Hongera rafiki yangu kwa siku hii nzuri sana ya leo.
Ni ile siku ambayo jana ulisema kesho nitafanya,
Nakukumbusha tu jana ndiyo leo, hivyo fanya, usiseme tena kesho, maana kesho huwa hazifiki.

Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu; KAMA HUTAKI KUFA, TUMA UJUMBE HUU KWA WATU 10.
Kuna jumbe nyingi za aina hii unatumiwa mara kwa mara, huenda hazina masharti makali kama yangu (kuhusu kufa), lakini zinakushurutisha kwamba lazima utume ujumbe huo kwa idadi fulani ya watu ndiyo uwe mtu mwema.
Ili kuhakikisha zinawateka watu na kusambaa, jumbe hizi huwa zinabeba maneno na picha za dini, watu wenye shida na wanaoumwa.
Jumbe hizi huwa zinaishia na maneno kama haya;
1. Wenye roho mbaya hawatatuma ujumbe huu kwa watu 10…..
2. Kama unamkubali Yesu kuwa mwokozi tuma ujunbe huu kwa watu 15….
3. Tuma ujumbe huu kwa watu 5 ili kumwaibisha shetani….
4. Andika Amen ili mtu huyu apone…
5. Tuma ujumbe huu kwa watu 7 na ndaninya siku 7 utapata muujiza….
6. Waliotuma ujumbe huu kwa watu 10 walipata baraka, waliopuuza walipata mkosi….
7. Tuma kuokoa maisha ya wengine….
Na kadhalika.
Sasa rafiki, hizi ni jumbe za kijinga, kama kweli utatuma, na ni jumbe za kukunyanyasa kisaikolojia, kukushurutisha ufanye kitu ambacho hujui kwa nini unafanya.
Ni ujinga kwa sababu kwa wewe kutuma tu ujumbe huwezi kupata chochote kile ambacho unakitaka.
Hata kama umeambiwa ukituma ujumbe utaenda mbinguni, mbingu siyo rahisi hivyo, vinginevyo kila mtu angetuma ujumbe na kusubiri kuingia mbinguni.
Ni unyanyaswaji wa kisaikolojia kwa sababu unapewa masharti ambayo kuyakiuka unajisikia vibaya. Hivyo unaona bora ufanye tu kwa sababu hakuna unachopoteza kwa kufanya.
Sasa rafiki yangu, napenda kukuambia, KAMWE, usitume ujumbe ambao chini yake umeshurutishwa kutuma kwa idadi fulani ya watu. Tuma ujumbe kwa sababu umekugusa na kuna kitu umejifunza na ungependa wengine nao wajifunze. Lakini ukishaambiwa tuma kwa watu sijui wangapi, achana nao, hata kama ni mzuri.
Kusisitiza zaidi, ukipokea ujumbe wowote ambao una dalili hizo, angalia kwanza pale mwisho wa ujumbe, ukiona pameandikwa tu TUMA KWA WATU…, wala hata usiusome, ufute haraka na endelea na yako.
Usikubali watu wakunyanyase kisaikolojia,
Usikubali watu wakutumie hovyo tu.
Usikubali kutuma ujumbe wowote ulioambiwa tuma kwa idadi fulani ya watu.
Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT.