Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?
Umeianzaje siku hii nzuri sana ya leo?
Hii ni nafasi nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa.

IMG_20170102_073855
Ni kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana leo na kila siku.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu LEVEL UP…
Maisha ni kama ngazi isiyo na mwisho, na jukumu letu ni kupanda ngazi hiyo mpaka pale ambapo tutafikia. Kadiri unavyopanda ngazi hii ndivyo unavyozidi kufanikiwa.
Kila kitu kwenye maisha tunaanzia chini kabisa, halafu tunapanda ngazi hatua kwa hatua mpaka pale tunapofikia.

Sasa yapo haya muhimu sana kujua kuhusu ngazi hii ya maisha.
1. Waliofanikiwa wamepanda sehemu kubwa ya ngazi hii kuliko wengine.
2. Walioshindwa na wenye maisha ya kawaida wamekwama kwenye ngazi za chini, wameamua wasipande tena.
3. Kila ngazi inachangamoto yake, na huwezi kuvuka ngazi moja kwenda nyingine kama utashindwa kutatua changamoto uliyonayo kwenye ngazi ukiyopo.
4. Kadiri unavyokwenda juu kwenye ngazi, ndivyo msongamano unavyopungua, hewa inakuwa safi na unaona vizuri maisha.
5. Hakuna lift ni lazima kila mtu apande ngazi hii.

Popote ulipo sasa kwenye maisha yako, jua ni ngazi fulani, na siyo mwisho hata kama umeridhika kiasi gani.
Kipo kitu unaweza kujifunza ambacho hukujua,
Kipo kitu unaweza kuboresha zaidi ya unavyofanya sasa.
Ipo thamani unaweza kuongeza zaidi.
Na yapo maisha ya wengine unayoweza kuyagusa zaidi.

LEVEL UP, PANDA NGAZI NA MAISHA YAKO YATAZIDI KUWA BORA ZAIDI.

Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.