huwezi kuona thamani ya hewa unayoivuta sasa mpaka pale utakapoikosa, hewa tunayoivuta huwa haionekani kwa macho kama vile ilivyo katika imani zetu. Kwa hiyo, hewa au pumzi unayovuta ndiyo kitu cha kwanza kabisa muhimu katika maisha ya binadamu kwa sababu ukikosa kuvuta pumzi maana yake huwezi kuendelea tena kuishi hapa duniani. Licha ya hewa kuwa muhimu na kitu cha kwanza katika maisha ya binadamu lakini pia kuna msaidizi wake wa pili ambacho ni muhimu sana ukiachana na hii pumzi tunayovuta sasa.

SOMA; Kitu Cha Kuepuka Kuongozwa Nacho Katika Ulimwengu Wa Mambo Leo.

Mpendwa msomaji, baada ya kuona kuwa hewa ni kitu cha kwanza kabisa muhimu, kwa sisi binadamu, basi kuna kitu ambacho katika maisha yetu ya kila siku huwa ndiyo jawabu la mambo yote. Mpendwa msomaji, ‘’fedha huleta jawabu la mambo yote’’ hakuna binadamu anayekataa kuwa fedha huleta jawabu la mambo yote, fedha hutatua matatizo yetu hapa duniani ndiyo maana huwezi kwenda sehemu kupata huduma bure, huwezi kupata huduma bila kulipia gharama.

Mpendwa msomaji, fedha huleta jawabu la mambo yote hata mhubiri sura ya kumi mstari wa kumi na tisa anadhihirisha hili. Matatizo mengi yanayomwandama binadamu chanzo chake kikuu ni fedha na wala siyo kitu kingine. Jaribu siku moja tembelea tu hospitalini wodi mbalimbali nenda kajionee wewe mwenye wagonjwa wanavyoteseka kwa kukosa matibabu na kupata vipimo sahihi kwa ajili ya kukosa fedha. Kwa hiyo, watu wengine wanapoteza maisha kwa kukosa fedha ya kuchangia gharama za matibabu, maisha yetu ili yaweze kwenda vizuri kila siku na kupata mahitaji yetu ya kila siku hayawezi kwenda hivi hivi bila kuwa na fedha. Yale mahitaji ya msingi ya binadamu kama vile nguo, chakula na malazi huwezi kuyapata bure kama hauna fedha, ndiyo mhubiri anatualika sisi sote kuwa fedha huleta jawabu la mambo yote.

Mpendwa rafiki, usikubali kujifariji na umaskini kwani umaskini hauna faida katika maisha yako, ni bora kufanya maamuzi na kufunga ndoa na utajiri na kuupa umaskini talaka kwani fedha huleta jawabu la mambo yote hapa duniani. Matatizo mengi hapa duniani yanamwandama maskini, sasa usiendelee kujifariji na umaskini bali kuamua kuweka juhudi na kupambana kutoka katika umaskini.

SOMA; Ushauri Unaoweza Kuwapa Vijana Ambao Hawana Ajira Ila Wanataka Kutoka Kimaisha.

Mpendwa msomaji, kuna watu wanajifariji na kusema hata katika kitabu cha Biblia imeandikwa ya kuwa ni rahisi ngamia kupenya kwenye tundu la sindano kuliko tajiri hivyo wanaamua kushikilia mstari huo na kujifariji kuwa tajiri ni hatari. Rafiki, kweli umaskini wa mtu hauanzii mfukoni bali umaskini wa mtu huanzia kichwani yaani akilini. Kiimani tunaalikwa kuwa maskini wa kiroho yaani maana yake tuwe na moyo wa toba uliopondeka na siyo umaskini wa kifedha.
Ndugu, kuna tajiri aliyewahi kutokea hapa duniani kama mfalme Selemani? Hakuna, kwa hiyo, fedha ni jawabu la mambo yote, weka juhudi katika kusaka pesa, acha maneno na weka vitendo umaskini ni mbaya sana unatakiwa kuupa talaka na wala usiuchekee kabisa. Duniani kuna maskini wengi sana ambao umaskini wao huanzia kichwani, umaskini wa kuanzia kichwani ni mbaya kwani mtu ni fikra kama akikataa kubadilika na kuendelea na fikra yake ni ngumu kumbadilisha. Badili fikra yako, badili namna unavyofikri, mtazamo wako uwe chanya katika mambo yote duniani na siyo hasi utaziona fura mbalimbali.

Hatua ya kuchukua leo, fedha huleta jawabu la mambo yote, hivyo ni muhimu kuamua kufunga ndoa na utajiri na kuupa umaskini talaka. Acha kutafuta sababu na fanya kazi ili uweze kupata fedha kwani huwezi kupata kitu chochote bila kujituma.

Kwa kuhitimisha, leo tumealikwa ya kuwa fedha huleta jawabu la mambo yote, tukiachana na hewa tunayoivuta basi pesa ndiyo muhimu kuliko vitu vingine. Ili uweze kuyafikia mafanikio makubwa katika maisha yako, kwanza jitambue wewe ni nani na unataka nini hapa duniani, bila kujua unataka nini ni ngumu kufanikiwa kwa mfano, unaenda dukani huwezi kupatiwa huduma bila kusema unataka nini.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com