Hongera rafiki kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa zaidi.

Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA tunao uhakika wa kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KANUNI YA KUPATA PESA KWENYE DUNIA YA SASA.
Karibu kila siku kunaibuka kitu kipya, ambacho kinaonekana ni fursa ya kupata pesa. Vitu vipya ambavyo vinaonekana ni njia ya mkato ya kukamata pesa haraka. Na wengi wamekuwa wanakimbilia njia hizo mpya.
Pamoja na hayo, ukweli unabaki kuwa, kanuni ya kupata pesa haijabadilika wala haitakuja kubadilika. Hivyo ili kuepuka kuyumbishwa, kupogezewa muda na hata kutapeliwa, ijue kanuni ya kutengeneza pesa na iangalie kwenye kila fursa unayokutana nayo.
Na kanuni ya kutengeneza pesa ni hii;
Tafuta tatizo au hitaji la watu ambalo halijatimizwa, kisha angalia jinsi gani unaweza kulitatua kwa haraka ha kwa uhakika, na watu watakuwa tayari kukulipa fedha
Ni hivyo rafiki, hakuna ujanja ujanja zaidi ya hapo, hakuna kutoa watu, kuingiza au kufanya nini. Ni kitatua tatizo, kutoa bidhaa au huduma na kuongeza thamani. Kama hilo halipo, kimbia haraka, haupo kwenye njia sahihi ya kutengeneza fedha.
Yeyote anayekuambia kitu fulani ni fursa, angalia namna gani unawapa watu kile ambacho hawana, namna gani unaongeza thamani kwao na namna gani wao wenyewe wanalipia kile unachofanya au kutoa.
Usikubali kupogezewa muda au kutapeliwa na fursa za uongo.
Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.