Makirita Amani:

Habari rafiki?

Karibu kwenye darasa letu la jumapili.

Jumapili ya leo tunakwenda kujadili kuhusu uwekezaji wa hisa, na fursa ya hisa za vodacom.

Nitafungua kwa ufupi kuhusu uwekezaji wa hisa, na baadaye nitafungua mjadala kwetu sote, kwa mwenye cha kuongeza, maswali na hata majibu.

Uwekezaji kwenye hisa ni fursa ya mtu kuwa sehemu ya wamiliki wa biashara au kampuno husika.
Kwa mfano kama unataka kuanzisha biashara ya mtaji wa laki moja, na wewe una elfu 10 tu, unaweza kuwatafuta watu 9 kila mtu akachangia elfu 10 na jumla mkapata laki moja.
Hivyo kama biashara itapata faida, kila aliyechangia atapata sehemu ya faida hiyo.
Na kama itapata hasara, basi inakuwa hasara kwa kila mtu.
Uwekezaji wa hisa ndiyo uko hivyo, ila hapa ni kwa kiwango kikubwa na udhibiti mkubwa wa kisheria.
Unaponunua hisa za kampuni, maana yake unakuwa umechangia mtaji wa kampuni na hivyo kuwa mmoja wa wamiliki.
Lakini wewe huhusiki kwa namna yoyote ile kwenye uendeshaji wa kampuni.
Kampuni itaendeshwa kulingana na taratibu zake.
Faida inapopatikana, basi unapewa gawio kama mwanahisa, kulingana na hisa ulizonazo.

Faida za kuwekeza kwenye hisa.
Zipo faida nyingi sana za kuwekeza kwenye hisa, hizi hapa ni chache.
1. Kupata faida kutokana na fedha ulizowekeza. Hapa fedha yako inafanya kazi huku wewe ukiwa unaendelea na mambo yako mengine.
Na hapa ndipo dhana halisi ya utajiri ilipo, PALE FEDHA INAKUFANYIA WEWE KAZI badala ya wewe kuifanyia kazi fedha ambao ni unasikini.
2. Kupata ongezeko la thamani ya fedha uliyowekeza. Licha ya gawio la faida, hisa huweza kuongezeka thamani, kulingana na uimara wa uchumi na soko. Kwa mfano unaweza kununua hisa ikiwa shilingi 500, baada ya muda thamani yake ikawa sh 1000, hapo ukiuza unauza kwa bei ya wakati huom siyo ile uliyonunulia.
3. Ni sehemu ya kuweka fedha ambayo huwezi kuitoa haraka.
Watu wengi wamekuwa wakilalamika kushindwa kuzituliza fedha, wakiweka benki hawawezi kujizuia kwenda kuzitoa. Unapowekeza kwenye hisa siyo rahisi kupata fedha zako kama unavyoenda kutoa kwenye atm, inabidi ujaze fomu kuuza hisa na usubiri zinunuliwe.

Hasara za kuwekeza kwenye hisa.
Hisa siyo kitu chenye faida tu wakati wote, zipo hasara na hatari pia. Zifuatazo ni baadhi kati ya nyingi.
1. Kampuni ikipata hasara na wewe unapata hasara. Kampuni ikifilisika na wewe unapoteza kabisa kile ulichowekeza.
2. Mabadiliko ya kiuchumi kama mfumuko wa bei vinaweza kuathiri thamani ya hisa, badala ya kupanda bei zinashuka bei.
3. Mabadiliko ya kisiasa yanaathiri pia soko la hisa.
4. Huna udhibiti wa moja kwa moja wa fedha zako, unanunua hisa lakini wanaoongoza kampuni ni wengine, hivyo wakifanya makosa yatakugharimu na huna namna ya kuokoa hilo, hata kama una ujanja kiasi gani.

Baada ya utangulizi huo nigusie hisa za vodacom.

Vodacom Tanzania imeweka sokoni hisa 560 000 100 kwa bei ya shilingi 850 kwa kila hisa.
Kwa sasa hisa hizi zinauzwa kwenye soko la awali mpaka tarehe 19/04/2017, baada ya hapo hisa zitaandikishwa kwenye soko la hisa la dar es salaam (DSE)
Kila mtu anayetaka anaweza kununua hisa hizi,
Kiwango cha chini cha kununua ni hisa 100.
Unaweza kununua hisa kupitia madalali wa soko la hisa, bank mbalimbali zilizoteuliwa kama nbc, wakala wa max malipo na hata njia ya simu.
Hii ni fursa ya uwekezaji iliyo wazi kwa kila mtanzania.

Uimara au faida za hisa za vodacom;
1. Vodacom ndiyo mtandao wenye watumiaji wengi tanzania, hivyo kuwa na soko kubwa la huduma zake.
2. Huduma za data zinakua kwa kasi kutokana na ongezeko la watu wanaotumia mtandao wa intaneti.
3. Huduma ya M Pesa imeendelea kuwa tegemeo kwa watanzania wengi ambao hawawezi kufikia benki na hata kwenye miamala ya kibiashara.
4. Kampuni imeonesha ukuaji wa kuridhisha tangu kuanzishwa kwake hapa nchini mwaka 1999 mpaka sasa.
5. Udhibiti wa kisheria ulipo chini ya mamlaka ya masoko ya mitaji na soko la hisa la dar es salaam.

Hatari au hasara inayoweza kutokana na hisa za Vodacom.
Zipo hatari zinazoweza kusababisha hasara kwa wale watakaowekeza kwenye hisa za vodacom, hizi ni baadhi kati ya nyingi;
1. Ushindani mkali wa kibiashara kwenye sekta ya mawasiliano. Ipo mitandao yenye nguvu na mingine inakua kwa kasi, kama tigo na halotel.
2. Mazingira magumu ya kibiashara hapa nchini. Vodacom ina baadhi ya kesi za kibiashara zinazotokana na sheria mbalimbali za kibiashara nchini, kama sheria ngumu ya kodi.
3. Miundombinu isiyo ya uhakika, inayoweza kupelekea gharama za uendeshaji kuwa kubwa na hivyo faida kuwa kidogo. Mfano kukosekana kwa umeme wa uhakika.
4. Kesi mbalimbali za kibiashara zinazoweza kutokana na shughuli za kampuni.
5. Mabadiliko ya sera na sheria za nchi yanayoweza kubadili uendeshaji wa makampuni na huduma mbalimbali.
6. Kupata hasara au kufa kwa kampuni, kwa sababu zozote za kibiashara.

Hayo ndiyo machache ya kufungua mjadala wa leo.
Karibuni tujadiliane juu ya uwekezaji na fursa hii ya hisa za vodacom.
Michango zaidi na maswali pia yanakaribishwa.
Meshack Maganga: Asante sana kocha…Iwapo kampuni Imekufa zile hisa za wawekezaji zinaenda wapi na wanapataje Faida yao ?
Mulokozi Silyvester: Kwahiyo kocha kampuni inapotoa hizo hisa inamaanakuwa kampuni hiyo inakuwa imeyumba kimtaji?
Jeremiah Wandili: Ahsante Coach nimefuatilia mjadala na pia kusoma hali halisi ya soko kwa sasa…. na kwa jinsi ulivyoeleza umebalance +- kwa uhalisia wake. Faida na hasara katika uwekezaji upo. Uzuri wa Hisa unatoa nafasi kwa wanahisa kuendelea kushauri na kutoa michango yao ya mawazo ili kuhakikisha biashara inahimalika. Ninachoweza sema kuna haja ya kuwekeza katika hili soko na hasa hisa za Vodacom ambazo kwa mara ya kwanza ndio kampuni ya kwanza kuanzalisting sokoni. Wakati wengine sheria ikiwataka wajiandae kulist Voda ndio inakuwa ya kwanza sokoni. Ninainami hii ni fursa kubwa si ya kuikosa
Makirita Amani: Kampuni ikifa, maana yake imefilisiwa, labda kutokana na kushindwa kulipa madeni. Hivyo mali zote za kampuni zinapigwa mnada kufidia deni, na hisa zinakuwa zimepotelea huko, kwenye kulipa hayo madeni.
Makirita Amani: Siyo lazima iwe imeyumba kimtaji,
Wakati mwingine inataka kuongeza mtaji, ili kukua zaidi.
Na kwa hili la vodacom na mitandao mingine pia inakuja, ni matakwa ya kisheria. Ambapo serikali iliamua makampuni haya ya simu yaorodheshwe kwenye soko la hisa ili wananchi wanufaike na faida kubwa yanayotengeneza.
Coach swali langu la pili, kwa mfano mie nimfanyabiashara wa kawaida na bado sijasajili kampuni. lakini nataka kukuza mtaji wangu naweza kuanzisha hii system ya hisa ili nikuze mtaji wangu kwa haraka na ili niepuke mkopo wa riba bank
Makirita Amani: Unaposajili kampuni, kuna aina mbili za makampuni.
Ya kwanza ni kampuni binafsi, hii inahitaji kuanzia watu wawili mpaka watu 50. Watu ambao mnajuana, na mnakubaliana mataji pamoja na uendeshaji wa biashara utakuwaje, hivyo mnaandaa articles na memorandum.

Aina ya pili ni kampuni ya umma, hii ndiyo inauza hisa kwenye soko la hisa, na kila mtu anaweza kuwa na hisa kwenye kampuni hii.
Huwezi tu kuandikisha kampuni yako au kuuza tu hisa kama unavyotaka, ili kampuni iwe ya umma, kuna viwango vya mitaji na hata uendeshaji, siyo kitu rahisi kwa yeyote kufanya. Lazima kampuni iwe kubwa na inayojiendesha kwa hali ya kuridhisha.
Lazima hesabu zikaguliwe, lazima taarifa zitolewe kwa umma juu ya uendeshaji wa kampuni.
Hillary Thomas: Na nikiiacha hizo his a mpaka zipande bei, ndio nichukue inawezekana?
Makirita Amani: Hapo ndipo penye paradox, na ndipo wawekezaji wanaponufaika.
Kwa hisia za kawaida za binadamu, pale hisa zinaposhuka bei, watu hukimbilia kuuza, ili wasipate hasara, sasa hii hupelekea bei kushuka zaidi, maana kadiri wengi wanavyouza ndivyo thamani inavyoshuka.

Na inapotokea hisa zinapanda bei, wengi zaidi hukimbilia kununua, zinakuwa adimu na hivyo bei kuzidi kupanda zaidi.

Hivyo wawekezaji wenye mafanikio huenda kinyume na watu, wakati kila mtu anauza wao wananunua, na pale kila mtu anaponunua wao wanauza. Hii ndiyo sheria anayotumia warren buffet, mwekezaji bilionea.

Hivyo wakati sahihi wa kununua, hi pale bei inapokuwa chini, maana mara nyingi bei huja kupanda.
Makirita Amani: Tumefika mwisho wa darasa letu la jumapili ya leo.
Naamini kipo tulichojifunza.
Tukitumie kufanya maamuzi sahihi.