Sisi binadamu hatupo hapa duniani peke yetu, tumezungukwa na wenzetu ambao wanaweza kuwa faida kwetu kwa upendo na urafiki. Pia watu hawa wanaweza kuwa chanzo cha hisia hasi kwetu kama hasira na wivu.
Watu wanaweza kufanya mambo ya kutuudhi au kushindwa kufanya mambo na ikapelekea sisi kuumia.

Marcus Aurelius anasema, binadamu tuna jukumu letu la msingi hapa duniani. Kama vile mti wa mwembe unavyotoa maembe, na mbwa anavyofanya kazi yake, basi hata sisi tuna kazi yetu.
Na Marcus anasema, jukumu letu ka msingi kabisa ni KUFIKIRI KWA USAHIHI. Binadamu sisi ni viumbe wa kufikiri, na fikra zetu ndiyo zinatengeneza maisha yetu.
Baada ya kufikiri sahihi na kwa kina, tunaweza kujua mchango wetu hapa duniani ni upi.

Marcus anasema kila siku utakutana na watu wabinafsi, wenye roho mbaya na chuki, hivyo jiandae ili usiumizwe.
Lakini pia anatusisitiza kuwa na mchango bora kwa wengine, kwa sababu kwa kufanya hivyo ndiyo tunakuwa na maisha mazuri.

Kwa kifupi, falsafa ya ustoa inatutaka kujua kusudi la maisha yetu na kulitimiza. Tutumie muda wetu mwingi kwenye kufanya kile ambacho ni muhimu kwetu kufanya, ili kuweza kutoa mchango na thamani kwa wanadamu wenzetu.
Tusipoteze muda kufanya ili kuonekana, au kutaka kusifiwa, bali sisi tufanye kwa sababu ndiyo jukumu letu. Kama ambavyo mti wa embe utazaa embe kila msimu hata kama hautasifiwa, basi na wewe fanya kazi yako kila siku bila ya kuangalia unasifiwa au la.

Kuwa na mapenzi kwa watu na utu, toa mchango bora kwa wengine kupitia kile unachofanya.