Habari za leo rafiki yangu katika mafanikio?

Ni matumaini yangu kwamba uko vizuri, na unaendelea kupambana ili kuishi yale maisha unayotaka wewe, na siyo yale maisha ya kusukuma siku.

 

Naomba nikiri kwamba mimi siyo mfuatiliaji mzuri wa kazi za sanaa, hasa miziki, maigizo na tamthilia. Hii inatokana na ufinyu wangu wa muda. Lakini kitu kinapokuwa maarufu, kila mtu anakisikia na anakuwa na wazo kwamba kitu fulani ni maarufu.

Moja ya vitu hivyo ni wimbo wa msanii Darasa unaoitwa WACHA MANENO WEKA MUZIKI… sina hakika kama hilo ndiyo jina la wimbo, lakini nina hakika hayo ndiyo maneno yanaoubeba wimbo huu.

Watu wamekuwa wanasema huu unapaswa kuwa wimbo wa taifa, kwa sababu kila mtu anauimba. Nakumbuka siku moja niliwahi kumuuliza mtu kwa nini uwe wimbo wa taifa? Nikahoji zaidi, kipi ambacho ni cha tofauti sana kwenye wimbo huu, kinachoufanya uwe maarufu zaidi ya nyimbo nyingine? Sikuuliza haya kubeza uzuri wa wimbo, bali napenda kujua vitu kwa undani zaidi.

Hakuna aliyeweza kuwa na majibu kamili, lakini watu walikuwa na uhakika juu ya jambo moja, kwamba wanaupenda wimbo ule, na kila wakati wanauimba.

Hivyo nilikaa chini mimi mwenyewe, na kutafakari kipi kinapelekea watu kuupenda wimbo huo kiasi hicho? Na hapa nimekuja na hoja yangu binafsi, ambayo kwa kiasi inaelezea kwa nini watu wanaupenda wimbo huu.

SOMA; Tabia Hizi Nne(4) Ulizonazo Zinakuzuia Wewe Kufikia Mafanikio Makubwa.

Hoja yangu ni kwamba, watu wameambiwa kile ambacho walikuwa wanataka kuambiwa muda mrefu, au mtu amewasaidia kusema kile ambacho walikuwa wanataka kusema. Ukweli ni kwamba, sisi watanzania tena maneno mengi sana, maneno mengi mno lakini matendo sifuri. Kila mtu akiulizwa atoe maoni yale ataongea kwa hamasa sana, ataongea na kuonekana jembe kweli, anajua kweli, lakini muulize amefanya nini, kimyaa. Kila mtu anaongea ongea sana, ni maneo maneno maneno kila mahali, lakini kazi hamna.

Hivyo basi, ACHA MANENO, WEKA MUZIKI,

Sasa mimi leo kwako rafiki yangu, nina neno moja tu, WACHA MANENO WEKA KAZI…
Nimewahi kusema hili na leo naomba nilirudie tena. Wakati naanza kazi hii ya uandishi na kushauri watu, nilikuwa nafurahia sana pale mtu anaponiambia anataka tukutane kwa ajili ya kumshauri zaidi. Nilikuwa tayari kusema ndiyo na karibu sana, nikiamini natoa mchango wangu mkubwa kwa watu na utawanufaisha. Na hivyo nilikuwa nasema ndiyo. Nakumbuka siku moja nimewahi kwenda kumfuata mtu nje ya mji kabisa, akitaka niangalie mazingira yake na nimshauri biashara gani anaweza kufanya, nilifanya hivyo.

Lakini nilipokuja kuwa nawafuatilia wale niliowashauri wamefikia wapi, tisa kati ya kumi hawakuwa wamefanya lolote. Kosa sasa uwaulize kwa nini bado hujaanza? Maneno yanaanza, oh mambo bado hayajakaa vizuri, sijui nilipeleka watoto shule, mara nilipata mgonjwa, msiba, nilisafiri na mengine mengi.
Ni MANENO, Maneno, maneno.

Ndipo nilipoona hilo halikuwa na msaada kwa wengi na zaidi lilikuwa linanipotezea muda, na kuamua kuliacha mara moja. Hivyo kwa sasa sikutani tena na watu kwa ajili ya maneno maneno, tunakutana kwa ajili ya kazi, kuna kitu unafanya tayari na unataka kiende mbele zaidi tunaanzia hapo, lakini maneno maneno unaweza kutafuta wengine wakufanya nao hayo maneno.
Watanzania tumekuwa watu wa maneno maneno mno, na ujio wa hii mitandao ya kijamii, ndiyo imemwaga petroli kwenye moto wa maneno. Sasa hivi kila mtu naye ana maoni kwenye kila jambo linaloendelea. Ni maneno maneno tu, na sasa tunahama kwenye maneno tunakwenda kwenye DRAMA, hii ndiyo hatari zaidi.

Kwa sababu bora maneno unaongea tu, lakini drama unahusika moja kwa moja, na ubaya wa drama huwa haziishi, ikiisha moja inaanza nyingine. Wewe angalia tu, linaanza jambo moja, wooote mnakwenda upande huo, kabla hata halijashika kasi linaibuka jingine kubwa zaidi, wooote wanasahau la kwanza na kuendea lile jipya, yaani ni DRAMA juu ya DRAMA. Zipo drama za kitaifa, kijamii na hata za kifamilia. Kadiri unavyokuwa nazo nyingi ndivyo unavyoshindwa kufanya kazi.

Samahani rafiki, hii ya drama tutakuja kuiongelea kwa undani zaidi siku zijazo, leo wacha tumalizane na MANENO MANENO.

Wapo watu wanaosema kila siku wanataka kuandika, lakini wanabaki na maneno maneno tu, kwamba wataandika, siku zinakatika na hawaandiki. Wengine wameniomba hata ushauri, na kitabu nikawauzia lakini bado hawaandiki. Nawajua wengi mno, huendana wewe ni mmoja wao, nakuambia WACHA MANENO ANZA KUANDIKA.

SOMA; Maneno Mawili (02) Yasiyokuwa Na Msaada Kwenye Maisha Yako.

Wapo watu ambao kila siku wanasema wataanzisha biashara, na ushauri wanaomba na mawazo wanayapata, lakini kila siku hawakosi sababu ya kuahirisha. Maneno yanakuwa juu ya maneno, miaka inakatika, biashara hakuna. Nakuambia WACHA MANENO ANZA BIASHARA.

Kuongea sana imekuwa kama sehemu ya utamaduni wetu, pima hata wanasiasa wetu, pima viongozi wa dini, utaona wale wanaoongea sana ndiyo wanaozoa watu wengi. Kwa sababu wanaopenda kuongea wataenda kwa wale wanaoongea. Ni maneno maneno tu, lakini hakuna kikubwa cha konesha.

Sitaki na mimi niseme maneno mengi hapa, japo angalau nimeandika, na nimekuwa naandika kila siku, kitu ambacho wengi wanasema watafanya lakini hawafanyi. Lakini nataka hapa uondoke na kitu kimoja rafiki yangu, WACHA MANENO WEKA KAZI.

Mwisho wa siku, maneno hayatakuwa na msaada wowote kwako, maneno hayatakuletea mafanikio, maneno hayatakuletea utajiri, bali kazi, NDIYO, kazi, itakupa kile unachotaka kwenye maisha yako.

Ipe kazi kipaumbele, fanya kitu kinachoonekana, kinachoongeza thamani kwa wengine, maneno ni matupu, yanapotea kama moshi, lakini unapofanya kitu, kitagusa mtu na kuleta mabadiliko hata kama ni madogo sana.

Kama ambavyo wewe utafanya mabadiliko madogo kwenye maisha yako leo, utaanza kufanya, kile ambacho umekuwa unataka kufanya siku nyingi lakini huanzi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.