Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.

img-20161217-wa0002
Msingi wetu mkuu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambao utatuwezesha kuzifikia ndoto zetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu NJIA PEKEE KWAKO…
Ipo njia ambayo wewe pekee ndiye wa kuipita,
Yaani kwenye maisha yako, yapo mambo ambayo wewe pekee ndiye wa kuyafanya, bila ya kujali wengine wanafanya nini.
Ipo njia maalumu kwako, ambayo hakuna mwingine awezaye kuipita ila wewe.
Njia hii ndiyo yenye mafanikio makubwa sana kwako.

Changamoto ni kwamba, hakuna anayeijua njia hii ila wewe mwenyewe.
Na hakuna mtu mwingine awezaye kuipita ila wewe.
Wengi wanaondoka hapa duniani hawajazipita njia zao, kwa sababu walikuwa wanasubiri waambiwe cha kufanya, na kama hawajaambiwa basi waliangalia wengine wanafanya nini na wao kufanya.
Hakuna awezaye kukuambia njia yako, wala huwezi kuiiga kwa yeyote.
Ni wajibu wako kuotafuta njia hii, kwa kuwa huru kujaribu mambo mengi uwezavyo, kuwa tayari kushindwa na kuwa tayari kujifunza kila siku.

Kama tayari umeshaijua njia, weka juhudi, pambana maana mafanikio ni yako.
Kama bado hujaijua njia basi jukumu lako kuu kwa sasa ni kuijua njia. Kuwa huru katika kufikiri, jaribu mambo mengi, jifunze zaidi na kuwa tayari kukosea na kushindwa.

Utajuaje kama njia uliyopo ni yenyewe?
Zipi njia nyingi, lakini rahisi kabisa ni hii KAMA UNAFANYA KWA SABABU ULIAMBIWA NA WENGINE, AU KAMA UNAFANYA KWA SABABU ULIONA WENGINE WANAFANYA, HIYO SIYO NJIA YA KIPEKEE KWAKO

Itafute njia yako, na maisha yako yatakuwa na mageuzi makubwa sana kwako.

Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Kumbuka leo ni KUTHUBUTU, USHINDI na SHUKRANI.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.