Biashara nyingi zimekuwa ni maboresho ya biashara ambazo tayari zipo. Yaani kama sasa kuna magari, basi watu wanaofungua kampuni mpya za magari wanaangalia kinachofanyika sasa na kuboresha zaidi. Lakini hivi sivyo dunia inavyopaswa kwenda, kwa sababu kama dunia ingeenda hivi tangu zamani, leo hii tusingekuwa na kompyuta, tusingekuwa na tv, redio wala hata magari. 

Kwa sababu kwenye usafiri, ambacho watu wangefanya ni kuboresha zaidi usafiri wa punda au farasi.

Dunia inasonga mbele pale panapokuwa na uvumbuzi wa vitu vipya na njia mpya za kufanya mambo. Hapa ndipo tunapopata bidhaa mpya ambazo tunazitumia na kufanya maisha yetu kuwa bora zaidi.

Kuboresha kile ambacho tayari kipo ni kutoka moja na kwenda namba nyingine nyingi. Lakini kuleta kitu kipya ambacho hakijawahi kuwepo, ni kutoka sifuri na kwenda moja.

Mjasiriamali na mwekezaji Peter Thiel katika kitabu hicho cha ZERO TO ONE, anatufundisha namna tunavyoweza kutoa sifuri mpaka moja, ambapo tunaleta vitu vipya na kuitengeneza kesho mpya na bora zaidi.

Karibu kwenye uchambuzi huu wa kitabu ili uweze kujifunza na kuona hatua zipi uchukue ili uweze kuanza biashara ya tofauti ambayo italeta mabadiliko makubwa kwa wengine pia.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kumudu Kuondoa Hofu Zako Za Kesho, Zinazokusumbua Na Kukutesa.

1. Kila wakati kwenye biashara ni wakati wa kipekee, unaotokea mara moja na haujirudii tena. Kulikuwa na wakati mmoja tu ambapo Bill Gates alianzisha kampuni ya Microsoft, kulikuwa na wakati mmoja tu Zuckerberg alianzisha Facebook. Hivyo nyakati zijazo zitakuja na vitu vipya na siyo hivi tena. Hivyo kama umejifungia mahali na unaiga kile ambacho watu hawa walifanya huko nyuma, unapoteza muda wako na hakuna unachojifunza kupitia wao. Ni rahisi kuiga na kuboresha ambacho tayari kinafanyika, lakini kutengeneza kitu kikubwa, unahitaji kufanya kitu kipya kabisa.

2. Tofauti ya teknolojia na utandawazi.
Watu wengi wanaosikia neno teknolojia moja kwa moja wanafikiria kompyuta na mtandao wa intaneti. Na wanaposikia utandawazi wanafikiria uhuru wa watu kuwasiliana na kufanya biashara bila ya kujali mipaka. Lakini hizi siyo maana halisi.

Teknolojia ni pale jambo jipya kabisa linapofanyika, hapo ni kutoka sifuri kwenda moja.

Utandawazi ni kuboresha yale ambayo tayari yanafanyika. Iwe ni ndani ya nchi moja au nchi nyingine.

Utandawazi unarahisisha kusambaa kwa teknolojia ambayo tayari imeshavumbuliwa, na teknolojia inaleta vitu vipya kwenye dunia.

3. Hakuna kanuni moja na ya uhakika ua ujasiriamali ambayo ukiifuata basi utaweza kuja na uvumbuzi mpya. Hii ni kwa sababu vipo vitu vingi vinavyochochea kupatikana kwa uvumbuzi mpya kwenye biashara na ujasiriamali. Lakini kitu kimoja kinachowawezesha wale wanaokuja na uvumbuzi mpya, ni kufikiri tofauti na wengine wanavyofikiri. Wanafikiri kama kitu kisingekuwepo. Hawaangalii namna ya kuboresha, wanaangalia namna ya kuja na kitu bora zaidi.

4. Hakuna mtu yeyote anayeweza kuitabiri kesho kwa uhakika wa asilimia 100, lakini tunajua mambo mawili kwa hakika kuhusu kesho; itakuwa tofauti na ilivyo leo na lazima tuitengeneze kesho leo. Hivyo kesho yetu lazima tuitengeneze leo, kwa kufikiri njia bora zaidi za kupambana na matatizo tuliyonayo leo, na yatakayoweza kujitokeza kesho.

5. Vizazi vilivyopita hapa duniani, vimekuwa na ndoto za kuwa na maisha bora zaidi, wamekuwa wakifikiria maisha kuwa mazuri kuliko siku za nyuma. Lakini kwa miaka 50 iliyopita, eneo pekee ambalo limeshuhudia mapinduzi makubwa ni kompyuta na mtandao. Maeneo mengine bado yapo duni sana, japo ni muhimu. Ambacho kimekuwa kinafanyika ni kuboresha kile ambacho tayari kipo. Hii ni fursa nzuri kwetu kuweza kuangalia namna ya kuja na njia bora zaidi kwenye maeneo mengine ya maisha yetu.

6. Unapoona watu wengi wanakimbilia kufanya kitu cha aina moja, hata kama kinalipa sana, jua kuna janga linakuja kutokea mbeleni. Hili lilidhibitishwa mwaka 1999 ambapo kila mtu alikuwa anakimbilia kuwekeza kwenye mtandao wa intaneti, kitu ambacho kilipelekea anguko kubwa la biashara za mtandao wa intaneti. Pia hili lilipelekea anguko kwenye uwekezaji wa majengo mwaka 2008 ambapo kila mtu alikuwa anakimbilia kuwekeza kwenye majengo. Unahitaji kufikiria tofauti na wengi wanavyofikiri ili kuweza kuja na mawazo tofauti na bora ya kibiashara.

7. Ushindani na kujitofautisha.
Watu wengi wanapoingia kwenye biashara, huangalia namna gani wanaweza kuendana na ushindani. Wachumi wanasema ushindani ni muhimu ili kuwa na mzunguko mzuri wa biashara. 

Lakini kwa uhalisia, ushindani hauna faida yoyote kwenye biashara. Makampuni yote makubwa na yanayotengeneza faidia hayashindani, badala yake yanajitofautisha. Yanatafuta kitu cha tofauti ambacho hakuna mwingine anayeweza kufanya na wanakifanya vizuri.

SOMA; Haya Ndiyo Mambo Yanakukwamisha Na Kukufanya Ushindwe Kufikia Malengo Yako Uliyojiwekea.

8. Biashara kubwa na zinazotengeneza faida kubwa huhakikisha jambo moja, zinahodhi soko lake. Zinahakikisha zinachagua soko ambapo zitatawala zenyewe bila ya ushindani. Zinajipa nafasi ya kupata wateja wa kutosha kwa muda mrefu, kupanga bei zao wenyewe na kupata faida kubwa. Unapofikiria kuanza biashara kubwa na ya tofauti, tafuta soko ambalo unaweza kulitawala wewe mwenyewe na wengine washindwe kabisa kuingia. Kitu pekee kitakachokupa nafasi hiyo bila ya kuvunja sheria ni kuwa na teknolojia ya tofauti kabisa ambayo wengine bado hawajaijua.

9. Tatizo kubwa la ushindani ni faida kuwa ndogo na utaji wa huduma kuwa mbovu zaidi kadiri faida inavyokuwa ndogo. Kwa mfano kama mtu ameenda kufungua mgahawa eneo lenye migahawa mingi, huna kikubwa cha kujitofautisha. Hivyo kinachobaki ni watu kuanza kupunguza bei ili kupata wateja zaidi. Wanapopunguza bei faida inakuwa ndogo sana na wakati mwingine hakuna kabisa, hivyo kufidia hilo wanapunguza gharama za uendeshaji na hivyo kuajiri watu watakaowalipa mshahara kidogo. Hili linapelekea huduma kuwa mbovu na mwishowe kukosa wateja na biashara kufa. Usiingie kwenye biashara ambayo huwezi kujitofautisha, utaishia kuumia kichwa.

10. Thamani ya biashara leo ni jumla ya fedha zote ambazo biashara itatengeneza kwa siku zijazo na siyo pesa inayotengeneza kwa sasa. Ukiangalia biashara nyingi, sasa zinaweza kuwa zinatengeneza fedha nyingi, lakini ukiangalia miaka 10 au 20 ijayo, huoni uwepo wa biashara hizi. Lakini biashara zinazotokana na teknolojia mpya, zinaweza zisiwe zinatengeneza fedha leo, ila ukiangalia miaka 10 ijayo, zinakuwa zinatengeneza fedha nyingi. Hivyo usikate tamaa pale 
unapoanzisha biashara na ikawa haitengenezi fedha nyingi mwanzoni.

11. Ili kampuni iwe na thamani kubwa, lazima iwe inakua na pia lazima iweze kudumu kwenye nyakati ngumu. Watu wengi hufanya makosa ya kuangalia mapato ya muda mfupi, na kushindwa kuangalia ukuaji wa biashara na uwezo wa kustahimili kwa kipindi kirefu. Unapoanza biashara, au biashara yoyote unayofanya, angalia fursa za ukuaji na uwezo wa kustahimili changamoto mbalimbali.

12. Tabia nne za biashara inayohodhi soko lake yenyewe, ambayo haina ushindani wa aina yoyote.

Sifa ya kwanza ni kuwa na teknolojia mpya ambayo wengine hawana. Hivyo kama huna teknolojia uliyovumbua, huwezi kuhodhi soko, chochote ulichoiga wengine pia wanaweza kuiga na kuwa washindani wako.

Sifa ya pili ni uwezo wa kutengeneza mtandao. Kadiri watu wengi wanaotumia kitu wanawaambia wengine nao watumie, ndivyo biashara hiyo inavyohodhi soko. Unapokuwa na mtandao mkubwa wa watu, unakuwa umehodhi sehemu kubwa ya soko.

Sifa ya tatu ni uwezo wa kukua. Biashara inayohodhi soko, inazidi kuimarika kadiri inavyokua. Inaweza kuanza na wateja wachache na kuendelea kuongeza wateja kadiri siku zinavyokwenda na mwishowe ikawa imehodhi sehemu kubwa ya soko.

Sifa ya nne ni jina (brand) la biashara. Kadiri jina la biashara linapokuwa kubwa ndivyo biashara inavyojikita kwenye kuhodhi soko lake. Kwa mfano zipo kampuni nyingi za kutafuta vitu kwenye mtandao, google, yahoo, bing, microsoft na nyingine nyingi. Lakini mtu akitaka kukuambia utafute kitu atakuambia hebu kigoogle, google ni brand kubwa inayohodhi soko la kutafuta vitu kwenye mtandao wa intanet, pia wana teknolojia inayoleta majibu haraka na kwa usahihi mkubwa.

SOMA; Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Kinachoitwa LETTERS From A SELF-MADE MERCHANT To His SON.

13. Unawezaje kuhodhi soko unaloingia? Anza kidogo na kua kumeza soko lote. Watu wengi wanapotaka kuhodhi soko, huanza kuangalia ukubwa wake na kufikiria wanahodhi vipi, hii inakuwa ngumu na hata wakijaribu wanaishia kushindwa. Lakini wanaohodhi huwa wanaanza na soko dogo, halafu wakishalihodhi wanasonga mbele zaidi. Baada ya muda unakuta wameteka sehemu kubwa ya soko. Ni rahisi sana kuanza kidogo na kuhodhi soko dogo kisha kwenda soko kubwa zaidi.

14. Unapoanza, usijaribu kuvuruga soko. Wajasiriamali wengi wapya wanapoingia kwenye soko jipya, huwa wanajinadi kama wavurugaji, wanaokuja kuleta vitu vipya na bora zaidi. Kelele hizi huwaamsha wengi na kuleta ushindani usio wa lazima. Unapochagua soko na kuliendea taratibu, unapata nafasi ya kukua bila ya kubughudhiwa. Kila anayekuona ukianza kidogo hapati wasiwasi kwa sababu haoni tishio lako, wanapokuja kustuka umeshateka soko zima.

15. Mtazamo wa watu kuhusu kesho pia una mchango kwenye maamuzi yao ya kibiashara. Kuna watu ambao wanaiona kesho kama kitu cha uhakika na hivyo kupanga na kuchukua hatua leo ili kesho iwe vile wanavyotaka iwe. Na wapo wengine ambao wanaichukulia kesho kama isiyo ya uhakika, na hivyo kushindwa kupanga chochote kwa sababu hawana uhakika kipi kitatokea. Bila ya kuwa na mipango bora ya kesho, hakuwezi kuwepo na teknolojia.

16. Wale ambao wanaiona kesho kama isiyo ya uhakika, hukazana kufanya mambo mengi kwa kuamini kwamba hata kama yatashindikana yapo ambayo yatawezekana. Kwa njia hii wanaikuta wanafanya mambo mengi, ambayo hayana uzalishaji kwao na mwishowe kushindwa kupata chochote. Unapoanzisha biashara yako, ione kesho yako kuwa ya uhakika, na chagua kufanya kile ambacho kitaiwezesha kesho yako kuwa bora zaidi. Usihangaike na mengine ambayo siyo muhimu.

17. Hali ya kutokuwa na uhakika wa kesho kwenye fedha imetengeneza majanga makubwa sana. Kwa sababu mtu anaweza kuanzisha biashara yake, akapata faida kubwa, kwa kuwa hana uhakika na kesho, asijue nini cha kufanya na fedha hizo, hivyo akaziweka benki. Benki nayo inakuwa haina uhakika ifanye nini na fedha hizo hivyo kuwakopesha wafanyabiashara wengine. Wafanyabiashara hao pia wanaweza wasiwe na uhakika na wafanye nini na fedha hizo, wanakwenda kuwekeza kwenye hisa za biashara nyingine. Mzunguko unakwenda hivi na hakuna thamani kubwa inayozalishwa.

18. Katika kuanzisha na kuendesha biashara ambayo italeta mapinduzi makubwa, unahitaji timu ya watu ambao wamejitoa kweli. Watu ambao wana mchango mkubwa kwenye kile mnachofanya, na pia wanaelewa maono ambayo wewe mwanzilishi unayo. Ikitokea hawaelewi maono yako, hawataweza kuweka juhudi kama unazoweka wewe. Hivyo hakikisha una maono makubwa ya biashara yako na kila anayehusika pale anayajua vizuri.

19. Unapoanzisha biashara au kampuni yako, jua sheria ya nguvu ya umoja. Sheria hii inasema kwamba unapofanya kitu kimoja, kina nguvu zaidi kuliko kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja. Hivyo kuchagua kitu kimoja unachoweza kufanya vizuri ni bora zaidi. Kuchagua soko moja la kuanza nalo unaweza kulitawala na kulihodhi vizuri.

20. Swali muhimu sana kujiuliza na kujipa jibu kabla ya kuanzisha biashara yoyote mpya ni hili; je ni siri gani ambayo watu bado hawajaijua? Je ni kitu gani ambacho watu hawakubaliani nacho ila wewe unakubaliana nacho? Ni fikra za aina hii ndiyo zinaleta teknolojia mpya mara zote. 

Kufikiria na kufanya kile ambacho kila mtu anafanya, utafanya kile ambacho kila mtu anafanya, labda kwa ubora zaidi. Lakini kufikiria kile ambacho hakuna anayefikiria, kutakuwezesha kuja na kitu kipya kitakachokuwezesha kutengeneza soko lako na kulihodhi.

Haya ni yale muhimu sana kuhusu kuanza biashara ya kutoka sifuri mpaka moja, yaani kuanza biashara ambayo haijawahi kufanywa popote duniani. Hii ni njia ambayo inaleta teknolojia mpya duniani. Japo siyo teknolojia zote zinapona, zile ambazo ni muhimu zimeweza kuyafanya maisha kuwa bora zaidi hapa duniani.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita