Hongera kwa asubuhi hii nzuri sana ya leo rafiki yangu.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana leo.

Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA tunaweza kufanya makubwa sana leo na siku zote za maisha yetu.
Asubuhi ya leo tunatafakari kuhusu GHARAMA NI ILE ILE…
Kuwa bora au kuwa hovyo, kunahitaji kulipa gharama,
Kufanikiwa au kushindwa, ni lazima mtu ulipe gharama.
Cha kushangaza sasa, gharama unayolipa ni ile ile.
Yaani gharama unayolipa ili kushinda, ni sawa kabisa na gharama unayolipa ili kushindwa.
Ukiwaangalia waliofanikiwa na wasiofanikiwa wote wapo bize, wote wana mambo ya kufanya, lakini matokeo ni tofauti.
Wakati wa kulipa gharama pia unatofautiana, ila hakuna anayekwepa kuilipa.
Wanaofanikiwa wanachagua kulipa gharama mapema na wanaishi maisha ya mafanikio.
Wanaoshindwa, wanakwepa kulipa gharama zao mapema, wanaona maisha ni mazuri mwanzoni wakati hawalipi gharama na baadaye wanakuja kulipa gharama kubwa.
Tuchukue mfano wa watu wawili ambao wana kipato kinachofanana, na wote wameanzia chini kabisa.
Mtu wa kwanza akawa anajinyima kwenye kioato chake, sehemu kubwa ya kipato hicho anawekeza maeneo mengine. Mwanzoni anaonekana maisha yake ni magumu mno na hayana maana.
Mtu wa pili yeye anaishi kulingana na kipato chake, akipata anatumia chote, anaonekana kuwa na maisha mazuri, anacho kila ambacho wengine wanacho. Wakati mwingine kama hana fedha ya kununua anachotaka, anakopa.
Miaka 30 inapita, na watu hawa hawana tena nguvu ya kufanya kazi kama walivyoanza.
Unafikiri nani atalipa gharama kubwa wakati huu?
Unadhani nani maisha yatampiga sana?
Majibu unayo.
Ninachotaka utafakari rafiki ni hiki, huwezi kukwepa gharama,
Kufanikiwa kuna gharama utalipa, na hata kushindwa kuna gharama utalipa,
Sasa kwa nini usichague kulipa gharama ya kufanikiwa?
Chagua sasa, na anza kulipa gharama hiyo leo.
Weka juhudi zaidi, ongeza muda wa kazi, punguza matumizi yasiyo muhimu, wekeza zaidi, epuka madeni ambayo hayazalishi.
Lipa gharama sasa, la sivyo utakuja kulipa baadaye, tena utalipa kwa riba kwa sababu hutakuwa katika hali nzuri.
Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.
🙏🏽 kwa tafakari ya leo