Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni fursa ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa kwenye kazi na biashara zetu, ili tuweze kupata matokeo bora kabisa.

Msingi wetu mkuu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KIKOMBE CHA BABU….
Najua unajua kuhusu kikombe hichi na namna kilivyopata umaarufu hapa nchini, namna ambavyo watu walijipanga kwenye msafara wa magari kwenda kukipata kikombe. Namna ambavyo watu walikimbia mahospitali kwenda kupata uponyaji huu wa MARA MOJA.
Kikombe hichi kilipata umaarufu kutokana na urahisi wake, KWAMBA UKINYWA TU KIKOMBE, MATATIZO YAKO YOTE YAMEKWISHA. Na watu waliamini hilo.
Ilikuwa ni hali ya kushangaza, kuchekesha na kuhuzunisha kwa wakati mmoja.
Sasa unaweza kufikiri kwamba zama hizo za kikombe zilishapita na sasa huwezi kudanganyika tena.
Lakini nataka nikuambie unajidanganya, yapo mengi unayofikiria kwa mfumo wa kikombe cha babu ila tu majina ndiyo yanatofautiana.
Chochote kile unachofikiri unahitaji kufanya kitu kimoja tu na kupata, ni aina ya kikombe cha babu.
Kwamba unahitaji njia moja tu ndiyo ufanikiwe,
Au unahitaji siri moja tu biashara yako ifanikiwe,
Au unahitaji kumeza kidonge tu uzito wako upungue,
Au unahitaji maombi tu uagane na umasikini.
Chochote unachofikiria unahitaji ili kupiga hatua, lakini HUTAKI KUWEKA KAZI, hiyo ni aina yako ya kikombe cha babu.
Chochote muhimu unachohitaji kwenye maisha yako, kimetenganishwa na wewe kwa KAZI. Hivyo unahitaji kuweka kazi nzito ili uweze kukipata. Akitokea mtu na kukuambia ipo njia ya mkato, ya kupata unachotaka bila kuweka kazi, kimbia haraka, anakuletea KIKOMBE CHA BABU.
FANYA KAZI, WORK HARDER, Siwezi kusisitiza hilo zaidi ya hapo.
Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.