Enzi za utawala wa Roma, wanafalsafa walikuwa wakipata shida kubwa sana ya kufukuzwa kwenye nchi zao na kwenda kuishi uhamishoni. Wengine walihukumiwa kufa kabisa.
Kwa watu wa kawaida, kwenda kuishi uhamishoni, sehemu ambayo hujaizoea na hakuna unayemjua, kunatosha kukuvuruga na kukuondolea furaha.

Lakini wastoa wote waliofukuzwa na kwenda uhamishoni, waliendelea kuwa na furaha.
Seneca anasema unapopelekwa uhamishoni, kinachobadilika ni mazingira tu, ila wewe unabaki yule yule. Akili yako ni ile ile, hivyo unao uhuru wa kuchagua namna gani unataka kuishi.
Seneca alipokuwa uhamishoni alitumia muda huo kujisomea, kuandika na kujifunza kuhusu asili. Na hili lilimwezesha kuwa bora zaidi na hata aliporudi kuweza kufanya makubwa zaidi.

Japo zama hizi wanafalsafa hawafungwi au kufukuzwa, bado tunahitaji kujifunza hili kwa sababu kuna nyakati kwenye maisha yako unaweza kujihisi kama upo uhamishoni. Labda umeoangiwa kazi eneo la mbali, ambapo maisha ni magumu. Au umeumwa na kulazwa hospitali.
Katika hali kama hizo, kutumia msingi huu wa ustoa kuendelea kutuliza akili zetu na kuwa na furaha, kutayafanya maisha yetu kuwa bora.