Hongera rafiki kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa.

img-20161217-wa0002
Ni kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana na kuweza kufikia ndoto zetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UNA NINI HAPO ULIPO SASA?
Watu wengi wanapofikiria mafanikio, au kufikia ndogo zao, basi huanza kwa kufikiria mambo makubwa sana, mambo ambayo hawana na hivyo kuishia kusema nikipata nitafanya.
Wanaahirisha kuchukua hatua sasa kwa sababu wamejishawishi hawana kile wanachotaka ili kupiga hatua.

Lakini huo siyo ukweli, siyo kweli kwamba ili mtu atoke pale alipo anahitaji makubwa ya nje. Ukweli ni kwamba kila mtu anaweza kutoka pale alipo sasa, kwa kuanzia pale alipo, kwa kile alichonacho pale alipo.
Ninachosema ni kwamba, hapo ulipo sasa, unavyo vitu vya kutosha kukufikisha kule unakotaka kufika, huhitaji kusubiri vitu vya nje.

Biashara uliyonayo, hata kama ni ndogo, ndiyo mlango wako wa kuelekea kwenye biashara kubwa.
Kazi uliyonayo, hata kama kipato ni kidogo na huipendi, ndiyo mlango wako wa kuweza kufika kule unakotaja kufika.

Changamoto ni kwamba, kuanzia hapo ulipo unahitaji kutumia nguvu kubwa, kuumia na uvumilivu wa hali ya juu. Kitu ambacho wengi hawakiwezi na hivyo kusingizia kuna kitu wamekosa.
Usiwe mmoja wa hao, anzia hapo ulipo sasa, anza na kile ulichonacho.

Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.