Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?

Karibu tena kwenye makala yetu ya leo ya falsafa mpya ya maisha, ambapo kwa pamoja tunajenga falsafa ya kutuwezesha kuwa na maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa. Najua unajua kwamba maisha yako ni jukumu lako, sahau kabisa kuhusu nani kafanya nini, bali jiulize unafanya nini kuyaboresha zaidi maisha yako. Hakuna wa kufanya hilo zaidi yako wewe mwenyewe.

Kwenye makala yetu ya leo ya falsafa mpya ya maisha, tunakwenda kuangalia eneo muhimu sana kwenye maisha yetu, ambalo ni matatizo na changamoto zetu za maisha ya kila siku. Hivi ni vitu ambavyo vimekuwa vinatuletea msongo wa mawazo, wengine wanakosa usingizi, wengine wanashindwa kabisa kujua hatua gani wachukue.

Yapo matatizo na changamoto kubwa sana ambazo tunapitia kila siku, nyingine zinakatisha tamaa, nyingine zinatufanya tuone hatuwezi tena, hakuna tena namna ya kufika kule tunakotaka. Pamoja na haya yote, bado tunahitaji kusonga mbele, bado tunahitaji kuendelea kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.

Ila swali linakuja, unawezaje kuendelea kuweka juhudi kubwa, unawezaje kuendelea kuwa na hamasa hata pale unapoona kabisa umefanya makosa makubwa au kukutana na changamoto isiyowezekana? Zipo njia mbili za kukuwezesha kuendelea kuwa na hamasa ya kufanya au hata kuanza upya.

Njia ya kwanza ni kwa kutumia maono makubwa uliyonayo kwenye maisha yako. Kutumia ile ndoto ambayo ipo ndani yako, ambayo inakusukuma kuamka asubuhi, kuipitia ndoto hii kila siku. Kama kweli unayo ndoto hii, hamasa utaipata, kwa sababu ni kitu kinachowaka ndani yako, hakitakuacha ukae hata kidogo. Na kama bado huna ndoto hii, kama huna maono hayo makubwa, kazi yako ya kwanza ni kutengeneza ndoto na maono hayo. Kwa sababu maisha ambayo hayana maono ni sawa na ndoto mtu anazozipata usiku, huwa hazikufikishi popote. Usitake kuishi maisha ambayo hayatakufikisha popote.

Njia ya pili ya kuendelea kupata hamasa na kupiga hatua, ni kutumia falsafa ambayo tunakwenda kujifunza leo. Hii ni falsafa moja muhimu ambayo itakufanya uyaone matatizo na changamoto zozote ulizonazo, hata kama ni kubwa kiasi gani, kuwa za kawaida na haziwezi kukuzuia kufika kule unakotaka kufika.

Falsafa hii inaanza kwa kufikiri NANI ATARITHI MATATIZO NA CHANGAMOTO ZAKO?
Kwanza kabisa tunajua kwamba tutakufa, kila anayepumua atakufa, kila anayesoma hapa, ipo siku atakufa, hii siyo habari mpya, hivyo haihitaji kukusononesha. Swala ni kwamba, hapo ulipo una mali, hata kama ni ndoto na pia una matatizo na changamoto zako, ambazo zinakupa hofu kila siku.

Sasa chukulia hivi, ukifa leo nini kitakachoendelea?

Watu wako wa karibu, wanaokupenda sana, watalia, wataomboleza, watakukumbuka ulivyokuwa mchango kwao.

Mazishi yatafanyika, ambapo utazikwa.

Halafu watu wataangalia ulikuwa unamiliki mali gani, na kuangalia watu gani watapewa mali zile waendelee kuzimiliki. Hata kama ni nguo, wapo watu ambao watapewa.

Lakini kuna jambo moja hatujasikia hapo, vipi kuhusu matatizo na changamoto zako? Nani anapewa aendelee nazo, nani atazirithi, nani ataendelea kubeba matatizo na changamoto zako kwa kuwa sasa wewe haupo tena?

Jibu ni hakuna, hakuna yeyote atakayebeba matatizo na changamoto zinazokusumbua leo. Hii ina maana kwamba ukifa tu, na zenyewe zinakufa, hapo hapo, hazina tena nafasi. Zinakusumbua wewe unapokuwa hai, ukifa na zenyewe zinayeyuka. Hakuna watu watakaokuja kugawana changamoto na matatizo yako binafsi.

Sasa hapa tunajifunza nini? Maana hili ndiyo muhimu sana, tunaondoka na nini cha kufanyia kazi kwenye maisha yetu, ili yawe bora, yenye furaha na mafanikio makubwa?

Unachopaswa kuondoka nacho ni hiki, matatizo na changamoto ulizonazo sasa, zitakwisha kabisa ile siku ambayo utakufa, hivyo basi, unaweza kuamua kuachana nazo, au kuzizuia zisikuathiri, kama ambavyo haziwezi kukuathiri tena pale utakapokufa.

Hii ina maana kwamba pale unapokata tamaa au kupata hofu kutokana na changamoto au matatizo uliyonayo, jikumbushe kwamba siku ukifa hakuna atakayebeba changamoto hizo kwa ajili yako, zitayeyuka na maisha ya wengine yataendelea kama kawaida. Hata kama ni kazi nyingi ulizonazo, siku ukifa hatafuatwa ndugu yako kuhakikisha kazi zinaisha, mambo yataenda vizuri tu bila ya hizo kazi zako kuwa zimemalizwa.

Hivyo jipe uhuru wa kuwa na maisha yako, usikubali kumezwa na changamoto na matatizo yako. Jiruhusu kuishi maisha, kwa kuwa haya ndiyo pekee uliyonayo, ukishaondoka hata changamoto hizo hazitakuwa tena na nafasi.

Ukiona bado huwezi kujituliza kwa kuchukulia kwamba siku ukifa changamoto zako nazo zinakufa, basi jichukulie umekufa (najua hili linatisha, lakini kwa wanafalsafa ni jambo la kawaida.) unapokwenda kulala usiku, jichukulie ni sawa na umekufa, hivyo usiruhusu matatizo au changamoto ulizonazo ziendelee kukunyima usingizi. Lala ukiwa na amani ukijua changamoto na matatizo yako yote yameyeyuka. Unapoamka asubuhi, chukulia kama umezaliwa upya, au umeyaanza maisha mapya, hivyo usiruhusu matatizo na changamoto za zamani kuwa mzigo kwako. Hivyo amka ukizichukulia zile changamoto kama ni mpya na anza kuzitatua kwa upya wake.

Maisha ni yako, namna unavyoyaishi ni uchaguzi wako binafsi, hivyo chagua kuyaishi maisha yako kwa namna ambapo utakuwa na amani ndani yako, utaweza kufanya makubwa na kuweza kupata makubwa pia.

Jikumbushe hili kila mara, UKIFA, HAKUNA YEYOTE ATAKAYERITHI MATATIZO NA CHANGAMOTO ZAKO, hivi ni vitu vya kupita na visivyo na maisha marefu, usikubali vivuruge maisha yako.

Tumia falsafa hii kuondokana na changamoto na matatizo yanayokupa hofu na kukukatisha tamaa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.