Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu hujambo na unaendelea vizuri, leo ni siku nyingine bora na ya kipekee sana kwetu hivyo tunaalikwa kumshukuru Mungu kwa zawadi hii ya uhai aliyetujalia mimi na wewe. Rafiki, tunaalikwa kutumia vizuri zawadi hii aliyotujalia Mungu siku hii ya leo, nenda katumie vizuri siku hii ya leo kwa nidhamu, uadilifu na kujituma, usipoteze muda kwa vitu ambavyo havina athari chanya kwenye maisha yako.

 

Mpendwa rafiki, napenda kukualika tena katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mambo mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Kwa hiyo, karibu sana rafiki tuweze kuambatana pamoja hadi pale tamati ya kipindi chetu cha leo. Leo tutakwenda kujifunza wote kwa pamoja sehemu au maeneo mawili muhimu yaliyosaulika katika uwekezaji.

Huenda mpenzi msomaji, ulivyoona kichwa cha makala ya leo ulikuwa unajiuliza je ni maeneo gani hayo yaliyosahaulika katika uwekezaji? Ukaona ni fursa kubwa kwako ya uwekezaji hivyo ukavutiwa uingie na uisome ili upate kujua ni uwekezaji gani huo. Rafiki, katika maisha ya binadamu huwa anakuwa ana maeneo matatu ya uwekezaji katika maisha yake ambayo ni ya kiakili, kimwili na kiroho. Sasa basi maeneo mawili yaliyosahaulika sana katika uwekezaji basi ni uwekezaji wa kiroho na kiakili.

SOMA; Mambo Matatu Ya Kuzingatia Kabla Ya Kufanya Uwekezaji Wa Majengo Ili Uepuke “Bomoabomoa”

Mpendwa msomaji, watu wamekuwa wabinafsi katika maisha yao kwa kuweza kuwekeza kwa wingi katika eneo moja ambalo ni eneo la mwili la kusahau maeneo mengine mawili muhimu sana kwa ukuaji wa binadamu. Ili uweze kukua kama binadamu unatakiwa kukua katika maeneo makuu matatu ambayo ni maeneo ya kimwili, kiroho na kiakili. Watu wengi wanapenda kuwekeza katika mwili kwa sababu wamezaliwa na kukuta watu wakiishi katika mfumo huo wa kuwekeza zaidi kwenye eneo la mwili.

Mpendwa rafiki, huwezi kufanikiwa kama maisha yako umejitoa katika uwekezaji wa kimwili tu, kuna watu wengine hawafikiri kitu kingine zaidi ya kuwekeza katika mwili kama kula, kulala sana, kujinunulia nguo, na vitu vyote vinavyowekezwa katika mwili. Lakini tukumbuke ya kuwa mwili haufai kitu, mwili hauna shukrani kama unaona uwekezaji wa mwili ni muhimu sana siku yako mwisho kuvuta pumzi hapa duniani uko kwenye kitanda ndiyo utakuja kuona kuwa uwekezaji wa kwenye mwili hauna maana.

Kwanini tunashauriwa tuwekeze sehemu katika akili? Kwanza akili ndiyo iliyokubeba wewe na kuonekana kama binadamu. Akili yako inahitaji chakula kama vile mwili wako unavyohitaji chakula, na chakula cha ubongo ni maarifa je mara yako ya mwisho kulisha ubongo wako ni lini? 

Binadamu unapimwa ukuaji wako kiakili na wala siyo kuwa na mwili mkubwa ndiyo umekuwa ndio maana busara na hekima ya mtu haikui katika mwili bali iko akili lini. Eneo hili la akili watu wamelisahau kabisa katika uwekezaji, watu wanatumia gharama kubwa kuwekeza katika mwili kuliko katika akili. Kwa mfano, ikitangazwa ofa ya nguo, na kitabu watu wengi wataenda kwenye nguo hata kama bei ya nguo na kitabu ni moja watu wamekuwa wagumu kuhudumia akili zao wakati akili ndiyo kiwakilishi cha kumtambulisha yeye kama binadamu.

Uwekezaji wa akili ni muhimu sana katika maisha yetu kwani hakuna uwekezaji mzuri na muhimu kama uwekezaji wa kwenye akili kwani unapowekeza katika akili ndiyo utapata maarifa ya kujenga na kuijaza duniani, hii ndiyo aina ya uwekezaji unaoleta mapinduzi unayoendelea kuyaona sasa unafikiri kama watu wangeamua kuwekeza tu kwenye mwili leo hii tungekuwa na teknolojia tuliyokuwa nayo leo?

SOMA; Hatua Muhimu Za Kukusaidia Uanze Uwekezaji Wa Ardhi Na Majengo Hata Kama Una Kipato Kidogo

Aidha, tunashauriwa tuwekeze katika eneo la kiroho, binadamu wa sasa wamekumbatia dunia na kusahau maisha yao ya kiroho, mambo ya kidunia yamegeuka ndiyo miungu yao na kumsahau hata Mungu aliyewaumba. Watoto wanakosa malezi bora ya falsafa ya kidini ambayo ni muhimu yanamfundisha mtoto kukua katika maadili mema. Leo hii eneo la ukuaji wa kiroho limepigwa teke na kukumbatia dunia. Eneo hili la kiroho ni muhimu sana katika maisha ya binadamu kama vile mwili wako unavyohitaji chakula nayo roho yako inahitaji chakula cha kiroho ili iweze kushiba, tunaliacha wazi eneo hili la kiroho hivyo kuruhusu kila aina ya uchafu kuingia katika nafsi zetu. Matatizo mengi ya nafsi yanayoendelea kuwatafuna watu wengi leo hii moja wapo ni kukosa kuwa na uwekezaji mzuri wa kiroho.

Ndugu msomaji, kila mtu anajua fika siku moja atakufa hivyo basi, pale unapokuwa kitandani na mwili wako haujiwezi kufanya chochote japo uliwekeza sana kwenye mwili na unakaribia kuaga dunia ukifikiria maisha yako yote ya hapa duniani utakuja kugundua kuwa uwekaji muhimu sana kwenye maisha ya binadamu ni uwekezaji wa kiroho kwani ndiyo unakuunganisha na kule unapokwenda baada ya kuiaga dunia.

Hatua ya kuchukua leo, uwekezaji wa mwili, akili na roho ndiyo mafiga matatu kwenye maisha ya binadamu, kama ukitoa figa moja kumbuka huwezi ukapika jikoni hivyo ni vitu vinavyoshabiana yaani vinakwenda sawa wakati wote kama vile mizani. Jaribu hata kuuadhibu mwili wako pale unapopata matamanio ya kitu Fulani kwani akili yako ndiyo imetawala mwili wako hivyo usikubali kuwekeza zaidi katika mwili kwani ni hasara.

Kwa hiyo, ili binadamu akue kikamilifu anatakiwa kuwekeza sehemu zote tatu muhimu nazo ni kiakili, kiroho na kimwili. Watu walioishi maisha ya zamani kama ya kuja kwa Yesu Kristo hawakuwekeza maisha yao katika mwili zaidi bali waliwekeza zaidi katika akili na kiroho ndiyo maana leo hii tunawakumbuka watu wa zamani kupitia mambo makubwa walioyoweza kuyafanya hapa duniani kama vile wanafalsafa na watakatifu.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com