Ni tabia ya binadamu kuwa na hamu na kuthamini kitu sana kabla ya kukipata, lakini akishakipata thamani yake inashuka.
Ukichukulia watu wanaoshinda bahati nasibu, siku za kwanza wanakuwa na furaha lakini haidumu, wanarudi kwenye maisha yao ya kawaida.
Pia mtu anaweza kusoma miaka mingi, akafaulu, akaomba kazi akiwa na matumaini makubwa ya kufurahia kazi ile, anaipata na baada ya muda anaanza kuichoka kazi ile.
Au mtu anachumbiana na mwenzake, wanapendana sana, wanakuwa na ndoto za kuishi pamoja, maisha ya furaha. Wanaoana kweli lakini baada ya muda wanachokana na kuanza kusumbuana.

Ukweli ni kwamba sisi binadamu huwa tunazoea vitu ambavyo tayari tunavyo, kwa sababu tunaviona na tunajua vitaendelea kuwepo.
Tatizo linatokea pale tunapopoteza vitu hivyo, fedha ulizozoea huzioni tena, kazi uliyozoea inaisha, au ndoa uliyozoea inavunjika, au hata mtu uliyekuwa umezoeana naye anaondoka.

Hapa ndipo wengi wanapoanza kuhuzunika na kusema KAMA NINGE….

Wastoa wanayo njia nzuri sana ya kuondokana na hili, njia ya kuhakikisha kila kitu tunakipa uzito wake na hatujutii pale tunapokikosa.
Njia hii ni KUTENGENEZA TASWIRA HASI au kwa kiingereza NEGATIVE VISUALIZATION.
Kwa mbinu hii, unatengeneza taswira kwamba kile ambacho umekizoea, ghalfa kimeondoshwa kwenye maisha yako, huwezi kukiona tena. Kama ni gari imeibiwa, kama ni fedha zimepotea, kama ni kazi umefukuzwa na kama ni mtu basi amekufa.

Kwa taswira hii unaona kabisa kile kitu kimeondoshwa na huwezi kukipata tena. Hapa ndipo utakapoanza kuvithamini vitu. Hapa ndipo utakapoona kwamba kile ambacho ulikuwa unachukulia kwa kawaida tu, ni cha thamani sana. Kwa kujua hilo utavipa vitu thamani yake.

Kujenga taswira hasi siyo sawa na kuwa na mtizamo hasi. Mtizamo hasi maana yake unaona kila kitu hakiwezekani. Lakini taswira hasi unaona uwezekano wa kukosa kile ulichonacho sasa. Na hii inaiufanya ukithamini zaidi.

Hivyo, popote pale ulipo, na chochote unachokipenda na kukithamini, jua kuna siku kitaondoka, hutakuwa nacho milele. Hivyo tumia vizuri muda ulionao sasa, ili kuweza kufaidi vizuri kila ulichonacho sasa.
Kujikumbusha kwamba unaweza kukipoteza, kunakuwezesha kukithamini zaidi.