Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Ni imani yangu kuwa umeianza siku yako kwa furaha na hamasa kubwa ya kwenda kufanya mazuri siku hii ya leo, kwani leo ni siku nyingine mpya na ya kipekee kwetu , wote leo ndiyo mara yetu ya kwanza kuiona siku na tarehe kama ya leo hivyo ni muhimu sana kuitumia vizuri siku hii ya leo na kuacha alama duniani.

 

Ndugu msomaji, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mambo muhimu nitakayokwenda kukushirikisha siku hii ya leo. 

Kwa hiyo, napenda kukualika ili tusafiri pamoja hadi pale tamati ya kipindi chetu cha leo. Katika kipindi chetu cha leo tutakwenda kujifunza wote kwa pamoja mada yenye kichwa cha habari inayosema jinsi ya kumgundua mtoto mwenye uwezo mkubwa darasani, karibu sana tujifunze.

Sisi binadamu wote tumetofautiana uwezo wetu wa akili, kuna kitu kinaitwa IQ yaani intelligence quotient kwa hiyo, kila mtu yuko katika kiwango Fulani cha IQ yake ambavyo viwango hivyo kuna vya juu kabisa na kile cha chini kabisa ambacho ndiyo cha mwisho kitaaluma tunakiita tabula rasa.

Rafiki, naomba turudi katika shabaha ya kipindi chetu cha leo, natumaini umeshawahi kusikia watu wakisema watoto wenye akili sana yaani ‘’genius’’ au wale watoto wenye uwezo mkubwa au wenye vipaji maalumu yaani gifted. Lazima tukubali kuwa kuna watu au watoto wenye uwezo ambao siyo wa kawaida ukilinganisha na wenzao. Sasa mpendwa rafiki, karibu nikushirikishe njia ya kumgundua mtoto wenye uwezo mkubwa darasani, hata kama wewe siyo mwalimu lakini itakusaidia katika malezi ya mtoto wako kumgundua uwezo wake ukoje.

Watoto hawa wenye uwezo mkubwa darasani wanakuwa na dalili au tabia zifuatazo ambazo wewe kama mwalimu, mzazi au mlezi unapaswa kulitambua hilo.

i. Anakuwa ana uwezo wa misamiati mingi ukilinganisha na umri wake, mtoto huyu darasani anakuwa ana misamiati mingi sana ukilinganisha na wenzake na hii yote inasababishwa na uwezo wake mkubwa wa kupenda kujifunza na kujua mambo kwa undani zaidi. Unaweza ukakutana na mtoto anavyoongea mpaka ukashangaa mwenyewe huyu mtoto mbona anaongea mambo makubwa ukilinganisha na umri wake. Watoto hawa huwa wanapenda sana kujifunza ndiyo maana huchangia kuwa na misamiati mingi ukilinganisha na rika lake.

SOMA; Mambo Matano(5) Muhimu Ya Kuzingatia Kwenye Malezi Ya Watoto Ili Kuwaandaa Kufikia Mafanikio.

ii. Anakuwa anakwenda hatua ya ziada ukilinganisha na mwenzake, kama mwalimu yuko mada ya kwanza basi yeye ameshafika hata mada ya tano kwa kujifunza mwenye tu, anakuwa ana tabia ya kuchimba vitu kwa undani na kuhoji mambo vizuri ili apate. Kama ni kuuliza maswali basi anauliza maswali makini ili yaweze kumsaidia kufika pale anapopataka. Mtoto kama huyu yeye hawezi kukaa chini na kulalamika mbona mwalimu hayupo ila una mkuta ana vitabu vya kusoma vyake binafsi kwa ajili ya kujifunza zaidi.

iii. Anakuwa na vitabu vingi vya kujisomea, watoto hawa wenye uwezo mkubwa ni watoto wanaopenda kusoma mambo kwa undani hata kama mwalimu amemfundisha kitu Fulani yeye anapenda kwenda hatua ya ziada kujifunza zaidi. Huwa hawaridhiki na kile anachompa mwalimu kwa hiyo lazima azame kwenye vitabu kwa kutafuta maarifa zaidi. Hii ndiyo inasababisha anakuwa na uwezo wa misamiati mingi na mikubwa ukilinganisha na wenzake.

iv. Anakuwa anapenda kudadisi mambo sana, kama ni darasani basi anapenda kuuliza sana maswali yenye tija ili aweze kujua zaidi. Wanadadisi mambo sana mpaka inawapeleka kusoma sana ili apate kudadisi kile anachokitaka ni kipi. Siyo watu wa kujibu ndiyo au hapana hawa ni watu kwa nini na tabia yao hii inadhihirisha ni mtu wa tofauti ukilinganisha na wengine.

v. Anakuwa anauelewa mpana wa mambo, unakuta mtoto anajua mambo mpaka una shanga amejifunza wapi. Anapangilia mada na kuwasilisha kwa kujiamini kama ukimpa nafasi ya kuelezea kitu Fulani atakuelezea vizuri sana na kukupa mifano hai itakayokufanya ushawishike na kile unachokiongea.

vi. Anakuwa na nidhamu sana, huwezi kukuta mtoto mwenye uwezo mkubwa anakuwa msumbufu, kama ni kazi za shule anafanya kwa wakati, huwezi kumkuta kwenye makosa ya kijinga kijinga hovyo. Wanakuwa ni watoto makini sana yaani wana kuwa na upekee wao ukilinganisha na wengine, siyo rahisi ukamkuta anapoteza muda kwa mambo yasiyokuwa na msingi kwake.

vii. Anafanya mambo kikubwa, kama umeshawahi kusikia watu wanasema mtoto yule ana akili za kikubwa, anafanya mambo makubwa kweli. Huwa napenda sana kuwadadisi watoto wakiwa wanacheza siku moja niliwaona watoto wakiwa wanacheza sasa mtu mmoja akapita akamwita mmoja ya watoto hao wewe mtoto hujambo? Yule mtoto alijibu mimi siyo mtoto ni Fulani. Kwa hiyo hata akiwa na mwenzake anajihisi yeye siyo mtu kiwango kile cha watoto kwa sababu anafikiria makubwa sana akili mwake.

SOMA; Huyu Ndiye Adui Namba Moja Kwenye Malezi Ya Watoto.

viii. Anakuwa anajielewa na kujitambua, kujitambua ni zawadi, ndiyo maana hata kuna watu mpaka sasa ni wakubwa lakini bado hawajajitambua ila watoto wenye uwezo mkubwa darasani huwa wanakuwa wanajielewa na kujitambua mapema sana. watakuwa wanafanya mambo ya ziada katika maisha yao na kushangaza jamii inayomzunguka.

ix. Pi, wanakuwa wabunifu sana, watoto wenye uwezo mkubwa ni watoto ambao wanakuwa wabunifu sana wa mambo hata wakishakuwa wakubwa katika maisha yao wanakuwa bado wana zile tabia. Mara nyingi kama tunavyojua ubunifu huleta furaha katika maisha kwa hiyo, watoto ambao wanakuwa wana ubunifu wa mambo wanakuwa na uwezo mkubwa.

x. Wanakuwa wana uwezo wa kujiamini, mtoto mwenye uwezo mkubwa yeye huwa anajiamini na kile anachokitenda na wala huwa haogopi watu kama akiamua kufanya jambo anafanya bila kuona aibu, wala nini. Mtoto unakuta ni mdogo lakini anakuwa anajiamini na vile anavyofanya yaani anakuwa yuko makini sana na akipewa nafasi ya kuongea utapenda jinsi anavyoelezea jambo kwa kujiamini.

Hatua ya kuchukua leo, leo mdadisi mtoto wako na kujua uwezo wake, huwezi kuzipata dalili zote kwa wakati mmoja na siyo lazima ziwe kama hizi ila anaweza kuonesha mambo mambo mengine zaidi ya haya kikubwa ni wewe kumgundua na kumlea katika malezi ya watoto wenye uwezo mkubwa yaani wenye vipaji vya asili.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com