Kuiishi falsafa ya ustoa siyo kitu rahisi,
Kwanza kutokana na mazoea ambayo tayari tunayo, tunahitaji kubadili mengi tuliyokuwa nayo kwenye maisha na kubadili maisha yetu kwa ujumla. Na hakuna kitu kigumu kwa wengi kama wao wenyewe kuridhia kubadilika.
Pia ugumu unakuja pale wengine wanapokuchukulia kwamba falsafa yako ni ya ajabu. Utakaposema una falsafs ya maisha, au unaishi kwa falsafanya ustoa, wengi watakushangaa na huenda wakakutenga.

Wastoa wanatuambia japo inaonekana ni vigumu kuishi kwa falsafanya ustoa, ni vigumu zaidi kwa kuishi bila falsafa ya ustoa, au falsafa yoyote ya maisha.
Kwa sababu bila falsafa hakuna kikubwa utakachokuwa unafanya, utayumbishwa na kila kitu, utafanya mambo bila ya kujali umuhimu wake.
Falsafa ya maisha inakuwezesha kujenga nidhamu nzuri ya maisha.
Falsafa ya maisha inarahisisha maisha, hasa kwenye kufanya maamuzi. Unapokuwa na falsafa unayoiishi, inakuwezesha kufanya maamuzi bora.

Je ni zipi faida za kuishi kwa falsafa ya ustoa?
Zipo faida nyingi na hizi ni baadhi;
1. Kujijengea tabia na maadili mema kwenye maisha.
2. Kuwa na maisha yenye utulivu.
3. Kuwa na furaha muda wote wa maisha na siyo kusubiri mpaka upate kitu fulani.
4. Kutokukasirishwa au kuhuzunishwa na vitu tunavyokosa au kupoteza.
5. Kutokuweka utegemezi wa furaha kwenye kitu chochote.

Je tunawezaje kuvuka ugumu wa kuishi falsafa ya ustoa?
1. Kwa kuanza kuishi falsafa hii mara moja, kwa kuanza kufanya mazoezi ya ustoa na kuishi kwa misimamo ya ustoa.
2. Kuishi falsafa hii kwa ukimya, badala ya kumwambia kila mtu kwamba sasa wewe ni mwanafalsafs, unachagua kuishi falsafa na watu watajionea wenyewe.
3. Kutokuonekana wa ajabu sana kwenye jamii. Japo wastoa wa zamani walifanya mengi kwa falsafa hii, siyo lazima ufanye yote, hasa yale yatakayoifanya jamii ione una tatizo fulani.

Wakati wa kuanza kuishi falsafa ya ustoa, anasema Epictetus ni sasa. Usisubiri tena, anza kuishi falsafa hii nzuri leo hii.