Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Ni siku nyingine nzuri sana kwetu ambapo tumepata nafasi ya kipekee kwenda kuweka juhudi kubwa ili kupata matokeo makubwa.
Siku hii ya leo twende tukaweke NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ili tuweze kupata matokeo bora sana.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUULIZA NI UJANJA….
Waswahili wanasema, KUULIZA SI UJINGA, lakini kitu ambacho, SI, kinaweza pia kuwa. Kwamba kujua kuuliza si ujinga, kunaweza pia kuwa ujinga, hivyo siyo msingi mzuri wa kuanzia.
Hivyo msingi mzuri wa kuanzia ni KUULIZA NI UJANJA,
Na nikuambie tu hakuna ujanja kama huu duniani, ni ujanja ambao utakusaidia sana.
Iko hivi, chochote unachokazana kufanya sasa, wapo ambao tayari walishafanya na wakafanikiwa vizuri sana.
Changamoto na matatizo yoyote unayopitia sasa, wapo watu walishayapitia na wakaweza kuyavuka vizuri.
Lakini watu wengi hawapendi kuuliza, bali wanapenda kupambana wenyewe, wafikie au kutatua kila kitu wao wenyewe.
Sasa hii inakupotezea muda, kwa kufanya makosa ambayo wengine tayari walishayafanya, hivyo wewe ungeweza kuyaepuka kama ungeuliza.
Hakuna medali yoyote utakayopewa kwa sababu ulifanya bila ya kuuliza, badala yake tu utachelewa kupata kile unachotaka.
Swali ni je, umuulize nani?
1. Muulize mtu yeyote mwenye uelewa, ujuzi au uzoefu kwenye kile unachotaka kujua zaidi.
2. Uliza vitabu kwa kutafuta na kusoma vitabu vinavyoendana na kile unachofanya.
3. Uliza mtandao, GOOGLE inajua kila kitu kinapatikana wapi, hivyo kuandika unachotaka kujua kwenye google na kutafuta, google inakupeleka eneo husika na itaweza kupata majibu yako. (Ukitafuta kwa lugha ya kiingereza unapata majibu mengi zaidi.)
Hivyo rafiki, huna sababu yoyote ya kutouliza, hata kama uko peke yako.
Maarifa yapo mengi, ni wewe uchague kuyatumia.
Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.