Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi nyingine nzuri na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa.

Tuendelee kuweka NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA kila siku kwenye naisha yetu ili tuweze kupata matokeo bora zaidi.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu VACUUM au UTUPU.
Asili (nature) haipendi kabisa utupu, huwa inahakikisha pale hali inaporuhusu basi kila kitu kiwe na utele.
Ndiyo maana ukiwa na shamba ahalafu hukulilima, halitabaki tupu, yataota magugu na vichaka.
Hii ni kazi ya asili, kuhakikisha hakuna utupu kwenye eneo lolote la dunia.
Hii pia inakuja kwetu binafsi, kuanzia kazi zetu, muda wetu na hata mawazo yetu.
Unaporuhusu utupu kwenye eneo lolote la maisha yako, unaipa ruhusa asili ijaze eneo hilo. Changamoto ni kwamba itajaza kitu ambacho hakina manufaa kwako, kwa sababu hujajisumbua kujaza kile unachotaka wewe.
Kama kwenye muda wako wa kazim ukawa hujapangilia kipi muhimu kwako, utajikuta yanajitokeza mengi ya kufanya na hayana maana kwako.
Kama utashindwa kupangilia muda wako, utashangaa siku imeisha na huoni umefanya nini.
Kadhalika kama unaruhusu utupu kwenye mawazo yako, utajikuta umejawa na mawazo hasi yasiyo na faida kwako.
Hii ni kazi ya asili kujaza kila ambacho ni kitupu, na inajaza na chochote kinachopatikana haraka.
Hivyo rafiki, kuepuka kujazwa vitu ambavyo siyo muhimu kwako, weka vipaumbele kwenye kazi zako, pangilia vizuri muda wako na muda wote kuwa na mawazo chanya kwenye akili yako.
Kwa namna hii asili itaendelea kukujaza vile ambavyo ni muhimu kwako.
Nakutakia siku njema sana ya leo.
Nenda UKATHUBUTU, USHINDE na uwe na SHUKRANI.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.