Kwenye ulimwengu wa sasa ni muhimu sana kuwa jasiri ili kuweza kufikia malengo uliyojiwekea. Kukosa ujasiri ni sababu kuu ya watu wengi kushindwa kutimiza ndoto zao.
Ujasiri ni muhimu sana kufikia mafanikio yako kwa sababu unakufanya uweze kutumia ujuzi, uwezo na vipaji vyako katika mazingira yoyote. Ujasiri ndio unawasaidia watu wengi ambao hawana uzoefu ila wanaweza kuanza mwanzo na mwisho wa siku wakawa wazoefu waliobobea.
Ujasiri ni kiashiria kwamba unajua unachokifanya na una imani kwamba utafikia malengo yako. Ujasiri ndio unakusaidia kutoyumbishwa na walimwengu.
Njia tano za kuongeza ujasiri na kufikia mafanikio.
1. Kaa na watu ambao wana mtizamo chanya, wanaojua ni nini wanataka kwenye maisha na wanafurahia maisha yao. Watu hawa ni jasiri na wako tayari kubadili sehemu ya maisha yao ambayo hawaifurahii. Ujasiri unaambukizwa, hivyo ukizungukwa na watu jasiri hata wewe utakuwa jasiri.
2. Kila siku fanya kitu ambacho kinakufurahisha na kukufanya utabasamu. Kufurahia maisha kunaongeza ujasiri kwa sababu utaendelea kufanya yale yanayokufurahisha na mwisho wake ni kuyafikia mafanikio
3. Zingatia malengo na mipango yako. Tumia muda wako mwingi kuangalia kule unakokwenda na kuna jinsi maisha yako atakavyozidi kuwa mazuri kwa wewe kufikia malengo yako, hii itakupa ujasiri mkubwa na kuweza kuyafikia malengo haraka.
4. Usikate tamaa unapshindwa. Sio mara zote mambo yanatokea kama ulivyopanga, hivyo usikate tamaa na kujiona umeshindwa. Tofauti kati ya waliofanikiwa na walishindwa ni jinsi walivyopokea na kuvishinda vikwazo.
5. Tumia muda wako vizuri inapokuja kwenye kutimiza malengo yako. Hakikisha unafanya kile ulichopanga kwa muda uliopanga, kufanikiwa kwenye mambo madogo madogo kama kuweza kukamilisha ratiba kunakujengea ujasiri.
Majasiri ndio wanaofanikiwa kwenye jambo lolote wanalofanya, waoga hushindwa kabla hata ya kushindwa. Ujasiri ndio unamfanya mtu kuweza ku ‘take risk’ na ‘risk takers’ ndio wanaleta mabadiliko duniani. Usiwe mwoga tena jenga ujasiri wako na uyafurahie maisha yako.